in , , ,

TFF, serikali wazikamua klabu

Rais wa TFF, Leodgar Tenga

Kile  kilico cha klabu dhidi ya makato makubwa dhidi ya mapato yatokanayo na mechi za ligi na hasa zinazochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kimeibuka tena ambapo baadhi ya klabu zimedai kuwa ‘zinakamuliwa’ sana na kurudishwa nyuma kiuchumi.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya viongozi wa klabu za ligi kuu wamesema kumekuwa na makato makubwa yanayotokana na taratibu zinazobarikiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na pia serikali inayoumiliki Uwanja wa Taifa.

Katibu mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema kuwa kumekuwa na idara nyingi zinazopata pesa kirahisi kutokana na makato hayo huku klabu ambazo hubeba gharama kubwa za maandalizi ya timu zikiambulia ‘senti’ kidogo mno kulinganisha na fedha zinazopatikana.

“Uwanja wa Taifa una idara nyingi mno ambazo zinatakiwa kulipiwa kila unapotumika. Kuna ulinzi, usafi, umeme, maandalizi na vingine vingi tu… lakini ukiviangalia vizuri, utabaini kuwa vingi vinafanana,” alisema Mwalusako.

Mwalusako aliitaka serikali na TFF kuangalia mfumo wa makato hayo ili kuondokana na utaratibu wa sasa ‘unaozikamua’ klabu na kuziacha zikitaabika kiuchumi.

Mratibu wa Mtibwa Sugar Jamal Bayser aliiambia NIPASHE jana kuwa makato viwanjani ni mengi mno na kuwakwaza kiuchumi, hivyo akazitaka klabu kuungana ili kulipatia ufumbuzi suala hilo ambalo limekuwa tatizo kubwa kwa maendeleo ya klabu za soka nchini.

Akitolea mfano wa mechi ya Simba na JKT Oljoro iliyochezwa Jumapili kwenye Uwanja huo na kuingiza sh. milioni 46.68 huku kila timu ikipatiwa mgawo wa sh. million 8.2 baada ya makato, Bayser alisema serikali na TFF ndiyo wamekuwa wakinufaika zaidi na mechi zinazochezwa si katika uwanja huo tu, bali hata kwenye viwanja vingine.

Meneja wa Azam, Patrick Kahemela alisema klabu zenyewe ndizo zinapaswa kujilaumu kwa kuipa madaraka makubwa TFF katika kupanga gharama za tiketi, kiingilio na makato mengine ya gharama za mechi husika; hali ambayo mwishowe huwaacha wakiambulia fedha kidogo mno kutokana na mapato ya milangoni.

“Haya yote yanatokea kwa sababu mwanzo wetu haukuwa mzuri. Klabu hazina umoja. Kama tungeungana katika hili, kusingekuwa na malalamiko,” alisema Kahaemela.

“Sisi (Azam) tunaomba Uwanja wa Taifa utumike kama sehemu ya huduma za jamii badala ya biashara kama inavyoonekana sasa,” aliongeza.

“Vitabu vya tiketi za uwanjani viko TFF na klabu hazioneshwi, kuna gharama za waamuzi, ulinzi, gharama za mchezo, maandalizi ya uwanja, gharama za mchezo, pesa ya Kamati ya Ligi. Katika hali kama hii tunategemea klabu itanufaika na kiingilio cha mechi.”

Mmoja wa wamiliki wa klabu ya African Lyon, Rahim Kangezi alisema wamekuwa wakisikitishwa na hali ya makato inayofanywa na TFF na serikali dhidi ya klabu za Ligi Kuu.

Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema klabu yao pia imekuwa ikiathiriwa na makato makubwa, lakini Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ndiye mwenye mamlaka ya kulizungumzia kwa kina suala hilo. Kaburu hakupatikana jana.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari hivi karibuni, Rais wa TFF, Leodgar Tenga alisema kuwa makato yote katika kila mechi yanafuata sheria na taratibu zilizopo.

Picha halisi itokanayo na kilio cha klabu inajionyesha katika makato ya mechi ya Simba na JKT Oljoro iliyoingiza Sh. milioni 46.68 kama kama ifuatavyo:

Kila klabu ilipata Sh. milioni 8.2, VAT Sh. 7,120,677.97, posho ya msimamizi wa kituo Sh. 120,000, kamishna wa mechi Sh. 193,000, waamuzi Sh. 210,000, mwamuzi wa akiba (reserve referee) Sh. 70,000, usafi na ulinzi wa uwanja Sh. 2,350,000 na Wachina (Stadium Technical Support) Sh. 2,000,000.

Makato mengine ni gharama za umeme Sh. 300,000, maandalizi ya uwanja Sh. 400,000, ulinzi Sh. 3,500,000, tiketi Sh. 3,175,000, gharama za mchezo Sh. 2,724,132.20, uwanja Sh. 2,724,132.20, Kamati ya Ligi Sh. 2,724,132.20, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) Sh. 1,634,479.32 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Sh. 1,089,652.88.

Simba na Yanga ziliwahi kutishia kutocheza tena kwenye Uwanja wa Taifa kuepuka makato makubwa misimu kadhaa iliyopita na Serikali iliwapoza kwa kuahidi kushughulikia suala hilo.

CHANZO: NIPASHE

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

NMB yadhamini Gofu….

KUFUZU KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA