Diego Costa kamili Chelsea
*Barca wamtaka Suarez, Liverpool Balotelli
*Man U wamtaka Hummels, Atletico Michu
Chelsea wamethibitisha kufikia makubaliano na Atletico Madrid kumsajili mshambuliaji wao namba moja, Diego Costa.
Jose Mourinho amemchukua Costa kwa pauni milioni 32 huku akitangaza kumwacha Samuel Eto’o aliyemaliza mkataba wake.
Costa (25) amechezea klabu za Braga, Penafiel, Celta Vigo, Albacete, Real Valladolid, Rayo Vallecano na sasa Atletico akicheza mechi 94 La Liga.
Ni mzaliwa wa Brazil lakini aliikana nchi hiyo na kujiunga na Timu ya Taifa ya Hispania baada ya kupata uraia kutokana na kuishi humo kwa zaidi ya miaka mitano. Msimu uliopita alifunga mabao 27 kwenye ligi, moja nyuma ya Lionel Messi na manne nyuma ya Cristiano Ronaldo na aliwawezesha Atletico kutwaa ubingwa wa nchi.
Costa atasaidia kuimarisha safu ya ushambuliaji iliyokuwa butu sana chini ya Eto’o, Fernando Torres na Demba Ba ambapo mabao mengi yalifungwa na viungo.
Atletico Madrid wanataka kumsajili mshambuliaji wa Swansea, Michu, ambaye atawaeleza Swansea karibuni juu ya nia yake ya kurudi nyumbani Hispania.
Barcelona wameanza mazungumzo na Liverpool kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wao, Luis Suarez aliyefungiwa kwa miezi minne kutokana na kumng’ata Giorgio Chiellini wa Italia.
Maofisa wa klabu mbili hizo wanakutana jijini London leo kufanyia kazi uhamisho huo, ambapo Liverpool wanatarajiwa kudai pauni milioni 80 waliyemsajili 2011 kutoka Ajax kwa pauni milioni 22. Barca wapo tayari kutoa pauni milioni 60.
Barca wanaweza kutoa fedha kidogo zaidi iwapo Liverpool watakubali kumchukua winga wao, Alexis Sanchez anayewaniwa na Arsenal na Manchester United.
Liverpool wanafikiria kumsajili mpachika mabao wa AC Milan, Mario Balotelli iwapo watampoteza Suarez. Tayari wamewasajili Rickie Lambert na Adam Lalana.
Kocha Brendan Rodgers wa Liverpool anataka kumsajili beki wa Southampton, Dejan Lovren katika mwendelezo wa kuwabomoa Saints.
Southampton wamekubali kutoa dau la pauni milioni 10 kumnasa winga wa FC Twente ya Uswisi, Dusan Tadic kuziba pengo la Lallana.
Wakala wa kipa matata wa mexico, Guillermo Ochoa amesema amepokea maombi ya kumsajili mchezaji huyo huru lakini bado hajapewa ofa za kueleweka. Liverpool wanamtaka, huku Arsenal wakitajwa pia.
Manchester City wamekaribia mwafaka kumsajili beki wa kati wa Roma, Mehdi Benatia lakini itabidi wasubiri hadi klabu hiyo ipate mbadala wake.
Arsenal wanafikiria kumsajili winga wa Napoli, Lorenzo Insigne.
Manchester United wamejiandaa kutoa pauni milioni 20 kumsajili beki wa Borussia Dortmund, Mats Hummels.
Bosi mpya wa Manchester United aliye bado na Uholanzi nchini Brazil, Louis van Gaal ana matumaini ya kuafikiana na Arsenal ili wamsajili beki wao wa kati na nahodha, Thomas Vermaelen kisha akutane na Feyenoord kuwapoka beki mwingine wa kati, tefan de Vrij.
Real Madrid wanataka kumuuza Angel Di Maria ili wamsajili nyota wa Colombia, James Rodriguez. Arsenal wanamtaka Di Maria.
Mchezaji mwingine wa Colombia anayechezea Porto ya Ureno, Jackson Martinez amesema angependa kujiunga na Arsenal, klabu aliyoshabikia akiwa mtoto.
Arsenal na Liverpool wanapigana vikumbo kupata saini ya kipa wa Costa Rica, Keylor Navas.
Comments
Loading…