Anasema anachia ngazi kwa vile Chama cha Soka cha England (FA) kinaendeleza mashitaka dhidi yake kuhusu kumtukana kibaguzi Anton Ferdinand wa Queen Park Rangers (QPR).
Terry aliyepata kuwa nahodha wa taifa, aliyechezea kikosi chake mara 78 katika miaka tisa, amefadhaishwa na kuendelea kushitakiwa licha ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Westminster kumsafisha Julai mwaka huu.
Anaachana na soka ya kimataifa katika ngazi ya taifa akiwa na umri wa miaka 31, lakini anabaki nahodha wa mabingwa wa Ulaya, Chelsea.
“Ninavyoona ni kwamba, FA kuendelea na mashitaka yake dhidi yangu wakati nimeshasafishwa na mahakama kunanifanya nishindwe kuendelea kuchezea timu ya taifa,” anasema Terry.
Terry alizaliwa Desemba 7, 1980 jijini London na alianza kuichezea timu ya taifa Juni 2, 2003 dhidi ya Serbia & Montenegro.
Agosti 15, 2004 alichukua nafasi ya Mfaransa Marcel Desailly kama kiungo wa Chelsea wakati Agosti 2006 alichukua nafasi ya kudumu ya David Beckham ya unahodha kwenye timu ya taifa.
Hata hivyo, Februari 5, 2010 alivuliwa unahodha wa England baada ya kutuhumiwa kutembea na rafiki wa kike wa zamani wa mchezaji mwenzake wa timu ya taifa, Wayne Bridge.
Machi mwaka jana alirejeshewa unahodha na Capello kabla ya kupokonywa tena Desemba, kitendo kilichosababisha kocha Fabio Capello kujiuzulu. Terry alianza kukabiliwa rasmi na tuhuma hizi Machi mwaka jana na Desemba ilitangazwa rasmi kwamba angeshitakiwa.
Licha ya kusafishwa na mahakama Julai, FA iliendelea na uchunguzi na hatimaye mashitaka dhidi ya Terry, ndipo baada ya kutafakari akaamua kung’atuka.
Pamekuwapo malalamiko dhidi ya kuteuliwa kwake kwenye timu ya taifa wakati akikabiliwa na tuhuma na hatimaye kesi kortini.
Wapo waliodhani ilikuwa bora zaidi kwa beki wa Manchester United, Rio Ferdinand (kakaye Anton Ferdinand) kupewa nafasi hiyo, lakini kocha wa sasa wa England, Roy Hodgson amekuwa akimteua, lakini si kumpa unahodha.
Hata hivyo, uamuzi wa Mahakama kutomtia hatiani Terry ulipokewa kwa hisia tofauti, baadhi wakidai ushahidi wa yeye kutukana ulikuwa bayana.
Kabla, katika na baada ya kesi, Terry amekuwa akikana kumtukana Ferdinand, ambapo timu zao zilipokutana hivi karibuni, Ferdinand alikataa kumpa mkono Terry na Ashley Cole aliyemtetea Terry mahakamani.
Kakaye Anton, yaani Rio, alimfananisha Cole anayechezea Chelsea na barafu iliyopakwa rangi tofauti na iliyo halisi ndani mwake. Rio aliadhibiwa na FA kwa kutozwa faini.
Ofisa Mtendaji wa Chama cha Wacheza Soka wa Kulipwa (PFA), Gordon Taylor alinukuliwa akisema sura ya soka iliathiriwa vibaya na sakata hilo na kutaka kampeni ya ‘Respect’ ienziwe.
Katika kuaga kwake wakati wa kuiacha timu ya taifa, Terry anasema tangu akiwa kijana aliota kulichezea taifa na kuwa nahodha wa timu yake, jambo analosema ni heshima kubwa.
Anasema kwamba sasa anajiwinda zaidi kufanya vizuri na klabu yake ya Chelsea katika ligi ya ndani na mashindano ya kimataifa.
Comments
Loading…