Wakati sakata la wizi wa tiketi likizidi kupamba moto kwa washukiwa kutiwa mbaroni na kuhojiwa na Polisi, Katibu Mwenezi wa klabu ya Simba, Said Rubeya ‘Seydou’ ameibuka na kumtaka Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Leodger Tenga kuvunja ukimya.
Akizungumza na Nipashe jana, Seydou, alisema pamoja na kufahamu Tenga hana ajualo katika vitendo hivyo vya wizi wa tiketi, lakini ni vema kama raisi wa shirikisho hilo kutoa kauli yake ili kumweka salama mbele ya wadau wa soka nchini.
Seydou alisema ukimya wake katika kipindi hiki kinaweza kumchafua kwa vile wadau wa soka tayari wameshaanza kukosa imani na shirikisho hilo kufuatia baadhi ya maafisa wake kutajwa kwenye sakata hilo.
“Kama mdau wa soka na ambaye nimekuwa nikilalamika mara kwa mara juu ya kuwepo kwa hujuma ya fedha za umma katika michezo, namuomba Tenga avunje ukimya na kuwatoa wasiwasi wadau walioingiwa na mashaka na shirikisho kuhusiana na sakata hilo,” alisema.
Alisema japo wizi wa tiketi na fedha za shirikisho hilo yamekuwa yakifanyika tangu enzi za FAT,lakini ni wajibu wa Tenga kama rais kujiweka salama mbele ya umma unaofuatilia sakata hilo jipya.
“Unajua kunaswa kwa tiketi hizo ni kama arobaini tu ya machafu yanayofanywa ndani ya taasisi za michezo na kwa vile tayari Watanzania wameshapoteza imani na TFF,” alisema.
“Yeye ndiye bosi, sasa unadhani kuchafuka kwa TFF kutamuacha salama hata kama hahusiki,” alisema Seydou.
Watu kadhaa wamekuwa akihojiwa na jeshi la Polisi akiwemo Mhazini wa Yanga, Godfrey Mwanje aliyenaswa juzi na kuthibitishwa na Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu.
Comments
Loading…