SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), linasaka wafadhili wa ziara ya wachezaji wa mpira wa kikapu kutoka vyuo vikuu vya Marekani wanaotarajia kuja nchini kwa ziara ya kimichezo mapema mwezi Juni.
Akizungumza juzi, Rais wa TBF, Richard Kasesela, alisema timu ya Young life kutoka Marekani inatarajia kuja nchini kwa mashindano ya kimataifa na timu za Tanzania.
Alisema timu hiyo inaundwa na wachezaji kutoka vyuo mbalimbali vinavyo shiriki ligi maarufu ya vyuo vya NCAA na kuunda timu ya Young Life America.
Ujio huo wa watu 35, una lengo la kuendeleza kiwango cha mpira wa kikapu nchini, kuendesha mafunzo ya mchezo huo kwa wachezajina makocha.
Pia alisema watakuza uhusiano baina ya vijana wa kitanzania na Marekani na kuhamasisha ujenzi wa viwanja vya mpira wa kikapu katika Manispaa za Dar es Salaam na baadae kuhamasisha mikoani.
Alisema licha ya Dar es Salaam, pia timu hiyo inatarajia kufanya kliniki mkoani Pwani, kwenye kituo cha michezo cha Filbert Bayi na kutembelea Zanzibar kwa mchezo mmoja.
Comments
Loading…