Chama cha mpira wa wavu nchini, TAVA, kimekipongeza chama hicho mkoa wa Dar es Salaam, DAREVA, kwa kufanikisha michuano ya klabu bingwa ya mkoa, iliyomalizika Julai 31 mwaka huu.
Michuano hiyo iliyoshirikisha timu saba, wanawake na wanaume, ilifanyika katika uwanja wa wavu wa Shule ya Uhuru Mchanganyiko ambapo Magereza waliibuka mabingwa wa jumla.
Akizungumza na Nipashe, Makamu Mwenyekiti wa TAVA wa fedha na utawala, Muharammi Mchume alisema mkoa wa Dar es Salaam umeonyesha mfano unaopaswa kuigwa na mikoa yote kwa maendeleo ya mpira wa wavu nchini.
Alisema licha ya ukosefu wa fedha na wadhamini, vyama vya mikoa vinapaswa kutekeleza programu zao ikiwemo uendeshaji wa michuano ili kuufanya mchezo uendelee kuwa hai.
Kwa mujibu wa kalenda ya TAVA, michuano ya klabu bingwa Tanzania Bara inatarajiwa kufanyika Septemba 16-20 mwaka huu ambayo hushirikisha vilabu mabingwa wa mikoa.
“TAVA ingependa kuona mabingwa wa mikoa yote wanashiriki michuano hiyo, jambo ambalo hushindikana kwavile baadhi ya mikoa haiendeshi ligi kwa kisingizio cha ukosefu wa fedha,“ alisema.
Alisema ili kupata udhamini ni lazima kuwepo na juhudi za makusudi za kushawishi mazingira ya kudhaminiwa ikiwa ni pamoja na kuendesha michuano kwa ufanisi kama walivyofanya DAREVA.
Michuano hiyo ya klabu bingwa ya mkoa wa Dar es Salaam, mbali na kuwapata mabingwa wa mkoa kwa upande wa wanawake na wanaume, pia ilipata kikosi cha timu ya mkoa kitakachoshiriki michuano ya kombe la Taifa baadaye mwaka huu.
Timu zilizoshiriki ligi hiyo mbali na mabingwa Magereza (Wanawake na Wanaume) ni JKT (Wanawake na Wanaume), Future na Makongo (Wanawake na Wanaume).
- SOURCE: Nipashe