in

Tatizo ni Marcio Maximo au ni sisi wenyewe?

Ndugu zangu Watanzania,

salaam sana. Kwanza niwashukuru wote wale ambao mumeweza kufikiria na kuona umuhimu wa kuanzisha webusaiti kama hii ambayo ilihitajika miaka mingi katika nchi yetu.

Michezo katika nchi yetu ipo katika njia panda. Nimekuwa katika kufuatilia michezo kwa miaka mingi tangu nilipokuwa mwandishi wa habari za michezo wa Uhuru na Mzalendo katika miaka ya sabini.

Naamini kuna kila sababu ya sisi kuinuka na kung’ara katika michezo. Tanzania inao uwezo huo. Wananchi wake wanao uwezo huo. Dhamira ya kisiasa ndiyo inayohitajika kwa sababu bila ya hiyo dhamira hakuna lolote lile linaloweza kusonga mbele katika jamii.

Naambatanisha makala ambayo ilitumika katika gazeti la Rai la wiki iliyopita baada ya kufungwa na Msumbiji kihalali kabisa.

Tutakuwa na mkutano wa wadau wachache siku ya Jumamosi mjini Dar Es Salaam, katika mgahawa unaojulikana kama Professors’ Corner kwa ajili ya kubungua bongo kuhusu maudhui ya makala hiyo.

Nia ni kuanza mchakato wa kutaka kuandikwa upya kwa Sera ya Michezo. Kwa hakika hakuna linalowezekana kama hakuna sera inayoeleweka na iliyo endelevu ambayo bila shaka itazaa sheria bora na endelevu.

Huu ni mwaliko wa wazi kwa wadau ambao wangependa kuchangia katika siku ya kwanza ya kutafuta na kufyagia njia kuelekea katika Sera ya Michezo inayoendana na mazingira ya sasa ya Uchumi na Siasa katika Tanzania.

Wote mnakaribishwa na mnaweza kupiga simu kuongea na katibu Leone Temu kwa simu +255 22 2700341 wakati wowote ule. Ni vyema kujiandikisha ili tupate idadi na kuweza kupanga mahitaji muhimu ya kikao.

Nashauri pia makala hiyo isomwe kabla ya kushiriki katika kikao hicho kama mahala pa kuanzia kubungua bongo.

Wakatabahu,

Dkt Gideon Shoo

Tatizo ni Marcio Maximo au ni sisi wenyewe?

na dkt gideon shoo

SIDHANI kama taifa letu katika miaka ya hivi karibuni limewahi kuwa na mshikano mkubwa kama katika hili la kuiandaa timu ya soka ya taifa Taifa Stars kwa ajili ya kuvuka kigingi cha kwenda kushiriki michuano ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Watanzania walisahau tofauti zote walizokuwa nazo na kujadili mpira na katikati ya mjadala huo walikuwapo watu kadhaa ikiwa ni pamoja na kocha mkuu Marcio Maximo ambao baadhi ya watu wanalisikia jina lake likitamkwa visivyo kwenye vyombo vyetu vya habari na hivyo kumwita Masikio badala ya Marcio.

Marcio Maximo aliletwa nchini kwa juhudi na msukumo mkubwa wa Ikulu. Si kwa sababu hiyo ni shughuli ya asasi hiyo muhimu katika taifa letu, la hasha, bali ni kwa sababu ya historia yetu na makocha mbalimbali wa ndani na nje. Ama wametimuliwa kwa bakora au wamefungasha virago wenyewe kwa kuandamwa na wapenzi wa kandanda waliojigeuza wakufunzi wa makocha wasio rasmi.

Kwa kuletwa kwa msukumo na baraka za Ikulu kocha huyo amesaidiwa pengine kushinda kocha mwingine ye yote yule ambaye amewahi kuifundisha timu ya taifa, Taifa Stars. Pamoja na mashambulizi ya hapa na pale kutoka katika benchi la ufundi lisilo rasmi kwa kiasi kikubwa kocha huyo amekuwa huru kufanya maamuzi yake ya kiufundi.

Kuingia kwa Maximo kuliwafanya baadhi ya wapenzi wa soka wakaamini kwamba muarobaini umeletwa kama ambavyo bila shaka alimiani binti mdogo sana Mwajuma Pembe katika wimbo wake wa Taifa Stars uliochukuwa nafasi ya tatu kwa ubora kwamba kashfa ya kichwa cha mwenda wazimu imefikia ukingoni. Masikini mjukuu wangu Mwajuma pamoja na kuamini hivyo nina hakika anajiuliza inakuwaje tushindwe wakati kila mmoja wetu aliamini kwamba ushindi tayari.

Mwajuma aliamini kama walivyoamini Watanzania wengi waliomzidi umri kwamba dawa ya huo ugonjwa ni Marcio Maximo akisaidiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete. Siku ilifika ya kumjaribu mgonjwa kama kweli amepona. Kilichotokea naamini hata Mwajuma anakumbuka kwamba mgonjwa bado hali yake si nzuri ingawa pengine anayo nafuu kidogo lakini nafuu si kupona na alichokitaka Mwajuma na sisi sote ni mgonjwa apone basi. Hakuna cha mgonjwa ana nafuu hapa. Si wakati wake.

Wimbo wa Mwajuma ni mtamu sana kama ari aliyokuwa nayo Rais Kikwete na nguvu alizozikusanya Maximo katika kutaka kuwaletea raha Watanzania. Bila shaka wote watatu pamoja na wengine walikuwa na nia njema na ni haki yao kujitutumua kwani ni mtu asiyejiamini tu ndiye athubutuye kuingia katika dimba angali amekwisha kujiamulia moyoni kwamba ameshindwa. Wote walioiunga mkono Taifa Stars na kuitakia mema nchi yetu wanastahili pongezi sana. Nami nawapongeza sana kwa ujasiri huo, tusishushe bendera zetu tuzibakize hapo hapo na tuzitumie kwa ajili ya shughuli nitakayoijadili hapa chini ili siku moja tuimbe kidedea.

Ni vyema tukaendelea kuzipepeza hizo bendera na kujiuliza maswali kadhaa kama njia ya kujiandaa kwa ajili ya kupata dawa ya kweli ya uwendawazimu wetu ambao Mwajuma ameuimba akiamini kwamba tayari tumekwisha kupona kabisa.

Hivi kandanda yetu ina msingi wowote ule wa kisayansi ambao unaisukuma au ni kandanda ya kubahatisha tu? Huyu Kocha aliyeletwa na wenzake walioletwa kwa ajili ya chipukizi wetu wana mazingira mazuri ya kuwawezesha kweli kugawa ujuzi wao na kuibua na kujenga vipaji vya wachezaji wetu au ni kubahatisha tu?

Ili kuweza kujibu maswali hayo ni vyema kujiuliza hivi baada ya kuwa yamefanyika mageuzi katika uchumi wetu kuna mageuzi yoyote yale ya msingi yaliyofanyika katika sekta ya michezo? Kama yapo yalifanyika lini na nani aliyeshiriki kuyajadili na kuyapitisha? Kama hakuna kwa nini na nani ayalete hayo mageuzi? Au nayo yanahitaji maelekezo ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa?

Katika zama za mfumo wa chama kimoja cha siasa suala la michezo lilikuwa ni sehemu muhimu katika sera za chama tawala na serikali yake.

Tanzania ilikuwa ni nchi ya ujamaa na kujitegemea. Elimu ilikuwa ikitolewa kwa uratibu wa serikali kwa kuzingatia sera iliyokuwapo iliyoundwa kwa mujibu wa siasa ya ujamaa na kujitegemea. Michezo ilikuwa ni sehemu ya sera ya elimu ingawa ilikuwa na sera yake mahsusi.

Michezo ilikuwa ikiendeshwa kwa sera ya michezo ambayo iliainisha wazi kwamba michezo katika Tanzania ni ya ridhaa. Hiyo ilikuwa na maana kwamba kwa kuwa michezo ni ridhaa basi na sheria zilizokuwa zimetungwa kwa ajili ya kusimamia na kuratibu shughuli za michezo zilihakikisha kwamba sera inatekelezwa.

Kwa mantiki hiyo basi michezo yote hapa nchini kwa mujibu wa sera ya michezo ya wakati huo ambayo iliendana na siasa ya ujamaa na kujitegemea ilikuwa ni sehemu ya mfumo huo na ushiriki wake ulilenga katika kuwajenga washiriki kuwa na siha njema na wakati huo huo ushiriki katika mashindano ya aina yoyote ile ulilenga katika kuliletea taifa sifa.

Katika utekelezaji wa sera ya michezo, serikali ililazimika na iliwajibika kuhakikisha kwamba kuna mazingira mazuri kwa ajili ya michezo. Hiyo ikiwa na maana ya kuwa na miundombinu ya michezo pamoja na sera na sheria ambazo zinajibu matakwa ya siasa iliyokuwapo zama hizo.

Sera ya elimu ilikuwa na sehemu ya michezo ambayo ilianisha wazi kwamba michezo ni sehemu ya elimu na kwa maana hiyo basi ratiba ya michezo ilikuwa ni sehemu ya ratiba ya masomo katika shule zote kuanzia chini kabisa hadi vyuoni.

Ni wazi kabisa kwamba katika mazingira ya uchumi wa kijamaa michezo nayo ni lazima iwe ya kijamaa. Haiyumkiniki kuwa vinginevyo. Uchumi wa kijamaa ulitanguliza jamii mbele na kwa mantiki hiyo mwanamichezo alijituma kwa ajili ya kuiletea sifa jamii yake na yeye anakuwa nyuma ya jamii au ndani ya jamii.

Katika kutaka kufanikisha michezo serikali ilikuwa na nafasi maalumu na ya pekee. Lilikuwa ni jukumu la serikali kutafuta mbinu za kuibua vipaji. Lilikuwa ni jukumu la serikali kuhakikisha kwamba kuna vifaa vya michezo na kwamba wananchi wanatengenezewa mazingira ya kushiriki katika michezo.

Itakumbukwa kwamba kuliwahi kuwapo na programu mbalimbali za kuibua vipaji hapa nchini na moja iliyopata umaarufu sana ni ile ya Michezo Kwa Wote ambayo ilifadhiliwa na Sweden katika miaka ya sabini.

Programu hiyo ilisaidia katika kuwashirikisha wananchi katika michezo kuanzia katika ngazi ya familia na wakati huo huo kuhamasisha michezo katika mashule na vyuo.

Kwa mujibu wa sera ya michezo iliyokuwapo michezo katika shule za msingi ilikuwa si tu ni sehemu ya masomo bali iliundwa mahsusi kwa ajili ya kusaidia kuibua vipaji na hivyo basi kuviendeleza kwa ajili ya ushiriki wa mashindano katika ngazi ya kuanzia chini hadi juu kabisa yaani taifa.

Shule za msingi zilikuwa na mashindano ndani ya shule yenyewe yaani darasa na darasa, hiyo ilisaidia katika kuunda timu ya shule na kuiandaa shule moja ya msingi katika wilaya kupambana na shule nyingine ya msingi ndani ya wilaya kama sehemu ya ratiba ya michezo katika muhula.

Wanafunzi walikuwa wakishiriki katika michezo yote. Mashindano ya kandanda, riadha, wavu n.k. yalikuwa ni jambo la kawaida na lililowekwa katika ratiba na Ofisa wa Elimu wa Wilaya na Mkoa walikuwa wakihakikisha kwamba hilo linafanyika.

Katika kuhakikisha kwamba michezo inapewa nafasi yake kama sehemu ya elimu kwa mwanafunzi sera ya elimu ilizungumza michezo na sera ya michezo ilizungumza elimu. Ushahidi huo ni katika michezo iliyokuwa maarufu kama Umoja wa Michezo wa Shule za Msingi Tanzania (UMISHUMTA).

Washiriki wa michezo ya UMISHUMTA walikuwa si wateule wa kupendelewa bali ni watoto ambao walionyesha vipaji katika michezo kuanzia katika mashindano ya madarasa katika shule zao na waliojipembua kwa umahiri.

UMISHUMTA yalikuwa ni mashindano yaliyokuwapo katika ratiba ya masomo iliyotambulika katika Wizara ya Elimu na hivyo haikuwezekana kuipuuza. Hilo lilikuwa tamasha la michezo la kitaifa na liliingizwa katika kalenda ya michezo na elimu nchini. Hakuna ambaye alikuwa na jeuri ya kulipinga hilo. Sekta nyingine za uchumi zilitambua hilo na zilishiriki katika kufanikisha mashindano hayo kila mwaka.

Aidha katika shule za sekondari michezo ilikuwa ni sehemu ya elimu na ndiyo sababu kulikuwapo na Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISETA).

Tamasha la michezo la vyuo vya elimu ya kati na ya juu katika Tanzania ulikuwa ni mwendelezo wa utamaduni uliojengeka kwa miaka mingi na bila shaka ulisaidia katika kuibua vipaji. Utamaduni huo ulijengwa kutokana na jitihada za kutekeleza sera ya elimu na sera ya michezo.

Vipaji vilivyoibuliwa katika ngazi hizo hapo juu ndivyo vilivyokuwa vikionekana katika mashindano yaliyoshirika mashirika ya umma.

Kutokana na umuhimu wa michezo ratiba ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma Tanzania (SHIMMUTA) ilikuwa katika ratiba ya uzalishaji na utendaji wa kila shirika la umma.

Ikumbukwe kwamba yote hayo hapo juu yalikuwa yakifanyika kwa mujibu wa sheria za nchi za wakati huo zilizotawala michezo ambazo ndizo zipo hadi leo. Sheria hizo zilitungwa kufuatana na sera ya michezo ya wakati huo ambayo kwa asilimia mia moja ni ya ridhaa. Sera iliyotokana na siasa ya ujamaa na kujitegemea ambayo hakuna asiyejua ilikoishia.

Baada ya mageuzi ya kiuchumi kushika kasi na kuanza kwa mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali kilichojitokeza ni kutelekezwa kwa sera nyingi zilizokuwapo na kufanywa mabadiliko rasmi yaliyotangazwa na mengine kimya kimya.

Uchumi ulihamishwa kutoka katika mikono ya serikali na kuelekezwa katika sekta binafsi. Hilo bila shaka lisingeweza kuendelea tu na kuacha sekta ya elimu mikononi mwa serikali. Kwa mantiki hiyo basi sekta ya elimu iliguswa sana na ndiyo sababu ikazaa sera mpya ya elimu kuanzia ya msingi hadi ya juu.

Hivi tunavyozungumza hivi sasa sekta ya elimu si tu kwamba ina sera mpya inayolingana na kuendana na mfumo wa uchumi na siasa tulio nao, bali umetungiwa sheria za kuhakikisha kwamba sera hiyo inalindwa na kurekebisha mahusiano katika utekelezaji wake.

Ni kutokana na ukweli huo wa kuwapo kwa sera mpya na kutungwa kwa sheria mpya za elimu ndiyo sababu leo tunazo shule za binafsi na hata vyuo vya binafsi vya elimu ya ufundi. Hilo lisingeliwezekana bila ya sera endelevu na sheria mpya. Nani angelithubutu kuingiza mtaji wake katika sekta ambayo hailindwi na sheria?

Sera mpya katika uchumi haiwezi kusonga mbele bila ya kuwa na sheria za kuiwezesha kufanya hivyo. Ni sheria ndizo zinazoweza kufanikisha ushiriki wa sekta binafsi katika nyanja mbalimbali za uchumi wetu.

Hivi leo si tu kwamba tuna wachimba madini binafsi tofauti na ule ukiritimba wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) bali tuna makampuni ya ulinzi binafsi tofauti na kipindi kile cha ujamaa na kujitegemea walipokuwapo polisi tu. Hayo ndiyo matokeo ya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa katika nchi yetu.

Lakini ni vyema hapa kuweka wazi kwamba yote hayo hapo juu kamwe yasingewezekana kama kusingekuwapo na sera mpya za kisekta zinazorandana na sera pana zaidi ya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa katika nchi yetu.

Kwa mantiki hiyo hiyo, haiyumkiniki leo hii tukazungumzia mafanikio katika michezo kama hatutaki kukubali ukweli kwamba michezo inaendeshwa kwa sera ya ujamaa na kujitegemea ambayo imepitwa na wakati kwa sababu sera hiyo haiwezi kufanya kazi na kutoa matunda yanayotarajiwa katika mazingira ya soko huria.

Sera ya michezo ya nchi yetu hadi sasa ni ile ya kuitambua michezo kama ridhaa na utumiaji wa vipaji kama ni kwa ajili ya sifa kwa taifa na si kwa ajili ya kumnufaisha mwenye kipaji chake pamoja na kwamba taifa nalo litafaidika kwa kusifiwa.

Ili kipaji kiweze kuwa na maana kwa mwenye nacho katika mazingira ya soko huria ni lazima kimnufaishe au kimhakikishie kunufaika nacho aliye nacho. Kinyume chake haiwezekani kwani hakuna mazingira yale ya ujamaa na kujitegemea yaliyokuwa yametengenezwa katika zama zile na zilizokuwa zinamfanya mwenye kipaji kuona sifa kukitumia kwa ajili ya kuiletea jamii sifa na maslahi yake kuwa si muhimu sana.

Katika mazingira ya soko huria vipaji hugeuka kuwa ni bidhaa adimu. Hii ni bidhaa ambayo mwenye nacho anaweza asikione na anayekiona asitake kujitumbukiza katika kukiendeleza kwa sababu haoni sababu za kiuchumi za kumfanya yeye kutumbukiza fedha yake katika shughuli hiyo.

Katika mazingira hayo basi ni muhimu kuwa na sera mpya ya michezo ambayo itatilia maanani mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa katika jamii.

Sera mpya ya michezo ni muhimu ikaandaliwa kwa kuzingatia masuala mbalimbali lakini moja la muhimu ni kwamba uwezo wa serikali kugharamia michezo kwa asilimia mia moja kama ilivyokuwa katika zama zile za UMMISHUMTA, UMISETA, SHIMMUTA nk. hivi sasa haupo. Hilo haliwezi kurudi. Ni historia.

Lakini pamoja na kutokuwapo kwa uwezo huo swali la msingi ni kwamba je, mfumo huo ulikuwa na faida yoyote ile na kama jibu lake ni ndiyo basi na tujiulize ni jinsi gani tunaweza kuubadili mfumo huo ili uweze kuingia kwenye soko huria na kuzaa matunda kwa wale wanaotaka kuwekeza katika michezo?

Sera mpya ya michezo itasaidia kuweka msingi wa kutunga sheria mpya za michezo. Katika mazingira ya sasa hivi kinachoendelea ni ubabaishaji katika sekta ya michezo. Kwa hakika katika sekta kama ya kandanda kinachoendelea ni uvunjaji wa sheria za nchi na ukiukwaji wa haki za msingi za wanamichezo kama ilivyok katika suala la uhamisho wa wachezaji.

Huwezi kuwapata wachezaji wazuri wa mchezo wowote ule kwa utaratibu wa sasa wa kuviziana na kunyang’anyana hao wachache ambao wameibukia kusikojulikana. Michezo inayoendeshwa bila ya mfumo madhubuti kamwe haiwezi kutoa matunda yanayotarajiwa.

Udhaifu wa sekta ya michezo kwa kutokuwa na sera na sheria zinazokidhi haja ya mazingira ya kiuchumi tuliyokuwa nayo ndiyo sababu kubwa ya ubabaishaji ambao upo kote nchini. Unapogusa mchezo wowote kama vile riadha, ndondi za ridhaa na za kulipwa au soka utagundua kwamba udumavu wetu unatokana na kutokuwa na sera endelevu na sheria za kusimamia michezo kwa haki.

Soka imeachiwa ubabaishaji wa Simba na Yanga. Klabu ambazo hazijulikani kama ni za ridhaa ama za kulipwa. Endapo tungekuwa na sera ya michezo inayotilia maanani zama tulizopo suala la usajili wa wanamichezo lisingekuwa na utata kwani sheria za michezo zingalikuwa wazi na zinazojitosheleza. Bila shaka yoyote katika usajili kila mchezaji angelipata fungu lake kihalali, serikali ingelipata kodi yake, mwekezaji angelipata fungu lake kutokana na kiasi alichokiingiza katika kuibua na kukuza kipaji n.k. ili mradi kila kitu kingelikwenda kwa mujibu wa sheria na kuondoa malumbano yanayotokana na ubabaishaji wa sasa.

Aidha, wawekezaji wa kweli kweli wangelijitokeza kwa sababu sheria zingeliwalinda na hivyo wasingeliona tatizo kuwekeza katika biashara ambayo wanajua italipa endapo watalengesha vizuri. Kwa nini mwenye mtaji asiwekeze katika asasi ya kuibua vipaji vya michezo kama anajua kwamba sheria inamlinda na hakuna awezaye kwenda kumnyang’anya tu mchezaji kwa ulaghai kama ambavyo inafanyika hivi sasa katika mazingira yasiyokuwa na sheria zinazoendana na wakati?

Nani atakubali kuwekeza fedha zake katika kuibua vipaji katika shule za msingi hivi sasa wakati hakuna sheria yoyote ile inayomlinda mwekezaji katika sekta ya michezo?

Kwa nini mtu akubali kujenga uwanja wa kandanda au kikapu au wavu kama hakuna sheria ya michezo inayomlinda na kumhakikishia kupata wateja kwa sababu michezo ni biashara na burudani?

Kwa nini mchezaji ajitose kichwa kichwa kama hakuna sheria inayomlinda yeye kama mwanamichezo wa ridhaa au wa kulipwa na ambayo itamhakikishia kwamba hata akipata madhara itahesabika kwamba ni ajali kazini na kwa mantiki hiyo basi anazo haki zake zote ambazo zimeanishwa katika sheria?

Vipaji vipo vingi katika Tanzania yetu na watu wake zaidi ya milioni 35. Katika vipaji hivyo vipo vya michezo. Lakini kama hakuna sera endelevu zinazolindwa na sheria madhubuti tutaendelea kutegemea miujiza kutoka kwa Marcio Maximo na Rais Kikwete na kamwe hatutaweza kung’ara si katika ulimwengu wa soka tu bali katika ulimwengu wa michezo kwa ujumla.

Kama kweli tunataka kwenda na wakati kama ambavyo tunajigamba kwa kuwa na uwanja mmoja wa kisasa, basi hatuna budi kufanya mambo kisayansi kwa njia endelevu. Tuingie katika mageuzi ya michezo nchini kwa kuandaa sera mpya ya michezo ambayo itajadiliwa kwa mapana na marefu na kwa kujifunza kutoka kwa wenzetu. Hiyo itabidi ifuatiwe na hatua nyingine ya juu zaidi ambayo itakuwa ni ya kutunga sheria za michezo ambazo zitatilia maanani hali halisi ndani ya nchi na nje ya nchi yetu.

Kama imewezekana kuwa na sera zinazooana na mfumo mpya wa uchumi katika takriban kila sekta na kila uchao tunajikuta katika mijadala ya sera hii au ile ya sekta nyingine ikiwa ni pamoja na ardhi, maji, barabara n.k. ni nini kinachotukwaza kufanya hivyo katika sekta ya michezo?

Kama kweli ule umati uliomiminika Uwanja wa Taifa majuzi na mamilioni waliokuwa wakisikiliza na kutazama majumbani wanayo haki ya kufurahi, basi ni vyema wakatambua kwamba hiyo furaha haitawezekana hadi tumefanya mageuzi ya kina katika sekta ya michezo.

Mageuzi hayo ndiyo yana uwezo wa kuhuisha michezo kuanzia ngazi ya kitongoji hadi taifa, na hali kadhalika kuhuisha michezo kutoka ngazi ya vidudu hadi vyuo vikuu.

Kwa kuwa na mageuzi yatakayolenga katika kutunga sera mpya tutajihakikishia kwamba michezo itafufuka upya kote nchini na bila shaka tutawapata akina Filbert Bayi wa ridhaa na akina Filbert Bayi wa kulipwa.

Hakuna njia ya mkato katika kufanikiwa kimichezo kama ambavyo hakuna njia ya mkato katika kufanikisha shughuli nyingine yoyote ile ya ngazi ya familia au ngazi ya taifa ni lazima kuwa na sera na kuilinda kwa sheria. Marcio Maximo hana kosa. Tatizo ni letu wenyewe. Tukimwandalia mazingira endelevu nina hakika atatupatia tunachokitaka. Hakuna muujiza wa ushindi isipokuwa mageuzi ya kweli katika sekta ya michezo. Mwenye masikio na asikie. Naomba kutoa hoja.

[email protected]

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply
  1. Salaam,

    kwa kweli marcio maximo ameweza kulibadilisha soka la Tanzania kwa kiasi fulani lakini tatizo kubwa ninaloliona kwa kocha huyu ni ubaguzi na chuki binafsi zidi ya wacheza, ni imani yangu kuwa knowlegde ambayo ameleta angekuwa kuwa flexible na kushirikiana vizuri na wadau wa soka kwa ujumla bila shaka hata south Africa mwaka tungekwenda.

    Ushauri wangu binafsi tu, this time, kocha wa Taifa ye yote tutakayempata awe wa kutoka ndani au nje ya nchi, tunaomba awe na wasaidizi wa ndani wasiopungua wanne, kwa mfano Mwl Mziray, Adorf Richard na wengine wazuri, system hii wamefanya ndugu zetu majirani hapo Rwanda imewasaidia kiasi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Jee michezo ni soka pekee?

Tujenge taifa la wanariadha, si wakimbaji