Pesa zilianza kumzoea mapema sana. Hakuweza kukaa bila ya pesa yoyote mfukoni mwake tangu akiwa mtoto.
Kwake yeye pesa kilikuwa kitu muhimu sana kuliko mwanamke. Vijana wengi wanapofikia umri wa kubalehe huwa machizi wa kutamani kuwa na wanawake wengi, lakini kwake ilikuwa tofauti kabisa.
Alikuwa binadamu mwenye asili nyingine na inawezekana alitoka katika udongo tofauti na udongo ambao wanadamu wengi walitumia kuumbwa nao.
Hata Mungu wake aliyemuumba alikuwa Mungu wa pesa hali ambayo ilimfanya kila kiungo chake cha mwili kinukie pesa.
Utaanzaje kumlaumu kuwa yeye anafikiria pesa muda wote wakati kaanza kuwa milionea akiwa na umri wa chini ya miaka 20!?
Umri ambao wewe unakimbizana na masomo ya kidato cha tano na sita mwenzako alikuwa tayari ana uchumi wake wa kujitegemea tena milionea.
Uchumi ambao ulianza kutengenezwa tangu akiwa na miaka 19 ambapo familia yake ilihama kutoka Salerno, kusini mwa nchi ya Italy na kwenda Napoli ambapo walifungua mgahawa ulioitwa “The Dutch City of Haarlem”.
Hapa ndipo akili ya kijasiriamali ilipoanzia, alijua jinsi ya kuwajali wateja. Alijua ni kipi mteja alikuwa anakitaka na alimtimizia kwa wakati sahihi.
Aliweza kuwapa sababu nyingi wateja wengi kwanini midomo yao inastahili kutafuna chakula kinachotoka katika Mgahawa wa “The Dutch City of Haarlem”.
Muda wote alikuwa jikoni na baba yake kutengeneza kitu ambacho wateja walitaka kukipata.
Alijua namna ya kuwatunza wateja na jinsi ya kupata wateja wapya, kwa kifupi alijua jinsi ya kuuza na kununua hisia za watu tangu akiwa na umri wa miaka 19 na alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kujifunza namna ya kujenga mahusiano na mawasiliano bora kati yake na mteja.
Kitu ambacho kilimfanya asiutumikie mpira kwa kutumia miguu yake, yeye aliamua kukiajili kichwa chake akitumikishe kwenye mpira.
Kitu ambacho kilianza kuonekana awali alijaribu kuwa mchezaji wa FC Haarlem. Alishindwa kuitumikisha miguu yake uwanjani, hata viongozi wa timu waliona hicho kitu wakaamua kumfanya awe Sporting director wa timu yao.
Kazi ambayo ilimfanya awe na mahusiano makubwa ya kibiashara na watu wengi, ilifikia wakati mpaka akawa anasaidia makampuni ya Uholanzi kupata mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao katika nchi ya Italy.
Utajiri ulimfuata akiwa na umri mdogo hii ni baada ya yeye kujiaminisha kuwa chakula chake kitakuwa pesa, maji yake ya kunywa na kuogea, nguo na kila kitu kwake kilikuwa pesa.
Pesa zilimfuata baada ya kuziandalia mazingira bora ya kuishi, ndiyo maana hata alipofanikisha usajili wake wa kwanza Bryan Roy kutoka Ajax kwenda Foggia mwaka 1992 watu wengi walimshangaa.
Na ndiyo usajili uliomfanya aitwe “one-man show”, alifanikiwa kusimama yeye kama yeye kukamilisha usajili huo uliompa mwanga mkubwa wa kuingiza pesa kupitia mpira.
Ndiyo usajili ambao ulimwingiza katika dunia ya kutoaminiwa na Sir Alex Ferguson, ndiye usajili ambao ulimweka sayari ya mbali na Pep Guardiola na Jurgen Klopp.
Hawamwamini hata chembe, kwao wao wanamuona kama mtu aayetazama pesa tu.
Ndiyo usajili ambao ulitufanya tujue Mino Raiola anakula hela kubwa baada ya kitabu cha Football leaks: The Dirty Business of Professionall Football.
Kitabu ambacho kilituonesha kuwa Mino Raiola alifanikiwa kula Pound Milion 41 kwenye zile Pound Milion 89 za uhamisho wa Paul Pogba kwenda Manchester United.
Muda umeshapita tangu apate hizo pesa, mate yake yanatamani pesa nyingine tamu kutoka kwa Paul Pogba.
Kwake yeye huu ndiyo muda sahihi anaouona yeye kujipatia pesa nyingi kupitia Paul Pogba kwa sababu ya umri mdogo wa Paul Pogba na ikizingatia ametoka kushinda kombe la dunia.
Anatumia nafasi hii, ni mtu makini sana kwenye matukio haya, atatengeneza kila aina ya mazingira ili afanikiwe kwenye kila anachokiwaza ili akaunti yake ya benki itoe tabasamu.
Tutasikia sana habari za Paul Pogba, hatutomuona wala kumsikia Paul Pogba akisema chochote kwenye vyombo vya habari na kuna wakati atajinasibu kuwa ana maisha mazuri ndani ya Manchester United lakini ukweli ni kwamba Mino Raiola ndiye aliyeshikilia usukani wa gari alilopanda Paul Pogba.