ENGLAND imempoteza mtu aliyekuwa golikipa wao hodari zaidi katika historia na aliyepata kuokoa mabao ya wazi kuliko wengine, Gordon Banks.
Mchezaji huyu aliyetwaa Kombe la Dunia na England 1966, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 81, akiacha nyuma kumbukumbu ya kazi nzuri, uhodari na uzalendo wa aina yake kwa taifa.
Ni huyu pia anayechukuliwa kuwa kipa bora zaidi kupata kuchezea klabu au timu yoyote katika historia ya soka. Alishiriki pia kwenye fainali za Kombe la Dunia 1970 dhidi yaBrazil, ambapo dhidi ya Brazil alifanya kile kinachoitwa ‘uokoaji mkubwa zaidi kuwahi kufanywa’ – ukiwa ni mpira mkali na wa karibu mno wa kichwa kutoka kwa Pele.
Aliokolea wapi bao hilo la wazi linalokumbukwa hadi leo na ambalo video yake ipo? Ilikuwa mjini Guadalajara, Mexico, ambapo England walikuwa wakicheza dhidi ya Brazil kwenye hatua za makundi. Jairzinho, mchezaji aliyekuwa na nguvu na kasi kubwa akicheza upande wa kulia, ndiye alitoa majalo kwa Pele baada ya kumzidi nguvu beki wa kushoto wa England, Terry Cooper.
Pele, mmoja wa wachezaji mashuhuri zaidi katika historia ya soka duniani, alikutana na mpira huo akiruka na kuupiga kichwa cha kudunda chini, na tayari alikuwa akishangilia kwa kusema ‘goooliii!’ pale Banks, kama muujiza vile, alipojitupa na kuhakikisha anaokoa kwa mkono wake wa kulia na kuutupa juu ya mtambaa wa panya, kana kwamba anapunga vila.
“Mara baada ya mkono wangu kufanikiwa kuufikia mpira, nilidhani ungeenda kwenye kona ya juu,” alikumbukia Banks baadaye na kuongeza; “lakini baada ya mie kuanguka pale chini palikokuwa pagumu nilitazama juu na kuona mpira ukipita juu ya wavu.”
Pele kwa upande wake, baada ya kubaini kwamba halikuwa bao, alimwangalia Banks na anabainisha kwamba alijisemea; “Banks, punguani wewe!” Kwamba alishangazwa sana kuona mpira haukuingia wavuni. Baadaye akasema: “Nimeshafunga mabao zaidi ya elfu maishani mwangu lakini kile watu wanazungumza zaidi juu yangu ni kile ambacho sikufanya, kama kutofunga bao hilo.”
Bwana huyu alizaliwa Sheffield, akiwa mmoja wa watoto wanne wa Thomas, mzee aliyekuwa akifanya kazi kwenye shirika la michezo ya kubahatisha. Kipa huyu alikuwa na urefu wa futi sita na inchi moja na alionesha umahiri wake tangu akiwa na timu ya mjini kwake – Sheffield Schoolboys, lakini ajabu ni kwamba hakuchukuliwa na klabu kubwa za mjini kwake – Sheffield United na Sheffield Wednesday.
Chesterfield waliokuwa wakijulikana kwa kuwa na makipa wazuri, walikuja kufaidi kwa kumsajili na akaanza kucheza msimu wa 1958/9. Alicheza mechi 22 nyingine za ligi katika msimu wa kwanza na klabu hiyo, kabla ya Leicester City kumchukua.
Hapo Leicester alicheza mechi 293 za ligi, akiwa na wajibu mkubwa kuwafikisha kwene fainali ya Kombe la FA 1961 na 1963, lakini wakapoteza mechi kwenye fainali zote hizo mbili dhidi ya Tottenham Hotspur na Manchester United mtawalia. Mwaka 1964 aliisaidia timu yake kutwa Kombe la Ligi walipocheza dhidi ya Stoke City.
Ilipofika Aprili 1967, hata hivyo, Leicester wakamng’amua kipa mahiri zaidi aliyezaliwa kwao, katika Peter Shilton, kisha wakamuuza Banks kwa Stoke kwa £52,500. Akiwa na umri wa miaka 34 alicheza kwenye ushindi wa Stoke dhidi ya Chelsea kwenye fainali za Kombe la Ligi – ambalo hadi sasa ni moja ya makombe makubwa timu hiyo kupata kutwaa. Alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa msimu wa mwaka England.
Banks alicheza mechi 510 kwa klabu hizo katika mashindano yote, kisha Stoke wakampa kazi ya ukocha kwa timu yao ya vijana. Alipata tatizo la jicho baada ya kupata ajali lakini 1977 Banks alijiunga na Fort Lauderdale wa Marekani akirudi kwenye ukipa na wakatwaa ubingwa huko. Alifuatwa na George Best mwaka uliofuata, akacheza tena mechi nyingine 11 kabla ya kutundika daluga 1978.
Alikuja kuwa kocha wa Telford United, lakini akaondokana na soka ya moja kwa moja, kabla ya kupata uongozi Stoke tangu 2000 hadi kifo chake. Ameacha mke, Ursulaaliyekutana naye akiwa jeshini 1955, na wana watoto watatu; Robert, Wendy na Julia. Kifo chake kilitokea Februari 12 mwaka huu.
=-=