MABINGWA wa soka wa Bara, Yanga leo wanavaana na Tusker ya Kenya katika nusu fainali ya pili ya Kombe la Kagame wakiwa wawakilishi pekee waliobakiwa na jukumu la kuikoa Tanzania katika aibu ya kulikosa tena Kombe la Kagame baada ya Simba kuondolewa jana.
Mabingwa wa Zanzibar, Miembeni waliondolewa kwa kufungwa mabao 2-0 na URA katika mechi ya robo fainali, wakati kipigo cha bao 1-0, ambacho Simba ilikipata mbele ya URA jana, kilitosha kuzima ndoto za klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ya kila mwaka kwa mara ya saba.
Yanga, ambayo imeonekana kuimarika kadri inapocheza mechi, inaingia uwanjani leo ikijua kuwa ndiyo pekee inayolibeba taifa wakati itakapovaana na Tusker iliyotinga nusu fainali kwa kuishinda Rayon Sport ya Rwanda kwa mikwaju ya penati.
“Tuna imani kuwa tutafanya vizuri katika mechi yetu ya nusu fainali,” alisema kocha Mserbia wa Yanga, Dusan Kondic baada ya timu yake kuonyesha kandanda safi na kuishinda Vital’O ya Burundi kwa mabao 2-0 Jumatano.
“Timu hii ni changa na inakuwa bora kadri inavyocheza mechi. Kwa hiyo ni vizuri mashabiki wakaiunga mkono, wakaipa nguvu na kuacha tabia ya kuzomea wakati wachezaji wanapokesea.
“Lakini timu ni nzuri na nina imani tutashinda mechi inayokuja.” Kocha huyo atakuwa akikumbuka jinsi mashabiki walivyokosa raha kutokana na washambuliaji wake kupoteza nafasi nyingi za wazi katika mechi zilizopita.
Kosakosa hizo ziliendelea katika mechi dhidi ya Vital’O kwa washambuliaji ama walishindwa kupiga pasi nzuri za mwisho baada ya kuwapita mabeki, ama kutolenga vizuri golini na wakati mwingine kutokuwa makini.
Mrisho Ngassa, Boniface Ambani, Ali Shamte na Kigi Makasi walipoteza nafasi kadhaa za wazi ambazo zingeweza kuifanya Yanga ishinde kwa idadi kubwa ya magoli kama zingetumika.
“Hakuna makosa ambayo hayawezi kurekebishika,” alisema Mserbia huyo.
“Ni kweli kwamba wachezaji wamepoteza nafasi nyingi, lakini timu huanza kufundishwa kulinda lango, baadaye kiungo na baadaye kutengeneza nafasi. Hilo la kufunga hatujalifanyia kazi, lakini linafuata.”
Kondic hategemewi kufanya marekebisho makubwa kwenye kikosi chake. Ambani na Ngassa wanatarajiwa kuongoza mashambulizi wakisaidiwa na Shamte na Kigi, ambaye alionyesha kiwango cha juu katika mechi ya Vital’O, huku Abdi Kassim akicheza nyuma ya washambuliaji na Godfrey Bonny akicheza mbele ya mabeki George Owino, Wisdom Ndlovu, Shadrack Nsajigwa, ambaye alipumzishwa juzi, na Nurdin Bakari.
Tusker ina uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na hiyo inaweza kuwa silaha yao kubwa kwa Yanga, ambayo kasi ya washambuliaji wake imekuwa ikizihangaisha timu nyingi walizokutana nazo.
“Yanga ni timu nzuri na kwa kweli si timu ya kuidharau,” alisema kocha Jackob ‘Ghost’ Mulee. “Tumeiangalia na tumeiona inacheza vizuri, lakini hilo halitutishi.
“Hata hivyo, hata kama tutashindwa, hayo ndio matokeo. Tumejiandaa kwa lolote kwa kuwa hii ni timu changa na tofauti na timu nyingine, haijashiriki mashindano yoyote ya kimataifa mwaka huu kwa kuwa Kenya ilifungiwa na CAF.”
Katika tukio mechi ya jana pamoja na Simba kupata penati katika dakika ya 120,haikuweza kujiokoa mikononi mwa Mamlaka ya Kodi ya Uganda (URA) ilipopigwa bao la uchungu 1-0 katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Kagame.
Mshambuliaji Mnigeria, Emeh Izechukwu, ambaye katika mechi nne zilizopita alikuwa mtoaji pasi za mwisho zilizozaa mabao matatu wakati Simba ikichanja mbuga kuelekea nusu fainali, ndiye aliyepewa jukumu hilo la kuwaokoa vijana wa Msimbazi.
Lakini Mnigeria huyo, ambaye ameazimwa Simba na Enyimba FC ya Nigeria, alipiga mpira pembeni ya goli na kuikosesha Simba nafasi ya kusawazisha ili mchezo uamuliwe kwa penati tano.
Comments
Loading…