RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amewataka Watanzania kuwa na moyo wa kuzisaidia timu za Taifa pindi zinapohitaji msaada na si kuiachia Serikali yenyewe kuendeesha kila kitu.
Pia amesema amefurahishwa na kiwango cha timu ya Taifa ya soka ‘Taifa Stars’ kiasi kwamba sasa si kichwa cha mwendawazimu kama zamani.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana, alipokuwa akipokea msaada wa fedha kwa niaba ya Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), kwa ajili ya maandalizi ya timu ya Taifa ya ngumi kwenda katika michuano Namibia na Aljeria Aprili mwaka huu, ambayo ni ya kutafuta viwango vya kufuzu michezo ya Olimpiki itakayofanyika China Agosti mwaka huu.
Alisema Serikali ina mambo mengi ya kushughulikia na si kila kitu mpaka Serikali ifanye, inawezekana kampuni na mashirika yakafanya harambee ya kuchangisha fedha na timu zikafanikiwa kushiriki mashindano mbalimbali.
Aliipongeza BFT kwa kuweka wazi matatizo waliyonayo, ambapo kwa kufanya hivyo watafanikisha malengo waliyojiwekea.
Wakati huo huo, Mwinyi ameishukuru Benki M, CXC Tours & Safaris Limited pamoja na Dengard Limited kwa kutoa michango yao kusaidia BFT katika maandalizi ya kwenda Aljeria na Namibia.
Benki M ilitoa sh. 6,550,000, Dengard System ilitoa sh. 500,000 na Kampuni ya CXC Tours & Safaris ilitoa sh.625,000, ambapo sh. 375,000 walitoa kabla kwa ajili ya kulipia ukumbi utakaofanyikia mchujo wa mwisho wa kupata mabondia 10 watakaoenda Aljeria na Namibia. Mchujo utafanyika kesho.
Rais wa BFT, Shaban Mintanga aliishukuru kamati maalum iliyoundwa kwa ajili ya kufanya harambee ya kutafuta fedha kwa ajili ya maandalizi ya safari hiyo, na kwamba ana imani timu itakayochaguliwa itawakilisha vizuri.
Katika hatua nyingine, Mwinyi alisema ameridhishwa na kiwango cha Taifa Stars kwa kuepuka kuwa kichwa cha mwendawazimu kila yanapotokea mashindano.
”Sasa hivi timu yetu imebadilika sana tumeepuka kuwa kichwa cha mwendawazimu kwa kila timu kuja kutufunga, lakini kwa kiwango cha sasa hivi kinaridhisha,” alisema Mwinyi.
Alisema Taifa Stars imepiga hatua kubwa ukilinganisha na zamani, ambapo sasa hivi pia imesogea zaidi katika ubora wa viwango vya FIFA (Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa), hali inayoashiria wapenzi wakiwa na subira mambo mazuri yatakuja zaidi.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Michezo, Juliana Yasoda alivitaka vyama vya michezo kutoogopa kuomba misaada pindi wanapokwama ili kuinua maendeleo ya michezo nchini.
Comments
Loading…