Katika soka wiki moja ni kipindi kirefu sana, maana kinaweza kushuhudia mabadiliko makubwa, iwe kwenye timu au uongozi wa klabu.
Desemba 26 mwaka jana, mabingwa wa zamani wa Ulaya, Nottingham Forest walikuwa na mchezo dhidi ya Leeds United katika ligi daraja la pili (Champonship) ya England.
Baada ya kuwa nyuma kwa bao moja, Forest waliibuka na ushindi wa mabao 4-2, uliokwenda kwa tambo nyingi, washabiki wakiamini mambo yameanza tena kuwanyookea vigogo hao wa zamani.
Kwa kiasi fulani, washabiki wake walifurahia mwenendo wa timu yao, lakini saa chache tu baada ya kipenga cha mwisho, wamiliki wa klabu hiyo kutoka Kuwait, familia ya Al Hasawi, walimtimua kazi kocha, Sean O’Driscoll.
Katika kumfukuza, Mwenyekiti wa Klabu, Fawaz Al Hasawi, alikiri O’Driscoll aliingia klabuni katika mazingira magumu na ana bahati mbaya kupoteza kibarua chake timu ikiwa pointi moja tu kufikia sita bora, lakini uamuzi ulifanywa kwa ajili ya malengo ya muda mrefu ya klabu.
Muda si mrefu baadaye, Alex McLeish aliyemrithi O’Driscoll naye ameondolewa kiaina klabuni hapo.
Mwezi Januari pia umeshuhudia Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Forest, Frank Clark aliyehusika na utafutaji na usajili wachezaji naye akifukuzwa. Huyu alipata kuwa mchezaji na kocha wa Forest.
McLeish aliondoka ‘kwa ridhaa’ ya pande zote baada ya kushinda mechi moja tu kati ya saba. Giza liligubika usajili wa dirisha dogo, baada ya mchezaji aliyelengwa kwa ubani na uvumba, George Boyd kushindwa kujiunga baada ya kukutwa na matatizo ya macho alipofanyiwa vipimo klabuni hapo.
Washabiki wa Forest waliingia kwenye mitandao ya jamii, wakilalamikia klabu kubwa inayoangamia kwa kukosa mpangilio.
Siku chache zilizopita, mchezaji na kocha wa zamani wa Forest, Billy Davies, aliteuliwa tena kwenye kiti hicho moto alichokizoea zamani.
Hata hivyo, kabla hajakaa sawa, timu yake ikacharazwa mabao 2-0 na Bristol City, ambao sasa wanafundishwa na Sean O’Driscoll aliyefukuzwa Forest.
Simulizi hiyo ni muhimu katika kuangalia klabu nyingine za England zinakoelekea na soka kwa ujumla.
Blackburn Rovers ni moja ya klabu kongwe zaidi nchini England, lakini ilipoteza umakini, ikaanza kushuka kutoka eneo la katikati ya msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL) ilikosoea hadi kushuka daraja.
Wamiliki wa klabu hio, Venky’s Group wa India walianza umiliki wao kwa kumfuta kazi kocha anayeheshimika ndani na nje ya nchi, Sam Allardyce Desemba 2010.
Tangu wakati huo, Wahindi hao wamejitumbukiza kwenye mkakati wa kujisafisha mbele ya vyombo vya habari, kuonyesha kana kwamba wanakwenda sawa.
Hivi karibuni, mchambuzi wa masuala ya michezo kwenye televisheni, Shebby Singh, alipewa kazi ya kuwa mshauri wa masuala ya kimataifa wa Venkys, lakini inasemekana haelewani na Mkurugenzi Mtendaji, Derek Shaw, kwa madai ya kuingilia masuala ya soka na migogoro ya mikataba ya wachezaji.
Umejengeka utamaduni Rovers wa watu wa zamani kuzozana na wale wapya, huku klabu ikiwa na kocha wake wa tatu katika msimu mmoja tu, na ndoto za kurudi EPL zikiwa za alinacha.
Venky’s Group na familia ya Al-Hasawi ni baadhi tu ya wimbi la wamiliki wa kigeni kutwaa udhibiti wa klabu za ligi nchini England.
Cardiff City inao wamiliki wapya kutoka Malyasia, walioamua kubadili kabisa rangi za klabu – kutoka bluu kwenda nyekundu na kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa wadau.
Pengine wanaweza kusamehewa, maana wanaelekea kupanda daraja na kuingia EPL.
Familia ya Glazer ya Marekani iliyoitwaa Manchester United, ilikumbana na uasi uliosababisha kuundwa kwa klabu mpya kabisa – FC United of Manchester.
Klabu hiyo mpya ilianzishwa na washabiki wa damu na waliokuwa wafurukutwa wa Manchester United, wanaosema wamechukizwa na kiwango cha kuticha cha deni la Man U kufikia pauni karibu milioni 360 linalowekewa klabu tu badala ya wamiliki wapya wenye uwezo kulilipa.
Kuna Roman Abramovich pale Chelsea, ambaye tabia yake inayotambulika zaidi ni kuajiri na kufukuza makocha anavyopenda, bila kujali washabiki wanamtaka nani na mazingira yakoje.
Sheikh Mansour wa Manchester City naye ana mambo yake, kwa sababu uwekezaji wake Etihad umewatoa macho Uefa, wakijiuliza iwapo unaendana na kanuni za haki katika masuala ya kifedha.
Washabiki huathiriwa na aina hii ya wawekezaji, upande mmoja wakifurahia kwamba fedha zinamwagwa ili kununua wachezaji na kufanya uwekezaji zaidi hadi kutwaa ubingwa.
Lakini upande wa pili kuna kujiuliza iwapo lazima kuondokana na mambo yaliyokuwapo, kwenda kinyume na matakwa ya washabiki na kuwafukuza makocha wanaopendwa au kuleta wanaojulikana kwa uhasama na washabiki – kama Rafa Benitez Chelsea.
Hata hivyo, kuna wawekezaji wanaogeuka na kuangalia jinsi ya kurudisha mtaji wao, hivyo wanaongeza bei za tiketi za kuingia mpirani ili kukabiliana na mishahara mikubwa ya wachezaji au pia wanafika mahali wanawauza wachezaji bila kujali.
Comments
Loading…