Taifa Stars walala 3 – 0
Timu ya Taifa ya Tanzania – Taifa Stars imeendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu baada ya kunyolewa 3-0 na Uganda.
Stars waliingia uwanjani wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri baada ya Kocha Mart Nooij (ambaye sasa amefutwa kazi) kuita wachezaji kadhaa wapya.
Mechi hii ilikuwa ya kwanza kwa ajili ya kufuzu kwa Kombe la mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2016.
Hii ni hali mbaya zaidi ya soka nchini katika muongo mmoja uliopita, ambapo pia Stars wametoka kufungwa idadi hiyo hiyo ya mabao na Misri katika mechi ya kwanza ya kutafuta kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017.
Nooij ambaye ni raia wa Uholanzi alilazimika kusindikizwa kutoka uwanjani na askari kwa ajili ya kumuepusha na kichapo kutoka kwa washabiki.
Wachezaji wa Stars walitupiwa mawe walipowasili kutoka Misri wiki iliyopita wakati wale ambao hawakwenda Misri pia walitupiwa mawe na basi lao kuvunjwa kioo wiki hiyo hiyo.
Aibu ya Tanzania ilikuwa kubwa zaidi kwa kufungwa na mechi zote tatu ilipokuwa imealikwa Afrika Kusini kucheza michuano ya COSAFA.
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliamua kusitisha ajira ya Nooij Jumamosi hii katika kikao chake.
Kadhalika ilivunjilia mbali benchi lote la ufundi na itatangaza benchi jipya la ufundi baadaye. Kulikuwa na habari kwamba inapanga kumchukua Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, lakini mabingwa hao wa Tanzania hawajapendezwa na mpango huo.
Yanga wanajisuka upya na kujifua kwa ajili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Klabu Bingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania.
Pamoja na mambo mengine, TFF imeidhinisha kwamba klabu inaweza kusajili wachezaji saba wa kigeni na hata kuwachezesha wote katika mechi moja.
Klabu, hasa Yanga na Azam ziliomba kupewa fursa hiyo ili kujiandaa vyema kwa mashindano ya kimataifa yanayowakabili, zikitolewa sababu kwamba wachezaji wengi wa ndani hawajitumi.
Simba waliunga mkono maombi hayo pia, japokuwa kwa mwaka wa tatu mfululizo sasa watakuwa wa ‘hapa hapa’ kwa maana kwamba watacheza tu ligi ya ndani, labda na mechi za kirafiki nje wakipata bahati.