Kuna dharau kubwa inafanywa na mamlaka za Tanzania kuhusu sekta ya michezo. Wachezaji wengi wanaochaguliwa kuunda Taifa Stars hawakutokana na mafunzo ya soka. Ni vipaji binafsi..
POINTI 8 kibindoni, moja zaidi ya wapinzani wa jadi wa Taifa Stars, Uganda zimeipa nafasi Tanzania kufuzu mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika maarufu kama AFCON. Katika mchezo wa mwisho dhidi ya kigogo cha soka, Algeria, Taifa Stars ilihitaji saresuluhu au ushindi. Lakini dakika 90 za mchezo huo zilimalizika kwa kutoka suluhu. Haikuwa kazi rahisi kwa vijana wa Taifa Stars kuwadhibiti Waalgeria nyumbani kwao. Ikumbukwe ni Algeria ambao waliwahi kuizaba Tanzania mabao 7-0 katika moja ya michezo ya kufuzu AFCON. Lakini Septemba 7 ilikuwa siku ya aina yake.
UKUTA WA KIBABE
TANZANIASPORTS ilisuhuhudia mabadiliko makubwa yaliyofanywa na kocha Adel Amrouch kwa kuwapanga viungo wakabaji wawili, Mzamiru Yassin na Sospeter Bajana. Nyota hawa wawili walidhibiti eneo la kiungo huku nyuma yao wakilindwa na Dickson Job aliyekuwa mlinzi wa walinzi wa kati. Kwamba Dickson Job alikuwa na kibarua cha kuwalinda Ibrahim Bacca na Bakari Mwamnyeto, huku upande wa kulia Haji Mnoga akiwakabili mawinga hatari wa Algeria. Upande wa kushoto alikuwa nyota anayekwenda kupambana na Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwakilisha klabu ya Shakhtar Donesk, Novatus Dismas Miroshi.
Katika safu ya ulinzi Taifa Stars walikuwa wakali na waliondosha hatari zote langoni mwao. Licha ya kutocheza kwa burudani, lakini wachezaji wot walikuwa hawana cha kupoteza, walicheza kwa ari na kutafuta matokeo kuliko kuhofia ukubwa wa Algeria na mastaa wake. Wengi wa nyota waliochezea Algeria wamezaliwa barani Ulaya kwenye miundo mbinu ya kiwango cha juu kuliko nyota wengi wa Taifa Stars.
SHANGWE LA KIZAZI KIPYA
Katika karne mbili, Tanzania imefuzu kwenye mashindano ya AFCON. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1980 wakati kikosi cha Taifa Stars kilipokwenda nchini Nigeria kushiriki AFCON. Katika karne ya 21 yaani kuanzia mwaka 2000 hadi sasa (2023) wachezaji wa kizazi kipya wamefuzu mara mbili. Mwaka 2019 na mwaka 2023. Hii ina maana kizazi kipya kimefanikiwa kufuzu mara mbili katika kipindi cha miaka 23. Huenda ikawa ni takwimu hafifu lakini wanacho cha kujivunia. Taita Stars ilicheza kwa nidhamu na mabeki wake ilikuwa ya kiwango cha juu. Ni kizazi ambacho kimeingizwa nyota mpya aliyepewa uraia Kibu Dennis.
Huyu ana uwezo wa kucheza nafasi zote za mbele, winga wa kulia, kushoto na mshambuliaji. Kibu Dennis alikuwa mwiba kwa Algeria na alifanikiwa kuvuta umakini wa wenyeji. Kizazi kipya kimeonesha kuwa mchezo wa soka sasa upo wazi na hakuna kinachoshindikana. Kufuzu kwa mashindano AFCON ni ishara kuwa maisha ya wachezaji wa kizazi kipya yatasonga na watakuwa na la kujivunia mbele ya kaka zao waliofuzu mara ya kwanza mwaka 1980.
KURUNZI KWENYE SEKTA YA MICHEZO
Kuna dharau kubwa inafanywa na mamlaka za Tanzania kuhusu sekta ya michezo. Wachezaji wengi wanaochaguliwa kuunda Taifa Stars hawakutokana na mafunzo ya soka. Ni vipaji binafsi vinavyoibuliwa na mashindano ya Ligi za soka. Hakuna akademi za maana za kuwapa mafunzo wachezaji wetu kama njia za kuvumbua vipaji. Viwanja vya michezo nchini vinavyomilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) vina hali mbaya.
Maeneo mengi ya wazi ambayo yangetumika kuvumbua vipaji huuzwa. Hakuna mkakati maalumu wa kukuza na kulea vipaji vya soka, hivyo sekta nzima imekuwa katika hali mbaya. Jasho la wachezaji wa Taifa Stars linatokana na jitihada za wachezaji wenyewe, lakini uongozi wa Tanzania kwenye sekta ya michezo hautoi nafasi ya kutosha. Mathalani bajeti ya Wizara ya Michezo na Utamaduni inaishia kuhudumia hadi mashindano ya SHIMIWI ambayo hayavumbui vipaji vyovyote vya kulinufaisha Taifa.
Sekta ya michezo na burudani imekuwa ikiishi kwa mtindo wa “tupo tupo”, na hakuna ndoto za Kitaifa kuitangaza Tanzania kupitia mchezo wa soka. Timu zinapofanya vizuri ndipo viongozi wenye mamlaka huibuka kuunda kamati na mengineyo, lakini hayana mwendelezo wa maendeleo. Ni muhimu kujenga viwanja vingi vya soka kwa viwango vya kati na juu. Hivi leo hatuna viwanja vya kati ambayo vingeweza kutumika kwa mashindano hata madogo ndani ya nchi. UMISETA na UMITASHUMTA hutumia viwanja vibovu na visivyotoa matosha kwa vipaji vya Kitanzania. Hali kadhalika michezo ya mpira wa pete, riadha,ndondi,volleyball na mingineyo mingi haipewi kipaumbele na hatuna viwanja vya michezo. Vilevile hata kumbi za burudani kwa asili ya kuwapa nafasi vipaji vya Kitanzania ambavyo ni ajira imekuwa vigumu. Ni wakati wa kusema na kutenda kwa wakati mmoja. Hamasa ya kununua goli kwa kiasi fulani cha fedha bila kuijenga sekta ya michezo asilani hatuwezi kupiga hatua za maendeleo.
Comments
Loading…