*Serikali iwaulize TFF ni msaada gani wanahitaji
*Tuachane na tabia ya kuunda”kamati za ushindi”
*Wanasiasa acheni kuingilia mipango ya timu
MWEZI Mei mwaka 1996, Simba ya Tanzania iliifunga Arab Contractors ya Misri mabao 3-1 jijini Dar es Salaam katika mashindano ya kombe la Washindi Afrika lililounganishwa na kombe la CAF kutengeneza kombe la Shirikisho.
Kwenye mechi ya marudiano, ili iendelee na mashindano, Simba ilihitaji kutofungwa 2-0 au idadi yoyote ya mabao ambayo ukiyatoa ya Simba kufunga yasibaki matatu, yaani kwa mfano 3-0, 4-1, 5-2 na kuendelea. Simba walilala 2-0 na kutupwa nje ya mashindano kwa bao la ugenini la Wamisri walilolifunga hapa kwani matokeo ya jumla yalikuwa 3-3.
Wakiwa wamefungwa bao moja ugenini, Simba walikaza ili wasifungwe bao jingine. Ghafla waarabu walipata penalti. Kipa Mohammed Mwameja ambaye alikuwa mzuri sana wa kucheza penalti aliiokoa penalti hiyo na kuwa kona.
Angalia sasa, wachezaji karibu wote wa Simba wakawa wamemzonga Mwameja kushangilia naye na kumpa pongezi nyingi alizostahili. Simba wakiwa kwenye shamrashamra hizo, Arab Contractors wakapiga haraka haraka kona iliyotokana na kazi nzuri ya Mwameja. Yaani Simba wanaendelea kupongezana, wenyeji wanaandika bao la pili na la mwisho lililowavusha mpaka raundi nyingine.
Nimelikumbuka tukio la penalti ya Mwameja, shamra shamra za Simba na bao la kuua la Arab Contractors kutokana na shamrashamra tulizo nazo sasa baada ya kuwafunga wagumu Morocco mabao 3-1 hapa nyumbani. Tumeshangilia, tumepongezana, tumefurahi na tumetamba. Kwa mashujaa wetu, hilo linatosha. Baada ya Mwameja wetu (vijana wote wa Taifa Stars) kufanya kazi kubwa ya kuokoa penalti kwa kutoa kona (kushinda 3-1), tusipongezane sana mpaka kuisahau kona (mechi tatu zilizobaki za kundi letu) ili wapinzani wetu (Morocco, Gambia na Ivory Coast) wasitushtukize bao la kona (wakatupa matokeo mabaya) na kutolewa mashindanoni (kukosa nafasi ya juu)
Ni vizuri tusahau matokeo hayo mazuri na kujizatiti kufanya vizuri mechi zilizobaki kama ambavyo Simba walipaswa wasahau mara moja kazi nzuri ya Mwameja, Mei 1996 nchini Misri na kujielekeza kuokoa kona.
Tunapaswa tuanze haraka kupanga mikakati ya kufanya mazoezi ya nguvu kila kalenda itakaporuhusu kwa hilo. Tuwahi kupeleka maombi ya mechi za kimataifa za ugenini na nyumbani za timu za viwango vinavyolingana na vya Ivory Coast na Morocco ambavyo kiuwezo viko juu ya kile cha Gambia. Kamwe tusiidharau Gambia kwani nao si wadogo wa soka na kama tuna uhakika wa kuwapiga, tukawapige kwao mabao mengi kwani kuna uwezekano mshindi wa kundi letu akaamuliwa kwa wastani wa magoli. Nasisitiza Gambia tusiwadharau na mechi dhidi yao ya ugenini tuicheze kwa tahadhari kama tutakapocheza ugenini na Morocco.
Kocha wetu Kim Poulsen aendelee kuachwa huru apange mambo yake na tusimshauri wachezaji gani aongeze na kina nani awaache. Ni wazi ataongeza wachezaji kwa sababu za msingi za kitaalam na atawaacha baadhi ya waliopo kwa sababu kama hizo lakini itapendeza kama atakilea kikosi chake cha sasa kama kilivyo.
Matajiri wa Yanga na Simba nao waache kuvuruga wachezaji wetu kwenye kipindi cha majukumu makubwa ya kitaifa kwa kuwashawishi kwa ahadi kubwa kubwa kujiunga na timu zao. Hilo litawachanganya. Kuna muda muafaka wa kuuza na kununua wachezaji lakini majukumu mazito ya kimataifa yakiwa katika kipindi kisicho cha usajili, vijana wasivurugwe.
Ushindi wetu dhidi ya Morocco usitufanye tuwadharau hao pamoja na Ivory Coast na Gambia. Wote tunapaswa tuwaheshimu sana kwa soka lao kubwa linaloheshimika duniani kutokana na kuwa na wachezaji maarufu wanaojulikana duniani lakini tusiwaogope kama ambavyo hatukuwaogopa Morocco na kuwapiga mabao mengi hapa nyumbani.
Mwisho tunatoa rai kwamba magazeti nchini Tanzania yaache utaratibu wa kutoa alama za utendaji za wachezaji wetu baada ya mechi za kimataifa. Wote wanajituma kwa uwezo wao lakini mmoja anapopewa alama 3 kwa 10 na mwingine 9 kwa 10 hapo kuna kukatishwa tamaa kwa yule mwenye alama 3 na kama alichangia kumfanya mwenzake apate 9 kwa 10, mechi zijazo huyo wa alama 3 hatatoa ushirikiano kwa yule wa alama 9 ili ashuke. Utaratibu huu hauna tija bali unashusha hamasa na unapoteza hali ya kujiamini huku ukiathiri ushirikiano kitimu.
Vipaji tunavyo na tukijipanga vizuri tutakwenda Brazil mwakani. Cha msingi kwa sasa tusimzunguke Mwameja kumpongeza kwa kuitoa penalti ikawa kona bali tujizatiti kuwachunga wachezaji wa Arab Contractors wasitufunge bao la kona. Kwa kuwafunga Morocco tusione kama tumemaliza kazi. Mungu ibariki Tanzania.
Comments
Loading…