Muda mwingi nilikuwa nimekaa jukwaani natazama hali nzima ya uwanja wa Benjamin William Mkapa maarufu “Lupaso”. Hali ilikuwa haitii matumaini kabla hata mchezo haujaanza. Asilimia kubwa ya majukwaa yalikuwa tupu.
Kumbuka hii mechi ni mechi ambayo tulikuwa nyumbani, tulikuwa tunacheza na timu bora barani Afrika, DR Congo na ni mechi ambayo tulihitaji ushindi ili tujiweke katika mazingira mazuri ya kufuzu Afcon 2025 nchini Morocco.
Umuhimu na ugumu wa mchezo huu tulitegemea kama Taifa zima tuungane kwa pamoja ili tufanikishe ndoto yetu. Kama Taifa tumekubaliana tunataka kufuzu Afcon 2025, kwenye makubaliano yetu neno ushirikiano linatakiwa liwe katikati yetu.
Neno hili kwa jana halikuwepo kuanzia nje ya uwanja. Mashabiki hawakujaza ule uwanja ili kuwapa nguvu vijana wetu na hata wale ambao walikuwepo uwanjani hawakuwa na nguvu za kuwasukuma vijana wetu wapambane.
Shabiki jukwaani anaweza kumkaba mpinzani kwa kumzomea na anaweza kumshambulia mpinzani kwa kumshangilia kwa nguvu Taifa Stars. Kitu hiki hakikuwepo kabisa kwenye majukwaa ya uwanjani.
Mashabiki tulikuwa kimya muda mwingi hatukutimiza majukumu yetu ya mshingi ya kuwazomea DR Congo na kuwashangilia Tanzania. Tulikuwa tunasubiri tukio zuri ili tushangilie.
Vijana walitoa jasho lao, walipambana sana lakini sisi hatukupambana nao kabisa. Ile nafasi ya sisi kuwa mwenyeji wa mchezo hatukuitumia kwa ufanisi mkubwa sana.
Wakati natazama mpira jana hasa kipindi cha pili, niliona tofauti kubwa iliyokuwepo kati yetu Tanzania na wenzetu DR Congo. Tofauti yetu ilikuwa kwenye mabadiliko ya wachezaji ambayo tuliyafanya na wao kuyafanya kipindi cha pili.
Sisi tulimtoa Lusajo Mwaikenda ambaye alionekana kuchoka na kuzidiwa kasi ya mchezo. Lakini swali kubwa lilikuwa, ni nani ambaye angechukua nafasi ya Lusajo Mwaikenda na kucheza kiwango kikubwa au kiwango kinachomkaribia Lusajo Mwaikenda?
Benchi letu halikuwa na mchezaji wa kiwango sawa au kinachokaribiana na Lusajo Mwaikenda kwenye nafasi ile ya beki wa kulia ndiyo maana aliingia Bakari Mwamnyeto kucheza kama beki wa kati na Dickson Job kucheza upande wa kulia ambapo kiuhalisia siyo nafasi yake ya kucheza.
Moja ya wachezaji ambao walicheza vyema jana hasa kipindi cha kwanza na kipindi cha pili mwanzoni ni Mudathiri Yahya. Mudathiri Yahya jana alitoa kila kitu ambacho alikuwa nacho lakini ilifika hatua akachoka.
Baada ya kuchoka na kushindwa kutimiza majukumu yake mengine kwa wakati alifanyiwa mabadiliko na akaingia Himid Mao. Himid Mao hakuwa na uwezo wa kucheza katika kiwango kikubwa kama ambacho Mudathiri Yahya alikuwa nacho kwa jana.
ulifikiria kama Mohamed Hussein kama angeumia jana nani angeingia kuchukua nafasi yake na kucheza kwa kiwango kikubwa kama alichokuwa anakionesha katika mchezo wa jana?
Ulifikiria nani angeweza kucheza katika kiwango kama au kinachokaribiana na Feisal Salum “Fei Toto” kama jana angeumia ? Kila ukiangalia benchi letu la timu ya taifa lilikuwa limepwaya.
Benchi letu halikuwa na wachezaji wenye viwango vya kwenda kubadilisha hali ya hewa uwanjani. Ulitazama mabadiliko ambayo timu ya Taifa ya DR Congo waliyoyafanya? Kimsingi mabadiliko yale ndiyo yaliamua mchezo wa jana.
Mfungaji wa magoli mawili ya jana Meshack Elia alitokea benchi jana na akabadili hali ya hewa ya jana. Fiston Mayele ambaye aliingia jana alikosa nafasi ya wazi akiwa na golikipa.
Hii inaonesha namna ambavyo kikosi cha DR Congo kilikuwa kipana kuzidi kikosi chetu. Na cha kusikitisha zaidi kikosi chetu kilikuwa finyu kuanzia jukwaani kwa sisi mashabiki mpaka wachezaji ambao walikuwa uwanjani.
Comments
Loading…