Kuna msemo maarufu wa waswahili ambao unasema kwamba kazi ngumu mpatie mnyamwezi. Msemo umekuja katika lugha ya Kiswahili kutokana na uhodari wa watu wa kabila la Wanyamwezi katika ufanyaji kazi. Kwani wamekuwa wanasifika kwa utendaji kazi kwa umahiri pamoja na kwa kujituma kwa hali ya juu. Kutokana na uchapakazi wao Wanyamwezi walikuwa wanaweza kujichanganya na watu wa maeneo mbalimbali nchini Tanzania na waliaminiwa sana katika kupewa kazi hususani kazi ngumu yaani zile ambazo watu wengi walikuwa wanaziogopa au walionekana hawaziwezi.
Tabia hii iliwasaidia sana kuweza kuwafanya waishi maeneo mengi tu ambayo hayakuwa makazi yao ya asili kwani wenyeji wa maeneo hayo hawakuona kama Wanyamwezi ni tatizo kuishi nao. Katika mkoa huo kwa miaka mingi sana hawakuwa na bahati ya kuwa na klabu ya kucheza ligi kuu ya soka ndani ya ardhi ya pale. Msimu ulioisha hivi karibuni mji huo wa wanyamwezi umewakilishwa katika ligi kuu ya soka Tanzania bara na klanu ya Tabora United ambao walikuwa wamejipa jina la Nyuki wa Tabora. Wakazi wengi wa mji huo walikuwa wana matarajio makubwa sana juu ya klabu yao kwamba ingekuwa inasumbua sana na ingemaliza ligi kuu katika hatua za 10 bora.
Klabu hiyo ilifanikiwa kuingia ligi kuu ya Tanzania bara katika msimu wa mwaka juzi na kuingia kwake katika ligi kuu ilikuwa ni stori yenye kusisimua. Wakati wanakaribia kuanza ligi klabu hiyo ilipata pigo la kusimamishwa kwa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo bwana Yusuph Kitumbo pamoja na aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo bwana Ulimboka Mwakingwe kutokana na makosa ya nidhamu ambayo waliyafanya wakati wako daraja la kwanza. Wakaanza msimu bila ya huduma ya aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo ambaye ndiye aliyeipandisha timu daraja katika msimu ambao uliotangulia.
Mechi yao kwanza ya ufunguzi wa ligi kuu walicheza dhidi ya klabu ya Azam football club wakati kabla mechi haijaanza klabu hiyo ilipata changamoto ya baadhi ya wachezaji wake wa kigeni kuwahawajapewa vibali vya kuwaruhusu wafanye kazi nchini Tanzania kwa hivyo hawakuweza kucheza kwenye mchezo huo na iliwalazimu kuingia uwanjani kwenye mechi hiyo huku wakiwa na wachezaji pungufu. Mechi hiyo haikuweza kuchezwa dakika zote 90 kwani mchezaji wa Tabora united alimchezea rafu mchezaji wa Azam ambako ikapelekea kuadhibiwa kwa kupewa kadi nyekundu. Tukio hilo lilipelekea Tabora united kuwa na wachezaji wachache sana kuzidi kiwango kinachoruhusiwa kuchezana hivyo kupelekea msimamizi wa mechi hiyo kuisimamisha mechi hiyo na kutomalizika kwa dakika 90 na hivyo Azam wakapewa ushindi. Kisaikolojia kuanza huku kunaweza kukawa kuliwaathiri Tabora United kwa namna moja ama nyingine. Mechi zilizofuatia hawakufanya vizuri sana na hii inawezekana ilitokana na kuanza vibaya kwa msimu.
Kuna dalili pia kwamba klabu hiyo kuna nyakati haikuwa na hali nzuri kifedha kutokana na kwamba ililipa faini nyingi sana ambazo zilitokana na kushindwa kuheshimu mikataba ya baadhi ya wachezaji wake. Wachezaji hao walishitaki klabu hiyo FIFA na waliwashinda huko kwenye mahakama ya soka, matukio ambayo walipelekwa mahakama ni kama ifuatavyo: Mnamo tarehe 7/1/2023 TFF ilifungia klabu ya Tabora United kutosajili wachezaji mpaka itakapimlipa mchezaji wa kimataifa Evariste Mutambayi kutoka Congo.Mnamo tarehe 1/11/2023 shirikisho la soka Tanzania liliifungia klabu ya Tabora United kutosajili mpaka itakapomlipa mchezaji wa kimataifa kutoka katika taifa la Congo Fabrice Ngoyi.
Mnamo tarehe 1/11/2023 klabu ya Tabora United ilipewa adhabu ya kutosajili mpaka watakapomlipa mchezaji wa kimataifa kutoka GHANA Asante Kwasi aliyekuwa anawadai stahiki zake na ambaye aliwafungulia shauri katika shirikisho la soka duniani FIFA.Mnamo tarehe 02/10/2023 shirikisho la soka la Tanzania TFF lilitoa adhabu ya kuwafungia kusajili wachezaji klabu ya Tabora United kutokana na kuwa wanadaiwa malimbikizo ya mshahara pamoja na ada za usajili wachezaji wao wawili ambao ni Emmanuel Lamptey na Collins Gyamfi.
Kadiri siku zilivyosonga mzunguko wa pili wa ligi ndio timu hiyo ikawa na hali mbaya kimatokeo na mpaka imepelekea kuwa katika hatua ya timu ambazo ziko hatarini kushuka daraja. Matokeo ya mwisho wa msimu hayakuwa mazuri sana na walifikia hatua ya kuingia kwenye hali ya kucheza mechi za mtoano. Katika mechi za mtoano awamu ya kwanza walicheza na klabu ya JKT Tanzania ambapo katika mechi zao dhidi ya JKT walifungwa mechi zote mbili kuanzia mechi ya kwanza ambayo walicheza ugenini katika uwanja wa Meja Isamuhyo ambao upo jijini Dar es salaam mpaka mchezo wa marudiano ambao waliucheza katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambao upo mkoani Tabora.
Kushindwa kuibakisha klabu yao katika ligi kuu kutawafanya wawe wameshindwa kuwaheshimisha wanyamwezi ambao ndio wakazi asilimia kubwa ya mkoa wa Tabora na ambao huwa mizigo mizito wanaibeba wao.
Comments
Loading…