Ushindi wa Ivory Coast wa mabao 3-0 dhidi ya Sudan jana uliwahakikishia kuwa vinara wa Kundi B la michuano ya Kombe la Chalenji na hivyo kutoa nafasi kwa timu ya taifa ya Rwanda kuvaana na wenyeji Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ katika robo fainali ya michuano hiyo itakayochezwa keshokutwa Jumatano.
Mshambuliaji Emmanuel Okwi wa timu ya taifa ya Uganda akijaribu kumpita bila mafanikio kipa Boniface Olouch wa timu ya taifa ya Kenya wakati wa mechi yao ya Kundi C la michuano ya Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Ushindi wa Ivory Coast uliwapaisha kileleni baada ya kufikisha pointi sita na kufuatiwa na Rwanda waliomaliza katika kundi lao wakiwa na pointi tano.
Stars walimaliza katika nafasi ya pili pia katika kundi lao la A baada ya kufikisha pointi sita, moja nyuma ya vinara Zambia.
Zanzibar waliomaliza katika nafasi ya tatu, walifuzu pia kucheza nusu fainali baada ya kuwa miongoni mwa timu mbili zilizomaliza katika nafasi hiyo huku zikiwa na matokeo bora zaidi kwenye makundi yao na watacheza Jumatano pia dhidi ya wana robo fainali wengine, Uganda.
Mechi nyingine za robo fainali ya michuano hiyo zitaanza kuchezwa kesho ambapo Zambia watacheza dhidi ya Ethiopia na Ivory Coast watavaana na Malawi.
Mechi nyingine ya jana iliyohitimisha timu nane zilizotinga robo fainali ya michuano hiyo, Kenya walitota kwa mechi ya tatu mfululizo baada ya kukubali kipigo cha magoli 2-0 kutoka kwa mahasimu wao, mabingwa watetezi Uganda ambao hatimaye walimaliza katika kundi lao C la michuano hiyo wakiwa vinara kwa kuwa na pointi saba na kufuatiwa na Malawi waliofikisha pointi tano.
Magoli ya ushindi ya mabingwa watetezi Uganda yalifungwa katika dakika ya 83 na mshambuliaji Emmanuel Okwi wa ‘Wekundu wa Msimbazi’, Simba na Andy Mwesigwa aliyefunga kwa penati katika dakika za majeruhi.
Wakati huohuo, kocha wa Kenya, Jacob Ghost Mulee alitangaza kujizulu kuifundisha timu hiyo bada ya kufungwa mechi zao zote za hatua ya makundi na kusema kwamba ameridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na vijana wake, lakini akasikitishwa na maandalizi yao duni ya kabla ya michuano.
CHANZO: NIPASHE
Comments
Loading…