Uwanja wa Wembley Jumanne hii uligeuka kama eneo la maadhimisho ya umoja na mshikamano wa Ulaya.
Katika mechi baina ya England na Ufaransa, wachezaji, washabiki na viongozi mbalimbali waliweka kando tofauti zao na kuwalilia watu 129 waliokufa jijini Paris.
Zaidi ya washabiki 70,000 waliofika kwenye uwanja huo wa taifa wa England, walishirikiana kuimba Wimbo wa Taifa wa Ufaransa, kuonesha mshikamano dhidi ya magaidi wanaotishia maisha na mali.
Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF) lilipokea ofa ya Chama cha Soka (FA) cha England kufuta mchezo huo kutokana na huzuni iliyokuwapo, lakini FFF wakasema wangesonga mbele na kucheza.
Baadaye wakasema kwamba ilikuwa muhimu mchezo huo kufanyika, ili kuonesha mshikamano wa hali ya juu walio nao jirani hao wa Ulaya Magharibi.
Makocha Roy Hodgson (England) na Didier Deschamps waliweka mashada ya maua kwa kumbukumbu ya wafu hao na minara ya Wembley ilipambwa kwa rangi za bendera ya Ufaransa – bluu, nyekundu na nyeupe.
FA ilitoa klipu ya wimbo huo wa taifa wa Ufaransa kabla na kuwaomba washabiki wajifunze ili wauimbe kwa nguvu kuonesha dunia kwamba wote wapo dhidi ya ugaidi.
Wachezaji wa Ufaransa walionekana kuwa na majonzi mengi na kupata hisia kali wakati washabiki wakiimba, ambapo mchezo ukielekea ukingoni wimbo huo uliimbwa tena kwa sauti kubwa na anga kuzizima.
Mechi hiyo ilimalizika kwa England kupata mabao 2-0, yaliyofungwa na mchezaji wa Tottenham Hotspur, Delle Ali na nahodha wa Manchester United na timu hiyo ya taifa, Wayne Rooney.
Mechi baina ya Ujerumani na Uholanzi na Ubelgiji na Hispania zilifutwa, kufuatia vitisho vya magenge ya magaidi na wasiwasi uliokuwa umetanda.
Wembley, maeneo yanayozunguka uwanja na pia maeneo mengine nchini England kwa ujumla yanapewa ulinzi mkubwa na uangalizi wa kuzuia majaribio ya milipuko kutoka kwa magaidi.
Ufaransa imeanza kuchukua hatua kufuatilia kwa karibu watuhumiwa wa mauaji hayo huku Ubelgiji, ambayo raia wake pia anatuhumiwa, ikiweka hadhari ya hali ya juu.