in

SOKA: Maofisa usalama kazini walalamika

Wakati Taifa la Uingereza likiwa katika mchakato na mijadala juu ya njia bora ya kurejea kwa mechi za soka kwa ajili ya kumaliza msimu wa 2019/2020, maofisa usalama kazini wamlalamika kwamba wanatengwa.

Maofisa hao wanasema kwamba mchakato umeanza ukishirikisha wadau kadhaa na mikutano imefanyika lakini hadi sasa mchango wao unakosekana, wakionya kwamba mipango isiyokamilika huishia kwenye majanga.

‘Project Restart’ ni mpango unaoratibiwa na Bodi ya Ligi Kuu ya England (EPL) kwa ajili ya kuona jinsi msimu utakavyomalizika, zikiwa zimebaki mechi 92 miongoni mwa klabu 20 za EPL na mpango unaodhaniwa utapitishwa ni kucheza katika viwanja huru pasipo watazamaji.

Haijajulikana lini hasa soka itarejea kwani hadi sasa kuna marufuku ya mikusanyiko na watu wanatakiwa kubaki majumbani mwao wakati huu wa janga la virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu. Mechi ziliahirishwa tangu Machi mwaka huu, kocha Mikel Arteta akipata maambukizi na kujitenga. Alishapona.

Maofisa usalama wa ngazi za klabu wana hofu kwamba wanavyoachwa kando na wasiposema sasa, watakuja kulaumiwa ikiwa mambo yatakwenda vibaya baadaye, kama vile maambukizi mapya kuongezeka.

Wanadhani kwamba wanatakiwa kushirikishwa katika majadiliano ili wachezaji, waamuzi, makocha na wafanyakazi wa viwanja husika wasije kudhurika. Tayari baadhi ya wachezaji, akiwamo Sergio Aguero wa Manchester City, wametangaza kuogopa kurudi uwanjani kwani ni hatari kwao na familia zao.

Chama cha Maofisa Usalama Kazini katika Soka (FSOA) ambacho wanachama wake ni waajiriwa wa klabu na ambao kwa kawaida wangekuwa na wajibu wa kuandaa randama kwa ajili ya kutathmini viwanja, kinaeleza masikitiko yake kwamba klabu zinaonekana zikijiandaa kuanza mazoezi wakati maofisa usalama kazini wengi wamepewa likizo za lazma au wanafanya kazi kutoka majumbani mwao.

FSOA inahofu kwamba bado maandalizi si ya kutosha na kwamba huenda majanga yakatokea baadaye, hasa kwenye ligi za chini ambako uangalizi na umakini ni mdogo zaidi. Matatizo ya kiusalama kazini yakizuka, kwa kawaida ni maofisa usalama kazini wanaolaumiwa, na sasa chama kinataka kuondokana na lawama hizo tangu sasa.

“Wajibu wa maofisa usalama kazini unaonekana kupotea kwenye majadiliano ya Project Restart. Wasiwasi wetu juu ya wanachama na wenzetu hawa ni kwamba asilimia kubwa ya klabu zinashinikiza kuelekea kwenye kuanza kwa mazoezi na kisha ligi kurudia wakati maofisa usalama wengi ama wamepewa likizo za lazima au wanafanya kazi wakiwa majumbani mwao,” akasema Mkurugenzi wa Operesheni wa FSOA, Peter Houghton.

Anaongeza kwamba hali hiyo imewaweka katika wakati mgumu wa kuweza kutathmini hatari zinazoweza kujitokeza kwenye mpango wa kuanza tena ligi katika viwanja vyao husika, kuanzia wakati huu ambapo viwanja hivyo bado vimefungwa. Anaonya kwamba klabu zisianze soka bila tathmini kutoka kwa wataalamu wa eneo hilo na hiyo haiwezi kufanywa huku maofisa husika wakiwa majumbani mwao.

Klabu za EPL zilikutana Ijumaa iliyopita kwa njia ya video kujaribu kuchora ramani kwa ajili ya kuanza tena msimu ambao Liverpool wapo kwenye nafasi kubwa ya kutawazwa mabingwa, wakiwa mbali mno yaw engine huku nafasi za kufuzu kwa michuano ya Ulaya na za kushuka daraja zikiwa wazi kwa timu nyingi.

Klabu hizo zitakutana tena Ijumaa ya wiki hii, ikidhaniwa kwamba mipango ya kuanza tena mechi itakuwa inakamilishwa, japokuwa itabidi kwanza kupata idhini ya polisi, madaktari wa klabu na taasisi ya serikali inayotoa leseni ya usalama wa viwanja. Kwa ujumla itategemea tamko la Serikali Kuu juu ya hali ya Covid-19 na iwapo itaruhusu watu kurudi mitaani.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

EPL viwanja huru

Tanzania Sports

Man U hawataki mkurugenzi wa soka