Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana, Rage alisema ameshasaini fomu za uhamisho pamoja na ya kuthibitisha kupokea fedha za usajili wa mchjezaji huyo TP Mazembe mwishoni mwa wiki.
“Napenda kuweka wazi kuanzia Aprili 30 Samata hatakuwa tena mali ya Simba na badala yake atakuwa mchezaji halali wa TP Mazembe kwa kuwa tayari tumeshapokea fedha za usajili,” alisema Rage.
Rage ambaye baadhi ya wanachama wanamtaka kuachia ngazi Simba kufuatia timu hiyo kupokonywa ubingwa wa Bara mdomoni na Yanga katika mchezo wa mwisho wa ligi kuu, alisema alipokea dola za Marekani 100,000 kutoka Mazembe.
Fedha hizo zilipokelewa Alhamisi, alisema Rage ambaye wanachama wanataka aachie ngazi wakihisi Simba imepokonywa ubingwa kutokana na yeye kukosa muda wa kusimamia tim hiyo kikamilifu.
Mbali na kuwa mwenyekiti wa Simba Rage pia ni mbunge wa Bunge la Jamhuri kwa tiketi ya CCM, mwenyekiti wa chama cha soka Tabora na mwenyekiti wa Jumuiiya ya wazazi mkoani humo.
Kukamilishwa kwa uhamisho huo na Simba kumekuja licha ya timu ya African Lyon aliyokuwa akiichezea Samata msimu uliopita kudai mchezaji huyo ni wake kwa kuwa Simba iliazimwa tu hivyo ndiyo inayopswa kupokea fedha hizo.
“Nasema nikiwa na vithibitisho na kwa kujiamini… Samata ni mali ya Simba na ndio maana tumekubali kumuuza,” alisema Rage kujibu madai hayo yaliyoibuka ghafla tangu kutangazwa kwa dau hilo.
“Endapo ikitokea kuwa Simba hatukufuata taratibu katika kumsajili mchezaji huyo nitakuwa tayari kujiuzulu uongozi na pia sitajihusisha tena na soka,” alisema Rage ambaye ni mbunifu wa kupunguza mashinikizo kila yanapomkabili.
Katika hatua nyingine, mwenyekiti wa klabu ya Simba huyo amesema timu yoyote inayotaka kuwasajili Mussa Hassan ‘Mgosi’, Juma Kaseja au Mohamedi Banka italazimika kulipa dau la dola 100,000.
Comments
Loading…