in

Simba yapeta..

TP Mazembe
Image via Wikipedia

WAWAKILISHI wa Tanzania katika mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika, Simba  jana waliichapa Elan de Mitsoudje ya Comoro mabao 4-2 katika mechi kali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo Simba itakutana na TP Mazembe ambao ni mabingwa DR Congo na mabingwa wa Afrika katika raundi ya pili ya mashindano hayo kati ya tarehe 18,19,20 mwezi Machi na kurudiana kati ya tarehe  01,02,03 mwezi Aprili 2011.

Katika mechi ya jana mpira ulianza kwa kasi huku safu ya ulinzi ya Simba ikiwa chini ya Kelvin Yondani, Juma Nyoso, Haruna Shamte na Juma Jabu, ambapo katika dakika ya sita Simba ilipata faulo baada ya mshambuliaji wake Mbwana Samata kuchezewa rafu nje kidogo ya 18, lakini Mussa Hassan Mgosi alipiga mkwaju dhaifu ulioenda nje.

Mgosi katika dakika ya nane pia aliwalamba chenga mabeki wa Elan de Mitsoudje ya Comoro pembeni ya uwanja na kupiga krosi nzuri, lakini Mbwana Samata akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga aliukosa mpira.

Winga wa kushoto wa Elan, Mohamed Mouien nae alikuwa akiwasumbua mabeki wa Simba, lakini krosi zake nyingi zilikuwa hazitumiwi vizuri na washambuliaji wa timu yake ambao ni Moustackina na mwenzake Madaha Mohamed.

Katika dakika ya 30 Madaha Mohamed wa Elan alikosa bao akiwa yeye na Kaseja baada ya kupiga mpira uliotua mikononi mwa Kaseja.

Madaha Mohamed alirekebisha makosa yake na kuipatia timu yake bao la kuongoza dakika ya 41 baada ya kuchomoka na mpira winga ya kulia na kumchambua kipa Juma Kaseja kwa kupiga shuti kali upande wa kushoto huku mabeki wa Simba wakidhani Madaha alikuwa ameotea.

Kabla ya kwenda mapumziko Mbwana Samata aliisawazishia Simba bao katika dakika ya 44 baada ya kupiga krosi ambayo ilimshinda kipa wa Elan, Youssouf Ahamada ambaye katika jitihada za kuuokoa mpira ule alijikuta akiutumbikiza wavuni.

Mpaka mapumziko timu hizo zilikuwa sare ya bao 1-1.

Simba katika kipindi cha kwanza walikosa mabao mengi kutokana na washambuliaji wake Mbwana Samata, Musa Mgosi na Ally Mohamed Shiboli kutokuwa makini.

Kipindi cha pili kilianza huku Simba wakipeleka mashambulizi katika lango la Elan, ambapo katika dakika ya 48 Simba walipata bao la pili ambalo lililofungwa na Patrick Ochan baada ya Mbwana Samata kupiga krosi iliyomgonga Ochan tumboni na katika jitihada za walinzi na kipa wa Elan kutaka kuokoa mpira huo walijikuta wakijichanganya na kuuacha mpira ukitinga wavuni.

Katika dakika ya 53 kocha wa Simba, Patrick Phiri alimtoa Mohamed Banka na kumuingiza Jerry Santo mabadiliko ambayo yalisaidia kuimarisha safu ya kiungo.

Kama haitoshi mshambuliaji Mbwana Samata aliiongezea Simba bao la tatu katika dakika ya 56 kwa shuti kali la umbali kama mita 30, bao hilo lilitokana na faulo aliyokuwa amefanyiwa Patrick Ochan.

Kocha wa Elan, Youssof Bachiro alifanya mabadiliko katika kikosi chake dakika ya 58 baada ya kumtoa kipa wake Youssouf Ahamada na kumuingiza Mohamed Hassan.

Baada ya mabadiliko hayo, Elan ilipata bao la pili katika dakika ya 63 ambalo lilifungwa na Abdoulhouda Abdouleafor.

Pia timu zote mbili zilifanya tena mabadiliko kwa wachezaji wao, ambapo Elan ilimtoa Madaha Mohamed na kumuingiza Zaidou Soilihi wakati Simba ilimtoa Ally Shiboli na nafasi yake ilichukuliwa na Amri Kiemba.

Mabadiliko hayo yalionekana kuinufaisha Simba kwa sababu katika dakika ya 72 Amri Kiemba ambaye alitokea benchi aliipatia Simba bao la nne akipokea pasi kutoka kwa Haruna Shamte.

Katika dakika ya 88 kocha Phiri alimtoa Rashid Gumbo na kumuingiza Salum Aziz.

Pambano hilo lilichelewa kuanza baada ya mwamuzi Issa Kagabo kutoka Rwanda kugoma kwenda kuanzisha pambano hilo kwa sababu wachezaji wanne wa Simba walikuwa hawana hati za kusafiria.

Baada ya suala hilo kupatiwa ufumbuzi kwa makubaliano ya wachezaji hao kupigwa picha, timu ziliingia uwanjani na muamuzi alianzisha pambano hilo.

Akizungumza mara baada ya mechi kumalizika kocha wa Simba, Patrick Phiri aliwashukuru mashabiki kwa ushangiliaji wao mkubwa katika dakika 90 za mchezo, pia aliwatetea wachezaji wake kwa kukosa mabao akisema ilitokana na umuhimu wa mechi yenyewe.

Mashabiki ni wengi waliojitokeza kushuhudia  pambano hilo, suala lingine ni kwamba ilibidi gari litumike kunyonya maji yaliyokuwa yametuama uwanjani kutokana na mvua zilizonyesha jana mchana.

Katika pambano hilo la jana rais wa Shirikisho la Soka Tanzania TFF, Leodeger Tenga alihudhuria, pia alikuwepo kocha mkuu wa Taifa Stars, Jan Polsen pamoja na Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana Profesa Juma Kapuya.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Premier League – Team news: Rio misses derby clash

Phiri confident of ousting Mazembe