|
||||
WAKATI Yanga wanahitaji kushinda mechi tatu ili kutangazwa mabingwa baada ya ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya Prisons, watani wao wa jadi Simba wameamka na kuisambaratisha Villa Squad 2-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Athumani Iddi ‘Chuji’ aliifungia Yanga bao pekee katika dakika ya 76 ya mchezo ulioshuhudia Tanzania Prisons ikilala 1-0, huku mvua kubwa ikiharibu ladha ya kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Yanga ambayo imejikusanyia pointi 36 hadi sasa inahitaji kushinda mechi tatu kuweza kujitangazia ubingwa mapema zaidi msimu huu.
Simba iliyomaliza vibaya mwaka jana kwa kuandamwa na matokeo mabovu, pamoja na jinamizi la kutimua makocha imeonekana kujiimarisha zaidi raundi hii ya pili.
Ikiwa chini ya Mzambia Partick Phiri, wekundu hao wameshinda mechi mbili za ligi pamoja na jana kuichabanga Villa Squad 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu wa Vodacom, duru ya pili na kufikisha pointi 20.
Washambuliaji Musa Hassan Mgosi na Ulimboka Mwakingwe kila mmoja alifunga bao lake na kuielekeza Villa Squad, njia ya kurudi daraja la kwanza msimu ujao kwa kuendelea kushikilia mkia wa msimamo huo.
Mpira ulikuwa mkali wa vuta nikuvute, ambapo katika dakika kumi za mwanzo Villa Squad ilitawala mpira, lakini ilishindwa kutumia nafasi zao.
Dakika ya 17, beki Juma Jabu alitaka kujifunga mwenyewe, baada ya kumrudishia vibaya mpira kipa wake Ally Mustafa. Hata hivyo kipa aliwahi na kuudaka.
Mussa Hassan Mgosi aliwainua mashabiki wake kwa kuachia shuti kali lililomshinda kipa wa Villa Squad na kujaa wavuni dakika ya 22 baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Juma Nyoso.
Hata hivyo Hemed Shaaban na Ally Kilwa wa Villa Squad katika dakika za 15 na 20 walikosa mabao ya wazi kwa kushindwa kumalizia mipira ya krosi.
Katika dakika ya 30 Simba ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Mohamed Banka na kuingia nahodha wa Tanzania, Henry Joseph na Villa walimtoa Musa na kuingia Idd Moshi
Mwanzoni mwa kipindi cha pili Ulimboka Mwakingwe aliipatia Simba bao la pili kwa shuti kali baada ya kupata pasi kutoka kwa Juma Nyosho.
Kocha wa Simba Patrick Phiri alisema timu yake imecheza vizuri, ndiyo maana walishinda na anaamini wataendelea kufanya vizuri. Lakini aliisifu Villa kwa kuonyesha kandanda zuri kwa kucheza kwa nafasi zaidi.
Naye kocha wa Villa, Ken Mwaisabula alisema amekubali matokeo, kwani anaamini kufungwa ni sehemu ya mchezo na washambuliaji wake hawakuwa makini katika umaliziaji.
Comments
Loading…