in

Simba wanamuhitaji Kotei kuliko Morrison

Wiki mpya inaanza, wiki ambayo ilitanguliwa na wiki ngumu sana kwa upande wa Yanga, wiki ambayo ilikuwa na hali ya sintofahamu katika kikosi cha Yanga , hali ambayo ilianza kutia mashaka kwenye mechi yao dhidi ya Mwadui kama kweli wanaweza kushinda.

Walipoingia ndani ya uwanja akili zao zilikuwa zinawaza mambo mengi zaidi ya ndani ya uwanja kuliko ya nje ya uwanja ndiyo maana walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kushinda mchezo ule ambao awali ulionekana mgumu kutokana na hali ngumu ya nje ya uwanja.

Hali ambayo ilianza baada ya kocha msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa kutofautiana na mshambuliaji wa Yanga, David Molinga baada ya kocha huyo msaidizi kutomjumuisha David Molinga kwenye kikosi kinachoenda Shinyanga kwa ajili ya kucheza na Mwadui FC.

Kocha Charles Boniface Mkwasa alimuona David Molinga hayuko vizuri kwa ajili ya mchezo huu kutokana na kuongezeka uzito kwa kiasi kikubwa , kitu ambacho kilikuwa sahihi kwa kocha huyo kwa sababu yeye alikuwa na dhamana ya kutazama aina gani ya wachezaji ambao wangemsaidia kwenye mechi dhidi ya Mwadui FC.

Wakati Charles Boniface Mkwasa na David Molinga wakiwa wametofautiana , Bernard Morrison alizima simu yake na kuonesha kuwa hakuwa tayari kwenda Shinyanga kwa ajili ya mechi ya Mwadui FC, hakusafiri na timu kwenda Shinyanga.

Kitendo hiki kilikuja na tetesi kuwa Bernard Morrison alikuwa kwenye mpango wa kujiunga na klabu ya Simba SC, nafsi yangu ilitulia kwanza, sikuruhusu kuipa akili yangu itafakari sana kuhusu usajili huu wa Bernard Morrison kwenda Simba.

Ila jana wakati natazama mechi ya Simba dhidi ya Ruvu Shooting akili yangu ikawa inaniambia kuwa inawezekana Simba hawaoni eneo ambalo wanatakiwa kufanya usajili. Mechi ya jana ilinipa majibu kuwa Simba wanatakiwa kuwa makini sana kwa kutazama eneo sahihi ambalo wanatakiwa kusajili.

Nikiwa kwenye jukwaa la uwanja wa Taifa, macho yangu yalitua mpaka eneo la kiungo cha kati hasa eneo la kiungo cha kuzuia ambapo alikuwa anacheza Mzamiru Yassin . Hatuwezi kuongea mengi kuhusiana na kiwango chake kwa sababu katika kwenye majeraha, pia katika kwenye likizo fupi ya Corona.

Mzamiru Yassin aliweza kuzunguka kila eneo la uwanja lakini hakuweza kuilinda safu yake ya ulinzi ambayo kwa muonekano wa kiufundi safu yake ya ulinzi inaongozwa na mabeki wa kati ambao miguu yao imeishiwa nguvu.

Ukiwa na mabeki wa kati ambao miguu yao imeishiwa nguvu lazima uwe na kiungo wa eneo la kuzuia ambaye ana miguu imara na mwenye uwezo wa kuzuia au kupunguza idadi ya mashanbulizi kwenda kwenye safu ya ulinzi.

Hiki hakikuwepo kwa kiasi kikubwa kwenye miguu ya Mzamiru Yassin. Muda huo Jonas Mkude yupo wodini kutokana na majeraha, mchezaji ambaye hucheza eneo hilo. Lakini pamoja na kwamba Jonas Mkude bado yuko Simba, kwa msimu huu safu ya kiungo cha ulinzi ya Simba imekuwa dhaifu ukilinganisha na safu ya kiungo cha ulinzi ya msimu uliopita.

Katikati ya uwanja kulikuwepo na James Kotei ambaye alikuwa na uwezo wa kuilinda safu ya ulinzi ya Simba, Jonas Mkude alikuwa anachukua mipira ambayo James Kotei alikuwa anaipokonya na Jonas Mkude alikuwa anaisambaza kwenda mbele.

Kwa sasa hakuna kitu kama hiki kwa Simba, Mzamiru Yassin hawezi kutibua mipango na kusambaza mipira kwa wakati mmoja, Jonas Mkude naye hawezi kufanya hiyo kazi kwa kiwango kikubwa. Hapa ndipo Simba wanatakiwa kuanza kutazama.

Wasifikirie kumsajili Bernard Morrison, wawaze namna ya kumpata James Kotei ambaye anaweza kuja kuziba madhaifu ya Simba kwa kiasi kikubwa, eneo ambalo Bernard Morrison anacheza ni eneo ambalo lina wachezaji wengi imara katika kikosi cha Simba, watazame eneo ambalo lina udhaifu na wasajili mchezaji wa kuziba udhaifu.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Simba Sports Club

Yanga Kuiadhibu Simba Kwa Morrison ?

Uingereza wameshindwa kukabili ubaguzi

Uingereza wameshindwa kukabili ubaguzi