Filimbi ya mwisho imeacha shangwe

MCHEZO wa soka huwa unamalizika pale filimbi ya mwisho ya mwamuzi inapopulizwa. Filimbi ya mwamuzi ndiyo inathibitisha matokeo ya mchezo ndani ya dakika 90. Katika dakika 90 za mchezo wa Simba na Azam kulikuwa na matukio mengi mazuri na yenye kusisimua. Matukio ya ufundi, kasi ya mchezo, umahiri wa makipa na zaidi ulionesha ni kwanini Ligi Kuu Tanzania ni miongoni mwa zile zenye mvuto Barani Afrika. 

Pia ilionesha ni kwanini Ligi Kuu Tanzania ina mvuto zaidi katika ukanda wan chi za Afrika Mashariki. Hakuna ubishi kuwa ulikuwa mchezo wenye kila aina ya ushindani kuanzia wachezaji binafsi hadi benchi la ufundi. Mashabiki walifanya mchezo huo uwe mzuri zaidi kwa kujazana kwenye dimba la Benjamin Mkapa. Lakini Simba waliokuwa wanaongoza kwa muda mrefu wakiwa na mabao mawili dhidi ya moja la Azam walijikuta wakimaliza dakika 90 kwa kwa kutoshana nguvu. TANZANIASPORTYS inachambua masuala muhimu yaliyojitokeza kwenye mchezo huo.

Bao la mapema

Iliwachukua dakika moja tu kwa mabwanyenye wa Chamazi, Azam FC kupachika bao la kuongoza  kupitia Aziz Gilla katika mchezo ambao ulikuwa na kila presha kuanza mashabiki, makocha na viongozi. Wakati Azam wakiwa wanaongoza bao hilo na kutaka kulilinda, walijikuta nguvu na maarifa yao yakidumu kwa dakika 25 baada ya Simba kupachika safi ya kusawazisha. Simba walipachika bao lao katika dakika 26 kupitia Elie Mpanzu aliwainua vitini mashabiki wao  kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na timu yake kulitengeneza bao hilo. Hata hivyo Simba walilazimika kumtoa beki wao Che Malone baada ya kuumia mguu na nafasi yake kuchukuliwa na Chamou. Bao la mapema halikuwanyima hamasa Simba waliokuwa wanacheza kwa utulivu, huku Azam wenyewe wakiwa na uchu zaidi wa kupachika bao la pili.

Kiwango cha Kimataifa cha Refa

Ahmed Aragija alidhihirisha ni kwanini anapewa mechi ngumu kama hizi. Mwamuzi huyo pia amedhihirisha kwanini yeye ana beji ya FIFA. Weledi, kumudu kasi ya mchezo na kuchukulia kama mchezo wa kawaida tu. Mwonekano wa mwili ulidhihirisha kuwa anajiamini kuliko kawaida na zaidi anamudu mechi zenye kashkash kama hiyo. Ni kama ambavyo waswahili wasemavyo mzigo mzito mpe mnyamwezi. Kwa dakika 90 Ahmed Aragija alitulia kwa kiasi kikubwa. Anajiamini, anaelekeza na anaacha timu zicheze mpira kwa uwazi bila kupuliza puliza filimbi. Mara nyingi alikuwa karibu na matukio yote yanayostahili adhabu ndogo. Alicheka pale ilipobidi. Alitoa onyo pale ilipotakiwa iwe kwa maneno au kadi za njano. Aliufanya mchezo wa Simba na Azam upendeze kote Afrika Mashariki. Mwamuzi alidhihirisha kuwa Ligi Kuu Tanzania ina mvuto na marefa wa kiwango chake ndiyo wanaohitajika.

Mbinu za Azam ni kujihami na kushtukiza

Kujihami kupita kiasi, na kushambulia kwa kushtukiza ni mbinu iliyotumiwa na Azam FC. Wakati wa kushambulia wakivuka mstari wa eneo la katikati kunakuwa na wachezaji watatu wanakimbia kwa kasi; mmoja kulia, mwingine katikati na upande wa kushoto anakuwa mwingine. Mtindo huu nimeona ukifanyw ana Liverpool walipokuwa wakicheza na Man City wikiendi iliyopita. Wachezaji watatu wa mbele wanapovuka mstari wa katikati ya dimba wanakimbia kwa kasi kubwa wakiwa na mpira kulisakama lango la wapinzani wao. Katika mfumo huo unahitaji wachezaji wenye uwezo wa kucheza dakika 90, hasa mawinga Gibril Sillah na Idd Nado. 

Bahati waliyonayo Azam ni beki mahiri Fuentes. Mkolombia huyu anajua maana ya kuwa beki wa kati, maarifa na matumizi ya nguvu za mwili ni miongoni mwa sifa zake. Kushambulia kwa kushtukzia kuliwachukulia aslimia karibia 70 ya mchezo wao. Hata walipoingia kipindi cha pili waliendeleza zaidi hadi pale walipofungwa bao la pili. Kocha wao Rachid Touasi alifanya mabadiliko na kuwaingiza wachezaji wenye kasi zaidi. Kasi yao na kujiamini kulikuwa na uwiano mzuri kwa wakati fulani lakini pia ilikuwa inakaribisha mashambulizi kila walipojiweka kwenye nusu yao.

Makosa ya walinzi wa Simba

Bao la kwanza la Azam lilifungwa sababu ya makosa ya walinzi wawili na kiungo upande wao wa kulia. pasi iliyopotea ilisababisha madhara kwenye lango lao. Azam walionekana kugundua mwanya ulipo upande wa kulia wa Simba kwa sababu beki wake Shomari Kapombe huwa anapanda kushambulia kwa mbinu ya ‘Wing back”. Mfumo huo unamfanya beki w akulia na kushoto kuwa mawinga wa pili katika kusaidia mashambulizi. Azam wakatumia njia hiyo kupiga pasi za haraka katika eneo hilo huku wakitegemea kasi ya Idd Nado katika kuwayumbisha mabeki wa Simba. Kuchezeshwa kwa kasi kila Azam walipopata mpira ni jambo ambalo liliwanyima uhuru Simba. Mabeki wao wanalijikuta wakilazimika kukimbia kw akasi sehemu kubwa ya mchezo huo hasa pale walipokuwa wakishambuliwa. Bao la pili la Azam pia limeonesha makosa ya safu ya ulinzi kwani halikuja katika mazingira yanayotarajiwa. Bao hilo lilifungwa kwa namna ya kipekee mchezaji mmoja kutumia makosa ya walinzi kuwaadhibu.

Kuna Zidane wa Azam mwenye bao gumu zaidi

Uliptangazwa usajili wake, wengi walidhani jina la Zidane ni la utani. Lakini jina lake kamili ni Zidane Sereri. Ni winga mahiri wa kulia na kushoto na pengine anaweza kucheza kama mshambuliaji. Kocha wa Azam aligundua makosa ya safu ya ulinzi ya Simba ilikabiliwa na kuchoka hasa upande wao wa kushoto kwa Mohammed Hussein. Badala ya kuongeza walinzi yeye akaingiza washambuliaji, Sopu na Zidane. Wawili hawa wana kasi kubwa, ni sawa na kwenda kuanza upya kukabiliana na mabeki waliokuwa wanaelekea kuchoshwa na kasi ya Azam. Bao la Zidane Sereri ni gumu sana. namna alivyoutokea mpira, namna alivyomhadaa Mohammed Hussein kisha akamlamba chenga golikipa mahiri Moussa Camara alionesha kuwa alifika Azam kwa kazi ya namna ile. Bao la Zidane Sereri ni la video kama wasemavyo vijana wa ‘vibandaumiza’. Ni bao ambalo lilionesha kujituma, stamina, na nguvu iliyoambatana na maarifa ya haraka sana kutoka kwa Zidane.

Ubora wa Ligi Kuu, Mchezo wa Simba na Azam unadhihirisha sababu ya kwanini Ligi Kuu T anzania inavutia katika ukanda wa Afrika mashariki. Ulikuwa mchezo wenye ufundi mkubwa kutoka pande zote mbili. Mchezo ambao karaka za makocha zinapangwa na kupanguliwa, ushindani wa wachezaji binafsi na masuala ya kiufundi yanaufanya mchezo huo kuwa mmoja ya vitu adimu kuviona kwenye Ligi Kuu Tanzania. Ni lazima tujivunie umahiri wa Ligi yetu hii bila kujali matokeo ya pande zote mbili. Mechi ilikuwa kali sana. pongezi kwa timu zote.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Siri ya Simba hii hapa

Tanzania Sports

Khusanov; sura ya kitoto, roho ya kikatili uwanjani