Vinara wa Ligi Kuu ya Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam, jana ilitumia vizuri dakika sita za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika, kufunga mabao mawili na kukamilisha ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya JKT Ruvu, na hivyo kubakiza pointi mbili kuwa mabingwa wapya mwaka huu.
Kabla ya mechi hiyo, Simba walihitaji pointi tano ili iweze kutwaa ubingwa kabla ya ligi kumalizika, lakini jana walikumbana na ushindani mkali toka JKT waliocheza vizuri na kuwabana wapinzani wao vilivyo.
Mshambuliaji aliye kwenye kiwango, na anayefukuzia tuzo ya ufungaji bora, Mussa Mgosi, baada ya awali kukosa penati ambayo ingeweza kubadilisha matokeo, alifunga bao la pili muda mfupi baada ya kibao cha muda wa nyongeza kunyanyuliwa juu, huku mashabiki wa Simba wakidhani mechi hiyo ingemalizika kwa sare.
Kabla ya bao hilo, kiungo Mohamed Banka alipiga mpira wa adhabu ndogo uliokwenda moja kwa moja wavuni ukimshinda kipa ‘kipenzi’ wa kocha wa timu ya taifa, Maxio Maximo, Dihile na kujaa wavuni katika dakika ya 26.
Makosa ya kipa Juma Kaseja kumuangusha Hussein Bunu wa JKT aliyeingia ndani ya eneo la hatari, yalizaa penati iliyofungwa na Haruna Adolf na kuwa bao la kusawazisha, dakika tano kabla ya filimbi ya mapumziko.
Katika kipindi chote cha kwanza timu zote zilishambualiana kwa zamu, huku Simba wakionekana kuwa juu zaidi na kukosa mabao ya wazi hasa kupitia kwa mshambuliaji wake Mgosi.
JKT Ruvu wangeweza kuwaliza Simba kama Bunu aliyebaki na Kaseja hasingefumua shuti lililokosa mwelekeo wa lango na kupaa juu ya mwamba mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Katika dakika ya 63, Mgosi alishindwa kufunga penati ya pili baada ya ile ya kwanza kuamuriwa kurudiwa kufuatia makosa ya kipa wa JKT kuchomoka kwenye mstari wa goli kabla ya mpira kupigwa, baada ya Nyagawa kuangushwa eneo la hatari.
Mgosi itabidi ajilaumu kushindwa kufunga baada ya mashuti yake mawili katika dakika za 79 na 84 kupaa juu ya lango la wapinzani wao akiwa ndani ya eneo la hatari.
Uhuru Seleman aliihakikishia Simba ushindi baada ya shuti lake kali nje ya 18 kwenda moja kwa moja wavuni, likiwa bao la tatu sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho.
Kocha wa Simba Patrick Phiri, ambaye awali alisema mechi dhidi ya JKT ingekuwa ngumu, alisema amefurahishwa na juhudi walizoonyesha wachezaji wake, kwani walipambana bila kukata tamaa hata baada ya muda wa kawaida kumaliza na hivyo kupata ushindi.
Phiri amesema kuwa, ana matumaini makubwa pointi mbili zilizobaki atazipata kwenye mechi inayofuata dhidi ya Azam itakayochezwa katikati ya wiki hii kwenye uwanja wa Uhuru na kuwa mabingwa rasmi.
Kocha wa JKT, Charles Kilinde, hakutaka kuongea na waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo, huku pia mchezaji wake Mwinyi Kazimoto akionyeshwa kadi nyekundu ya ‘kujitakia’ baada ya mchezo kufuatia kumlalamikia mwamuzi akipinga mabao ya Simba.
simba dume…keep on shinnin!!