Rais wa Shirikisho la mpira wa Rugby Africa, Bw Abdelaziz Bougja ameeleza jitihada mpya kukuuza mchezo huu usiofahamika vizuri barani. Akihojiwa na runinga ya Ufaransa- TV5 Monde- mwishoni mwa wiki jana alisema kati ya jitihada hizo ni kuimarisha Rugby mashuleni kwa wasichana na wavulana.
Bwana Bougja mzawa wa Tunisia – makao makuu ya Rugby Afrika- alisema ni muhimu kuelemisha jamii kuhusu mchezo huu.
“Rugby ni mchezo wa kiungwana sana. Kinyume na soka au michezo mingine mcheza Rugby anatakiwa afuate masharti na kanuni bila ujeuri au kubishana bishana.”
Maneno ya Bw Bougja yanaweza kutatanisha kwa wasiozoea Rugby inayohitaji maguvu na kusukukamana sukumana kwa wachezaji wenye musuli na vifua vipana. Kwa hiyo picha ya utemi na kabali, si ya kweli.
Rugby iligunduliwa na Waingereza karne ya kumi na tisa. Mwaka 1871 baraza la Rugby Football Union, liliundwa kama kitivo cha ligi ya michuano na hatimaye kuwa msimamizi wa Rugby duniani (Rugby Union) hadi leo.
Shirikisho la Rugby Afrika liko chini ya Umoja wa Rugby duniani (Rugby Union) linalosimamia ligi ya kimataifa yaani International Rugby Football (IRF) yenye mataifa mia moja.
Ingawa Tanzania si mshiriki mkubwa wa ligi na michuano ya Rugby barani, ilikuwa kati ya waanzilishi wa Shirikisho la Afrika mjini Tunis, mwaka 1986. Waasisi wengine ni Morocco, Kenya, Seychelles, Senegal, Ivory Coast, Madagascar na Tunisia. Mwaka 2006 Tanzania ilishinda kombe la “Castel Cup” lililoshirikisha majimbo ya kusini : Botswana, Mauritius, Zambia, Zimbabwe, Reunion na Madagascar.
Kinyume na soka, Rugby humtaka mchezaji kuukamata mpira ulio na umbo la papai na kukimbia nao. Sheria ya karne ya 19 iliamuru, “akisharushiwa mpira, mchezaji atakimbia nao mkononi hadi upande wa upinzani. Wakati akikimbia mchezaji wa upinzani ataruhusiwa kumzuia kwa kumtegea, kumkamata au kumgonga.”
Pamoja na kuwa mchezo wa kunyang’anyana, kupigana mieleka, kukimbizana na kuangushana angushana, Rugby haina fujo na huhudhuriwa na kujazana wanawake, watoto na familia. Kwa kuwa ni mchezo wa “waungwana” au wanaojiweza (Gentleman’s sport) mcheza Rugby anapopewa amri au ishara na refa anatakiwa ajibu “Ndiyo, Bwana” (Yes Sir) au “Hapana, Bwana” (No, Sir).
Wakati ambapo kandanda huwa na washiriki 22, Rugby inao 30, yaani 15, kila timu.
Ligi ya kimataifa International Rugby Football (IRF) ina nchi 100 na makao yake makuu yako Ireland, Uingereza. Afrika inawakilishwa na Afrika Kusini (ya pili kidunia), Namibia (23 ), Zimbabwe (26 ), Uganda (31), Kenya (32) , Tunisia (34) na Madagascar (36). Tanzania haipo kabisa. Uingereza, mgunduzi wa mchezo, inashika nafasi ya tatu.
Moja ya sababu za Tanzania si mhusika mkubwa wa Rugby ni kutokana na historia ya mchezo. Ilipoanzishwa Tanganyika mwaka 1956, Rugby ilikuwa shughuli ya Wazungu na Walowezi wa Afrika Mashariki. Hatimaye wenyeji walianza kucheza miaka ya 1970, lakini hadi leo, tumezidiwa na wenzetu wa Kenya na Uganda wenye maingiliano zaidi na utamaduni wa Kizungu.
Kiuchumi, michuano ya Rugby haiingizi mamilioni ya fedha kama Kandanda, Ngumi, Tennis au Golf. Mbali na kujenga ukakamavu, Rugby ni mjenzi mzuri wa afya ya watoto, kupambana na unene na kuimarisha nidhamu masomoni.