‘Project Big Picture’
Mpango unaosukwa na Manchester United na Liverpool katika kubadili mwelekeo wa soka ya England, ukienda kwa jina la ‘Project Big Picture’ unatarajiwa kuangukia pua.
Habari za mradi huo zilivuja Jumapili hii na klabu 18 za Ligi Kuu ya England (EPL) hazikubaliani na mageuzi hayo, huku West Ham wakiwa klabu kubwa inayoupinga kwa nguvu zote.
Tayari maofisa mbalimbali wa kwenye klabu na wa idara na wizara wamegusia habari ya mpango huo na inaonekana kwamba hata Ofisi ya Waziri Mkuu haitambui na haitarajii kwamba utapitishwa.
Ilivyo ni kwamba, Manchester United na Liverpool wanataka kuona kwamba klabu za Ligi ya Soka ya England (EFL), kwa maana ya zilizo chini achilia mbali zile za Ligi Kuu ya England (EPL) zipate mgawo wa pauni milioni 250 wagawane sasa miongoni mwao, pamoja na asilimia 25 ya mapato yatokanayo na dili za televisheni zitakazopatikana EPL.
Klabu hizo, zikiongozwa na Mwenyekiti wa EFL, Rick Parry, zimekuwa zikidai fedha kutoka EPL kwa muda sasa, kutokana na ukweli kwamba zimepigika kifedha, hasa kutokana na kutokuwapo watazamaji, na hivyo viinglio kutokana na janga la Covid-19.
Wazo zaidi ni kwamba kwa kusaidia klabu za EFL, zile klabu kubwa zitakuwa zinatengeneza piramidi ya soka inayoonekana kuwa ndio mwenendo wa maisha nchini. Tayari mpango huo upo katika shinikizo la kukataliwa, ambapo klabu hizi mbili ambazo ndizo watani wa jadi wa asili nchini, wanakosa uungwaji mkono.
Mkutano mkuu maalumu wa wadau unatarajiwa kuingiza wadau kwenye majadiliano makali, kwani kuna mpango wa kupunguza ukubwa wa EPL, kutoa fedha nyingi zaidi kwa EFL na kuongeza maslahi kwa klabu tisa zilizokaa kwa muda mrefu zaidi EPL.
Hakuna hata klabu moja ya EPL iliyojitokeza kuunga mkono mradi huo, huku baadhi zikilalamikia jinsi mpango huo ulivyoandaliwa kwa siri bila kushirikisha wadau wote kwa usawa. West Ham ambao wangeweza kufaidika na mpango huo, wanadaiwa kushituka kuusikia.
Katika hatua nyingine inayoonesha kuongeza shinikizo, Serikali yenyewe imechagiza mpango wenyewe, ikitaka wadau wajikite kwenye kusaidia klabu zilizo hoi kutokana na Covid-19. Mtendaji Mkuu wa EFL, David Baldwin alijiuzulu miezi minne tu tangu aanze kazi hiyo na Parry anaonekana kuwa kiongozi pekee anayeunga mkono mpango huo.
EFL imejitetea ikisema kwamba kuondoka kwa Baldwin hakuhusiani na sakata la mradi huo wa ‘Project Big Picture’ na kwamba maamuzi yake yalichukuliwa kabla ya mapendekezo ya mpango huo kuwekwa hadharani wikiendi iliyopita.
Klabu 20 za EPL zinatarajiwa kukutana kwa njia ya mtandao na ni wazi zitajadili na kuua mradi huo hata kabla haujaanza. Mpango huo unataka kuona zile klabu sita kubwa – Liverpool, Manchester City, Manchester United, Chelsea, Arsenal, Tottenham Hotspur na nyingine tatu – West Ham, Everton na Southampton zikipewa udau wa muda mrefu na haki za kupiga kura zaidi.
EPL ya mfumo wa sasa ilianza rasmi 1992 na kwa klabu nyingine kupewa nguvu zaidi ikiwamo kupiga kura kutaondoa ushindani wa kweli. Wanahoji pia suala la kuweka pamoja mapato yatokanayo na dili za televisheni kutangaza na kuonesha mpira pamoja na matangazo yake ya biashara, ikionekana kwamba hakuna uhakika wa kuongeza mapato.
Waziri wa Utamaduni, Oliver Dowden anasema anaogopa kwamba mpango huo ni sawa na kunyakua mamlaka.
Comments
Loading…