*West Brom wawabomoa West Ham FA
Aston Villa wamemtangaza Tim Sherwood kuwa kocha wao mpya hadi 2018, akichukua nafasi ya Paul Lambert alieyefukuzwa kazi baada ya timu kuzama kwenye eneo la kushuka daraja na kutoshinda mechi 10 mfululizo.
Sherwood aliyekuwa kocha wa Tottenham Hotspur kisha akafutwa kazi, atatakiwa kuwafufua Villa ambao katika mechi zilizopita walifungwa na Arsenal 5-0 kisha wakapoteza kwa mabingwa watetezi, Manchester City na kwenye mechi 10 zilizopita wamefunga mabao mawili tu.
Sherwood (46) alichukua nafasi ya Andre Villas-Boas klabuni Spurs Desemba 2013 lakini akafukuzwa mwishoni mwa msimu uliopita na tangu wakati huo hakuwa na kibarua popote. Ameeleza kwamba ni heshima kubwa amepewa kufundisha moja ya klabu kubwa zaidi kwenye soka ya England.
Eneo la ushambuliaji linaonekana kuwa na tatizo kubwa, ambapo kinara wao Christian Benteke hayupo kwenye kiwango kizuri na pia kabla ya hapo alikuwa na tatizo la utimamu wa mwili. Katika mechi 25 wamefunga mabao 12 tu, pungufu kuliko timu yoyote ile katika historia ya Ligi Kuu ya England.
Sherwood alikuwa akitajwa tajwa kuchukua nafasi ya ukocha Queen Park Rangers (QPR) baada ya kocha wao, Harry Redknapp kuacha kazi kwa maelezo kwamba anakwenda kufanyiwa upasuaji wa miguu, lakini timu ikiwa katika hali mbaya. Mechi iliyofuata baada ya kuondoka kwake walishinda.
Villa wanashika nafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na pointi 22 na mizania ya mabao -22, mbaya kuliko timu nyingine yoyote katika hatua hii ambapo kila timu imeshacheza mechi 25.
WEST BROM WAWABOMOA WEST HAM 4-0
Katika michuano ya Kombe la FA, West Ham wa kocha Sam Allardyice wameonesha unyonge wa aina yake, baada ya kukubali kibano cha mabao 4-0 kutoka kwa West Bromwich Albion wanaonolewa na Tony Pulis.
Mchezaji aliyesajiliwa kwa pauni milioni 10, akivunja rekodi ya West Brom, Brown Ideye alifunga mabao mawili, mengineyakifungwa na James Morrison na Saido Beraniho, hivyo kuwapeleka West Brom robo fainali ya michuano hiyo.
Mchezaji wa West Ham aliyeingia dakika ya 60, Morgan Amalfitano alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumsukuma usoni Chris Brunt na kabla ya hapo alishapewa kadi ya njano kwa mchezo mbaya.
Katika mechi nyingine, Liverpool waliopata kutwaa kombe hilo mara saba wameendelea kuchanua kwa kuwafunga Crystal Palace 2-1 kwa mabao ya Daniel Sturridge na Adam Lalana huku la Palace likifungwa na Fraizer Campbell mwenye uzoefu wa kuwafunga vigogo.
Liverpool yashinda
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers alimsifu Sturridge, akisema kurejea kwake ndiyo sababu ya timu yake kurudi katika hali nzuri na kushinda mechi baada ya kuwa taabani kwa muda mrefu tangu kuanza kwa ligi kuu.
Matokeo mengine ni Blackburn kuwacharaza Stoke 4-1 na Derby kulala kwa Reading 2-1. Jumapili hii Arsenal wanajitupa uwanjani kucheza na Middlesbrough waliowatoa mashindanoni Manchester City.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho, amesema anatarajia rafiki yake, Aitor Karanka anayewafundisha middlesbrough atamfurahisha kwa kuwafunga Arsenal ambao ni mahasimu wake. Chelsea walishatolewa kwenye mashindano hayo.
Mechi nyingine ni baina ya Aston Villa wanaowakaribisha Leicester huku Bradford wakichuana na Sunderland, kwenye mechi ambayo kocha wa Sunderland, Gus Poyet amewaonya wachezaji wake wasitoe pasi za nyuma wala pembeni, bali wasonge mbele kufunga mabao, akisema pasi zao ni za hovyo.
Comments
Loading…