SERIKALI imelaani kitendo cha Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) cha kutangaza kuvunja uhusiano na Shirikisho la Soka (TFF) kwa madai kuwa kinanyimwa mgao wa dola 250,000 za Kimarekani, ambazo hutolewa kila mwaka na shirikisho la mchezo huo ulimwenguni, Fifa, ikisema hizo si fedha za mgao.
ZFA ilizua kizaazaa wiki iliyopita ilipotangaza kuwa imevunja uhusiano na TFF kushinikiza ipate mgao wa fedha hizo, ambazo hutolewa kwa nchi zinazoendelea duniani kusaidia kukuza mchezo huo. Tamko hilo lilisababisha Serikali ya Mapinduzi kutangaza kutounga mkono uamuzi huo.
Jana, baada ya kuibuliwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera alitoa ufafanuzi, akisema kuwa fedha hizo kutoka Fifa hutumwa kwa ajili ya maendeleo ya soka kwa pande zote mbili na si kwa ajili ya kugawia vyama.
”Suala la mgawo wa fedha za Fifa haliwezekani ni kwa ajili ya maendeleo ya soka ya pande zote mbili. Fifa haitoi fedha kwa ajili ya mgao,” alisema kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Dimani, Hafidhi Ali Tahir (CCM) aliyetaka kujua sababu za TFF kutumia fedha hizo, ambazo ni sawa na Sh milioni 260 za Tanzania, bila ridhaa ya ZFA.
ZFA inahesabiwa na Fifa kuwa ndani ya TFF, ambayo inatambuliwa kuwa chama kinachosimamia uendeshaji soka nchini. Lakini Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) na Baraza la Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki (Cecafa) vimeipa Zanzibar hadhi maalum ya uanachama.
Kuhusu mpango wa kuunda chombo kitakachosimamia masuala ya kimataifa, Bendera alisema serikali pia haina mpango huo kwa kuwa haioni kama suala la ushiriki huo lina utata.
Alisema: “ZFA inatambuliwa na Caf na Cecafa wakati TFF inatambuliwa na CAF, CECAFA na FIFA, tatizo liko wapi”?
Bendera aliongeza kuwa mgogoro huo kati ya TFF na ZFA upo katika fedha hiyo hizo na si vinginevyo, hivyo hakuna umuhimu wa kuendelea kuwepo.
Alifafanua kuwa fedha hizo hutumika kwa shughuli za maendeleo ya michezo kwa manufaa ya pande zote mbili, akitaja maeneo yaliyoguswa kuwa ni utawala, mipango, timu za taifa, mashindano, ununuzi wa vifaa vya ofisi, dawa za wachezaji na semina.
Comments
Loading…