*Wenger asema amedhihirisha imani yake
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger anaamini kwamba imani yake kwa kinda Mjerumani, Serge Gnabry imelipa.
Wenger ameanza kumpanga Gnabry katika mechi za hivi karibuni, ambapo aliwapatia Washika Bunduki wa London bao la kuongoza dhidi ya Swansea Jumamosi iliyopita.
Gnabry ni kijana mwenye umri wa miaka 18, akiwa anashika rekodi ya kuwa mchezaji wa pili mdogo zaidi kufunga bao katika Ligi Kuu ya England (EPL) kwa klabu hiyo baada ya Cesc Fabregas.
Winga huyo alikuwa anacheza katika mechi ya pili tu ya EPL na alifumania nyavu katika nusu ya pili ya mechi, akimalizia vyema mpira uliohusisha mtandao wa Bacary Sagna, Olivier Giroud, Jack Wilshire na Aaron Ramsey.
Gnabry alianza kutumiwa kwa majaribio baada ya mchezaji wa kimataifa wa England, Theo Walcott kuumia, ambapo anafanyiwa upasuaji wa misuli ya tumbo, lakini si wengi waliotarajiwa kwamba angewika.
Wenger ameeleza kuridhishwa na ufanisi wake katika mechi iliyowafanya Arsenal wapae katika uongozi wa ligi kwa tofauti ya pointi mbili, sasa wakifuatiwa na Liverpool na Tottenham Hotspur, wawili hao wakifungana pointi baada ya mechi sita.
“Nahisi kwamba amedhihirisha imani yangu juu ya uwezo wake. Kijana huyu ana uwezo mkubwa, ana hadhi dimbani, anajituma na ameonesha hiyo kila wakati alipotumwa, kwa hiyo namchukulia kwa uchanya sana,” anasema Wenger.
Awali kabla ya Gnabry kuingia uwanjani katika mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya West Bromwich Albion, Wenger alisema kwamba anamwamini kwa kuwa ana kipaji, anajiamini lakini bahati mbaya si Mwingereza.
“Alikuwa na umri wa mwaka mmoja nilipojiunga na Arsenal, siwezi kuamini. Sasa nina wachezaji kwenye kikosi change ambao hawakuwa wamezaliwa nilipoingia Arsenal,” akasema Wenger aliyepata kuonesha nia yake ya kujenga kikosi imara kuzunguka wachezaji Waingereza.
Gnabry anafuata nyayo za mchezaji aliyeaminiwa, kupendwa na kuheshimiwa sana Arsenal – Fabregas aliyefunga bao lake la kwanza akiwa na umri wa miaka 17 na siku 113.
Comments
Loading…