Kocha wa Yanga, Mserbia Kostadin Papic
Kocha wa Yanga, Mserbia Kostadin Papic, amesema kuwa sare tatu mfululizo ambazo timu yake imezipata zimemchanganya na hivyo anahitaji kufanya mabadiliko katika kikosi chake kabla ya mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza itakayofanyika Novemba 7 dhidi ya Toto African kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Tangu ushindi wa 1-0 dhidi ya mahasimu wao Simba Oktoba 16, Yanga wameambulia pointi 3 katika sare tatu mfululizo, huku ‘Wekundu wa Msimbazi’ wakiwaengua kileleni baada ya kuzoa pointi tisa tangu kufungwa na ‘Wanajangwani’ baada ya kushinda mechi zote tatu. Simba sasa wana pointi 24 na Yanga wako katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 22 baada ya mechi 10.
Yanga ambao mapema mwakani wataiwakilisha nchi kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho ilitoa sare na JKT Ruvu, Azam FC na juzi ilitimiza sare ya tatu dhidi ya African Lyon.
Akizungumza na gazeti hili jana mchana baada ya kurejea jijini Dar es Salaam, Papic, alisema kuwa haamini na haelewi ni kwa nini timu yake imepata matokeo hayo wakati kila alichotakiwa kufanya na wachezaji wake kabla ya mechi hiyo ili ushindi upatikane, alikitekeleza.
“Sielewi, siamini ni kwa nini imekuwa hivi,” alisema kocha huyo ambaye aliipa Yanga ushindi wa 1-0 dhidi ya mahasimu wao Simba katika mechi waliyocheza Oktoba 16 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Papic alisema kuwa anatarajia kukutana na wachezaji wake ili kuzungumza nao kabla ya kuanza mazoezi ya kuikabili Toto African kwa sababu anaamini wanaweza kufahamu tatizo linalosababisha matokeo hayo.
“Nahitaji muda wa kujadili hili kwa pamoja, naamini hatua hiyo itatusaidia kupata ufumbuzi,” aliongeza kocha huyo ambaye bado yuko katika mazungumzo na viongozi wa klabu hiyo kabla ya kusaini mkataba mwingine baada ya ule wa awali wa mwaka mmoja kumalizika mapema mwezi huu.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga, jana jioni ulitarajiwa kukutana na benchi la ufundi la timu yao ili kupokea ripoti kuhusiana na matokeo hayo waliyoyaita ‘mabovu’ kwao.
Mbali na kujadili taarifa ya timu, pia kikao hicho kitajadili utetezi uliowasilishwa kwao kutoka kwa mchezaji Bakari Mbegu, ambaye hivi karibuni uongozi ulimuondoa kikosini jijini Tanga kutokana na tuhuma zinazomkabili za utovu wa nidhamu.
Afisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu, alithibitisha kuwepo kwa kikao hicho na kuongeza kuwa kitatathmini kiwango cha timu kilichoonyeshwa katika mechi zao 10 za mzunguko wa kwanza.
Katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga iko katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 22 wakati mahasimu wao, Simba, ndio wanaoongoza kutokana na kuwa na pointi 24.
CHANZO: NIPASHE
Comments
Loading…