BAADA ya Romelu Lukaku kuondoka Manchester United na kwenda Inter Milan wa Italia, Mashetani Wekundu wanataka kumpeleka Alexis sanchez huko huko, lakini suala la mshahara limekuwa pasua kichwa.
Mazungumzo yanafanyika baina ya klabu mbili hizo lakini kila wakizungukia hoja mbalimbali, wanarudi kwenye mshahara ambapo wanashindwa kuelewana, kwa sababu analipwa kiasi kikubwa mno ambacho Inter wanaona si sawa.
Klabu hiyo ya Serie A awali walikuwa wakiangalia iwapo kuna uwezekano wa kumsajili mchezaji huyo kwa mkopo kwanza, ambapo ingewezekana United wakaendelea kumlipa mshahara mzima au sehemu yake.
Uwezekano mwingine ni kwa Sanchez kukubali kuhamia Italia lakini apunguziwe mshahara, jambo analoelekea halitaki, kwani amekaa kimya tu Old Trafford, akiendelea kukinga kiasi cha £390,000 kwa wiki.
Inaelekea yupo radhi kubaki benchi ili mradi mshahara unaingia kwenye akaunti yake, ikizingatiwa kwamba ameshafikisha umri wa miaka 30. Inter wapo tayari kumlipa kwenye pauni 190,000.
Mchezaji huyu wa zamani wa Barcelona na Arsenal huenda akaungana na rafiki na mshambuliaji mwenzake wa zamani wa Man U, Lukaku – wote wawili wakiwa wameonekana ni mizigo na kocha Ole Gunnar Soskjaer ambaye anapendelea kutumia wachezaji chipukizi na wepesi katika Marcus Rashford, Anthony Martial na Jesse Lingard.
Inter wanaelezwa kutaka sana kumchukua raia huyu wa Chile kwa ajili ya kuimarisha kikosi na kukipa hadhi ya kushindania ubingwa dhidi ya Juventus ambao wamekuwa wakiitawala soka ya Italia na kubeba ubingwa mara kwa mara.
Sanchez aliondoka Arsenal akiwa moto lakini mara akaanza kupooza kupita kiasi hivyo kwamba katika kipindi cha msimu mmoja unusu amefunga mabao matano tu. Kadhalika amefunga idadi hiyo ya mabao kwa nchi yake kwenye michuano ya Copa America kiangazi cha mwaka huu kama alivyofanya kwenye msimu mzima wa 2018/19.
Ikiwa Inter watashindwa kuongeza kiwango cha fedha hadi Septemba 2 wakati dirisha la usajili la Ulaya likifungwa, itamaanisha kwamba Sanchez atabaki Old Trafford hadi, walau, Januari mwakani atakapotwaliwa.
Na ikiwa atabaki Man U, huku kocha Solskjaer akiwa habadili msimamo wake, itamaanisha kwamba Sanchez atacheza tu kwenye Kombe la Ligi – Carabao Cup, kwani hapewi tena nafasi kwenye kikosi cha kwanza. Jumanne iliyopita, alichezeshwa kwenye mechi ya kirafiki iliyofanyika bila washabiki. Alicheza sambamba na akina Matteo Darmian, Chris Smalling na Phil Jones.