in , ,

SALAH ANAWEZA KUMSHINDA MESSI, LAKINI NI ZIADA YA MAHITAJI NDANI YA BARCELONA

Mabao manne ya Mohamed Salah aliyofunga Jumamosi yamemuweka kwenye usukani katika vita ya kuwania kiatu cha dhahabu cha Ulaya. Mshambuliaji huyo aliisaidia Liverpool kuwafunga Watford 5-0 na kufikisha mabao 28 kwenye michezo 30 pekee ya Ligi Kuu ya England aliyocheza msimu huu.

Idadi hiyo ya mabao inamfanya kuwa na alama 56 kwenye chati ya vinara wa mabao kwenye ligi za barani Ulaya. Kila bao kwenye Ligi Kuu ya England na zile za Hispania, Ujerumani, Italia na Ufaransa huwa na thamani ya alama 2 kwenye mashindano ya kuwania kiatu cha dhahabu cha Ulaya.

Kwenye ligi za Urusi, Ureno, Ukraine na nyingine za daraja la kati kila bao hupewa alama 1.5 kwa mujibu wa kanuni za Chama cha soka cha Ulaya. Wafungaji wa kwenye ligi za daraja la chini kama zile za Sweeden, Serbia, Slovakia na nyingine huzawadiwa alama 1 pekee kwa kila bao.

Lionel Messi ndiye anayemfuatia Salah akiwa na alama 50 baada ya kufunga bao lake la 25 la msimu kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Athletic Bilbao nyumbani Nou Camp siku ya Jumapili. Mshambuliaji huyu wa Barcelona ndiye aliyenyakua tuzo hii ya kiatu cha dhahabu msimu uliopita kwa alama 74.

kutoka kushoto juul: Lionel Messi, Edin Dzeko, Wissam Ben Yedder, Robert Lewandowski, Cristiano Ronaldo, Gonzalo Higuaín, Sergio Agüero na Mohamed Salah.

Wapo washambuliaji watatu nyuma ya vinara Mohamed Salah na Lionel Messi. Hao ni Edinson Cavani wa PSG, Ciro Immobile wa Lazio na Harry Kane wa Tottenham Hotspur ambao kila mmoja ana alama 48 baada ya kufunga mabao 24 ya ligi mbaka sasa.

Hata hivyo ni Salah na Messi wanaoonekana kuwa kwenye mchuano mkali. Salah akiwa amebakiza michezo 7 pekee ya ligi, Lionel Messi bado ana michezo 9 ya La Liga iliyosalia. Ikiwa mshambuliaji huyo wa Barcelona ataweza kumpiku Salah atakuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kuinyakua tuzo hiyo mara tano.

Na iwapo Salah atafanikiwa kusalia kileleni mbaka mwishoni atakuwa mchezaji wa kwanza wa Ligi Kuu ya England kushinda tuzo hii tangu alipoitwaa Luis Suarez kwenye msimu wake wa mwisho akiwa na Liverpool. Nyota huyo wa Barcelona alifungana na Cristiano Ronaldo na hivyo walitwaa kwa pamoja tuzo ya msimu huo wa 2013/14.

Salah anaonekana kuwa tishio mno. Moto wake wa kufunga mabao na namna anavyoyafunga kwa mguu wake wa kushoto akiwahadaa walinzi kumemfanya afananishwe na Lionel Messi. Mafanikio haya hayamuachi hivi hivi. Yanamfanya kuhusishwa na Barcelona na Real Madrid kama ilivyo kwa nyota wengi wanaong’ara wakiwa nje ya timu hizo.

Inaarifiwa kuwa klabu hizo mbili za kifahari zaidi duniani ziko tayari kuvunja rekodi ya ada ya uhamisho kwa ajili yake. Salah anaweza kupata nafasi Real Madrid? Jibu la swali hili haliwezi kuwa ‘Hapana’. Gareth Bale ambaye hucheza nafasi kama ya Salah ya kushambulia kutokea upande wa kulia kwa sasa anaweza kumpisha kinara huyo wa mabao. Marco Asensio na Lucas Vazquez pia wanaweza kuketi kwenye benchi na kufaidi vyema burudani ya Salah.

Vipi kuhusu Barcelona? Salah anaweza kuwa na nafasi Nou Camp? Jibu ni ‘Hapana’. Nafasi anayoimudu vyema Salah hawezi kupata fursa ya kuicheza akiwa na uzi wa Blaugrana. Inashikiliwa na Mfalme ambaye katika umri wa Salah alikuwa ameshapokea ‘Balon d’ or’ mara nne. Labda aende akawe mbadala wa Mfalme huyu. Lakini mapesa mengi kiasi hicho hayawezi kutumika kwa ajili ya mchezaji wa akiba.

Inaweza kusemwa kuwa mfumo wa 4-4-2 ambao Barcelona wamekuwa wakiutumia chini ya mwalimu Ernesto Valverde unaweza kumpa nafasi Salah ya kucheza kama kiungo wa kulia nyuma ya Messi. Barcelona haiwezi kumsajili kwa fedha nyingi kwa ajili ya matumizi haya kwa kuwa kuna Ousmane Dembele ambaye paundi milioni 135 zilitumika kwa ajili yake miezi michache iliyopita. Yafaa Dembele apewe nafasi.

Salah anaweza kupata nafasi ndani ya Real Madrid ya sasa. Ameonesha makali yanayotosha kumfanya kuwemo kwenye 11 ya kwanza ya mabingwa hao wa Dunia kwa gharama ya Gareth Bale, Marco Asensio na wengine. Lakini hakuna nafasi yake ndani ya Barcelona. Anaweza kushinda kiatu cha dhahabu mbele ya Lionel Messi, lakini anabaki kuwa ziada ya mahitaji ndani ya Nou Camp.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

HOTUBA YA RAIS WA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU ALIPOZUNGUMZA NA WAHARIRI WA HABARI ZA MICHEZO JUMATATU MACHI 19,2018 KWENYE HOTEL YA SEASCAPE.

Tanzania Sports

Naiona Taswira ya Township Rollers kwenye kivuli cha Wolayta Dicha