in

Sakata la utovu wa nidhamu kwenye timu ya Taifa stars..

SAKATA la tuhuma ya utovu wa nidhamu kwenye timu ya Taifa ya soka ya Tanzania,Taifa Stars, dhidi ya wachezaji Haruna Moshi ‘Boban’ na Athumani Idd ‘Chuji'(ambao katika makala hii nitakuwa nikiwataja kwa majina ya Boban na Chuji) limekuwa ndiyo gumzo kubwa la soka yetu kwa siku hizi zaidi ya tathmini ya jumla ya ushiriki wetu wa mashindano ya kwanza ya fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani,CHAN, yaliyomalizika Jumapili ya Machi 8,2009 na DR Congo kuwa mabingwa wa kwanza wa michuano hiyo baada ya kuishinda Ghana 2-0 kwenye fainali.Hata kubahatika kwetu kutoa mchezaji mmoja,Mussa Hassan Mgosi,kwenye timu ya Afrika ya mashindano hayo imekuwa si habari, si lolote mbele ya habari ya utovu wa nidhamu wa Boban na Chuji.Hata hivyo,kwa kiasi kikubwa,katika kushughulikia suala hilo,wengi wetu tumekuwa hatuwatendei haki wachezaji hao.

Kwa upende mmoja,watu wanaozihusu klabu zao za Yanga kwa Chuji na Simba kwa Boban hawakuwatendea haki vijana hao hata kidogo.Hii ilitokana na kuwapa mapokezi ya kishujaa na kuwaongezea thamani kubwa waliporejea kwenye klabu zao wakitokea kwenye mashindano hayo na harufu kali ya kuchefua ya ukosefu wa nidhamu! Jinsi walivyopokewa na kupewa maneno matamu ya kuwatuliza,hakukuwa na tofauti na wanasiasa waliojeruhiwa kwa tuhuma nzito za ufisadi walivyopokelewa kishujaa kwenye maeneo yao kana kwamba walikotoka wamefanya jambo bora sana! Labda huu ndiyo utamaduni wetu mpya Watanzania kwamba anayeharibu kazi ya nchi anachukuliwa kuwa shujaa wa eneo la kwao!

Kumpokea Boban au Chuji kishujaa kwenye klabu baada ya tuhuma ya utovu wa nidhamu kwenye timu ya Taifa si kumtendea haki mchezaji huyo kwani hatajilazimisha kujutia kosa lake kwa siku zijazo.Aidha,hali hiyo itawafanya wachezaji wengine walio nao kwenye timu ya Taifa,ambao hawakupewa mapokezi ya thamani na klabu hizo “kwa sababu hawakutuhumiwa utovu wa nidhamu kwenye timu ya Taifa”,waone kuwa kumbe utovu wa nidhamu kwenye timu ya Taifa ni ‘dili’ la thamani kubwa kwenye klabu zao kwani linapandisha chati ya mchezaji! Hii si sahihi na si haki hata kidogo kwani haiwajengi bali inawabomoa vibaya kina Boban,Chuji na wachezaji wengine.

Kilichosikitisha ni kwamba watu wa klabu hizo wameeleza wazi kuwa wachezaji hao ni muhimu kwa klabu zao,wanawategemea sana kwa mafanikio yao na kamwe hawatawachukulia hatua yoyote kwa sababu hawajui walikosana nini na kocha wa timu ya Taifa.Kauli hiyo ni wazi imekuwa,kwa kiingereza, pre-emptive (ya kulitangulia jambo) kwa matazamio kwamba klabu hizo zingetakiwa ziwachukulie hatua wachezaji hao.Kwa kauli hizo za klabu kutowachukulia hatua wachezaji hao,klabu hizo zimetangulia kuieleza TFF isisumbuke kuwataka wawachukulie hatua wachezaji hao! Kutangulia huku ndiko kwa kiingereza kunaitwa to pre-empty.

Walichopaswa kufanya watu wa klabu hizo ni kuchunguza nini kilichotokea kuwahusu wachezaji hao ndani ya timu ya Taifa na endapo ingebainika walitenda utovu wa nidhamu,wangewachukulia hatua,angalau hata ya kuwaonya vikali.Angalau basi wangechukua hatua ndogo kama hiyo ingetosha kuwaweka wachezaji hao na wengine kwenye mstari mzuri kinidhamu. Ni dhahiri klabu zetu hizi hazipendi mtu wa nje yake amtuhumu mchezaji wao kwa utovu wa nidhamu kama ambavyo TFF nayo isivyopenda mchezaji wa timu ya Taifa aadhibiwe na klabu yake kwa utovu wa nidhamu! Kwa mfano,wakati Chuji alipokabili tuhuma ya kunyoosha kidole kwa matusi kwenye mashindano ya Tusker kule Mwanza mwaka juzi,iliamuliwa klabu yake ya Yanga impe onyo kwa kosa hilo bila mchezaji huyo kuchukuliwa hatua yoyote zaidi ya hiyo! Yanga ilikubali na iliahidi kutekeleza.

Kwa mshangao,Yanga hiyo hiyo ilikuja juu pale mchezaji huyo alipoadhibiwa kwa kosa hilo na kusema wazi kuwa mchezaji huyo hakufanya kosa lolote! Katika mazingira hayo,Yanga ingemuonyaje mchezaji wake iliyoamini hakufanya kosa lolote? Wakati Simba wanamfungia Chuji huyo huyo kwa kutoripoti mazoezini alipokwisha amua kuichezea Yanga,TFF iliifuta adhabu hiyo ya Simba kwa mchezaji “wake” (wa Simba).Huu ndiyo mtindo ambao sasa unaonekana kukomaa.Klabu inapoona kuna utovu wa nidhamu kwa mchezaji wake anayechezea pia timu ya Taifa,TFF inasema hakuna utovu wa nidhamu! TFF inapoona kuna utovu wa nidhamu wa mchezaji wa timu ya Taifa,klabu yake anayochezea inasema hakuna utovu wa nidhamu! Tutaendeleaje namna hii kila mmoja akivuta kamba upande tofauti?

Kwa upande mwingine, Boban na Chuji hawakutendewa haki kwani wengi wetu tulivamia kuwalaani sana baada tu ya kocha Marcio Maximo kueleza kuwa wachezaji hao wamefanya vitendo vya utovu wa nidhamu,vikiwemo kuzembea mazoezi tangu hapa nyumbani na Boban kucheza chini ya kiwango alipopangwa kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Senegal.Ambacho tungefanya kabla ya kuwalaani wachezaji hao ni kufuatilia ukweli wa tuhuma dhidi yao ikizingatiwa kuwa kocha Maximo ni binadamu mwenye hisia za upendo na chuki kama binadamu mwingine.Tusiwe tunamuamini sana kama vile ana hadhi ya juu ya ubinadamu.Chukua mfano huu,amesema Boban na Chuji walizembea mazoezi wakiwa hapa kabla ya kwenda Ivory Coast.Mbona Chuji alikuwa anaumwa wakati huo hata kukosa pambano la kirafiki dhidi ya Zimbabwe? Mbona Boban, “mzembea mazoezi”, alipiga soka ya hali ya juu dhidi ya Wazimbabwe mpaka Wazimbabwe hao kumpa hadhi ya mchezaji bora wa mechi hiyo (Man of the Match)?

Wakiwa huko Ivory Coast,Chuji alitangazwa na kocha huyo kuwa mgonjwa muda wote huku akikataa tu kumpanga mchezaji huyo aliyekuwa mzima kabisa! Kwa nini amelidanganya Taifa wakati halazimishwi na mtu yeyote kumpanga au kutompanga mchezaji yeyote kwa sababu zake zozote za kitaalam? Kuharibu kwa Boban kwenye mechi aliyopangwa kumeelezwa kuwa moja ya sababu za yeye kutoswa na kocha huyo.Ni mchezaji gani duniani asiyewahi kukataliwa na mpira angalau siku moja? Kwa nini isingetafutwa sababu ya yeye kuharibu siku hiyo na kwa nini hakupewa nafasi nyingine labda angekuwa vizuri tena kama ilivyo kawaida yake?

Tuwe makini sana na kauli za Maximo kwa wachezaji.Hivyo,tusiwe watu wa kuzidaka upesi upesi na kuzisambaza kwa maneno makali ya laana kwa wachezaji kabla hatujasikiliza na upande mwingine.Kama hakuwavisha jezi wachezaji hao siku ya mechi yetu na Zambia na kama aliwashusha kweli kwenye basi alipotaka kuongea na wachezaji wake kuhusu matokeo ya mechi yetu na Zambia,tulitegeme kweli wachezaji hao waendelee kuwa naye vizuri wakati walishaona wametengwa wazi wazi? Hata kujiondokea kivyao kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA),Dar es Salaam yalikuwa ni matokeo ya uhasama huo alioujenga kocha kwa wachezaji hao ingawa kitendo walichofanya uwanjani hapo si cha kuungwa mkono.

Ninachotaka kusema ni kwamba siku zote tuwe watu wa kuchunguza,kutafakari na kupima mambo mazito bila kuchagua kwamba hili limetoka kwa Maximo tuliunge mkono bila mashaka na hili limetoka kwa Mshindo Msolla linapaswa lifuatiliwe kabla ya kulitolea hukumu.Kwa mfano, akiwa anaifundisha timu ya Taifa,kocha Mshindo Msolla alipomuondoa kambini Ulimboka Mwakingwe kwa kuchelewa sana kuripoti,wengi miongoni mwetu tulimlaumu kocha huyo kwa sababu ni Mshindo Msolla! Marcio Maximo alipomfukuza jumla kwenye timu hiyo kipa Juma Kaseja,bila sababu iliyo dhahiri mpaka leo, wengi tunaiunga mkono hatua hiyo huku tukihangaika kujaza sababu za yeye kufanya hivyo ikiwemo ya eti Kaseja alishangilia tulipobugizwa bao 4-0 kule Senegal! Nani kasema hiyo,Maximo au Kaseja? Kasemea wapi? Mbona ya Boban na Chuji kayaeleza haraka(ingawa hayana mashiko) lakini la Kaseja halisemi?

Kama tulivyoipima kesi ya kuadhibiwa kwa Hamis Yussuf wa Yanga na kocha wake Micho kwa kulimwa kadi nyekundu kwenye mechi ya timu yake dhidi ya Esperance ya Tunisia kwenye kombe la Shirikisho mwaka juzi nchini Tunisia na kumlaumu kocha hiyo kwa hatua hiyo,kama tulivyoipima kesi ya kuadhibiwa na klabu yao kwa wachezaji Shadrack Nsajigwa na Ivo Mapunda baada ya mechi ya timu yao ya Yanga dhidi ya Simba ya kule Morogoro mwaka juzi na kuiona klabu hiyo haikuwatendea haki wachezaji hao na kama tulivyoipima kesi ya kufungiwa kwa Chuji na Simba wakati alishajitoa kwenda Yanga na kuiona Simba kutomtendea haki mchezaji huyo ndivyo ambavyo tungeipima kesi ya Maximo na wachezaji Boban na Chuji kabla ya kuwahukumu wachezaji hao.

Ni vigumu kuamini kwamba mchezaji aliyejituma siku zote kwenye timu ya Taifa na kufanya juhudi kubwa za kuiingiza timu hiyo kwenye fainali za CHAN akazembea mazoezi wakati ameshafika kwenye fainali hizo za kujitangaza dunia nzima! Kuna uwezekanao Maximo ana ugomvi binafsi na wachezaji hao na amewatafutia sababu za kuwaondoa jumla kwenye timu yake kama kulivyo na uwezekano wa wachezaji hao kuwa watovu wa nidhamu waliopitiliza.Ukweli ni upi,itategemea uchunguzi na siyo kuibuka tu na kuanza kuwashambulia wachezaji hao.Tuwe makini na hoja zetu za kuhukumu watu haraka haraka.Kwa upande mwingine,hakuna busara kumpa hadhi kubwa mchezaji mwenye tuhuma ya utovu wa nidhamu kana kwamba utovu wa nidhamu ni sifa nzuri kwa mchezaji.Katika mazingira yote hayo mawili,kuwalaumu kabla ya kuthibitisha tuhuma na kuwapa mapokezi ya kifalme baada ya kutuhumiwa,Boban na Chuji hawatendewi haki.

MWISHO

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Champions League – United held by effervescent Porto

Champions League – Ivanovic hands advantage to Chelsea