Viwango vilivyooneshwa na Jamie Vardy na Harry Kane kwenye michezo ya kirafiki ya timu ya taifa ya England mwishoni mwa mwezi uliopita vimeleta maswali mengi kuhusiana na nafasi ya Wayne Rooney kwenye kikosi cha Roy Hodgson.
Wapo wanaosema kuwa Rooney hastahili kuwemo kwenye XI ya kwanza ya England kwa ajili ya Euro.Wengine wanadai kuwa hastahili kuitwa kikosini kabisa. Nalazimika kujiuliza. Rooney hahitajiki kwenye kikosi cha England?!
Kwenye mfumo wa 4-3-1-2 wa mwalimu Roy Hodgson kwa kawaida nafasi ya Rooney ni kuwa mmoja kati ya washambuliaji wawili. Vardy na Kane wameonesha kuwa ni wao wanaostahili kucheza kwenye nafasi hizo mbili.
Achana na idadi ya mabao 41 ambayo washambuliaji hao wawili kwa pamoja wameshatumbukiza wavuni kwenye Ligi Kuu ya England msimu huu.
Viwango walivyoonesha kwenye michezo ya England mwishoni mwa mwezi uliopita wakifunga mabao matatu kwenye michezo miwili vinamfanya kila mmoja wao astahili nafasi ya uhakika kwenye kikosi cha England.
Wakati huo huo Daniel Sturridge na Danny Welbeck wapo nje wakisubiri nafasi. Hivyo nafasi ya Rooney wa kiwango chake cha sasa ni kuungana na wenzie hao kwenye benchi endapo wote watatu wataitwa kwa ajili ya Euro.
Ikiwa tunasema kuwa nahodha huyo hawezi kumuondosha Kane wala Vardy kwenye nafasi ya washambuliaji wawili, je hawezi kupata nafasi kwenye sehemu ya kiungo mshambuliaji?
Hapa anaingia kwenye mpambano dhidi ya Adam Lallana na Ross Barkley. Hapa napo napata shida kukubali kuwa Rooney anastahili kupewa kipaumbele dhidi ya yeyote kati ya wawili hao.
Lallana ingawa hana msimu mzuri kiasi hicho kwenye EPL lakini kiwango chake kwenye michezo migumu ya karibuni aliyocheza dhidi ya Southampton, Manchester United na Manchester City kinatosha kumpa nafasi kwenye kikosi cha Hodgson.
Ana uwezo wa kutosha wa kufunga na kutengeneza nafasi za mabao bila kusahau mchango wake kwenye ulinzi pale timu inapopoteza mpira. Amethibitisha ubora wake huo kwenye mchezo dhidi ya Uholanzi wiki iliyopita.
Ross Barkley pia ni mmoja kati ya viungo mahiri washambuliaji. Uwezo wake wa kukokota mpira, kupiga pasi za kupenyeza na mashuti ya mbali unamfanya astahili nafasi kwenye kikosi cha England.
Hivyo kwa upande wangu Rooney wa kiwago chake cha sasa hana nafasi kwenye XI ya kwanza ya England. Wapo wanaaonesha viwango vizuri zaidi yake kwenye kila nafasi ambayo angeweza kucheza.
Lakini hilo halina maana kuwa naungana na wanaosema kuwa hastahili kabisa kuitwa kwenye kikosi cha England. England inamhitaji nahodha huyo kwa ajili ya Euro. Si kwa sababu ya jina lake. Wala si kwa sababu ya mabao 51 aliyoifungia England.
Kinachomfanya awe na umuhimu mkubwa kwenye kikosi cha England ni uwezo wake wa kuwaongoza na kuwahamasisha wachezaji wenzie ndani na nje ya uwanja. Tofauti na uhasimu wa klabu huwa havina nafasi kwake.
Nyota wa Manchester City Raheem Sterling aliwahi kukiri wakati akiwa Liverpool namna Rooney alivyokuwa akimpa moyo na kumhamasisha kufanya vizuri walipokutana kwenye timu ya taifa.
Sterling alisema kuwa nahodha huyo alimsifu mno kwa kasi yake akimfananisha na nyota wa zamani wa Arsenal na Barcelona Marc Overmars. Hilo kwa vyovote vile lilimfanya Sterling ajitume zaidi.
Hivyo ndivyo alivyo Rooney. Ni kiongozi na mhamasishaji hasa kwa nyota wanaochipukia. Inaweza kuwa kweli hana nafasi kwenye XI ya kwanza ya England, lakini vyumba vya kubadilishia nguo vya England vinamhitaji nahodha huyo.