Wengi wamepita na wengi waliweka rekodi nyingi ambazo ziliwapa heshima kubwa katika uso huu wa dunia ya mpira wa miguu.
Hapa ndipo paliwahi kuitwa na bado panaitwa kuwa ni sehemu ya nyumba ya vipaji vyote bora vya dunia hii tuliyopo sasa.
Huwezi kuwa mbali na ukweli kama utasema kuwa RealMadrid ni Hija ya mpira, kila mcheza mpira wa miguu hutamani nyayo zake za miguu kukanyaga Santiago Bernabeau kwenda kufanya ibada ya mpira.
Uwanja wenye historia kubwa katika soka la dunia. Ndiyo uwanja ambao unaongoza kupokea makombe ya klabu bingwa barani ulaya.
Kombe lenye hadhi na msisimko mkubwa sana duniani, lakini kwao wao kombe hili wamelizoea. Hata kuchukua mara tatu mfululizo lilikuwa jambo la kawaida kwao kwa sababu wanaamini kuwa kombe hilo lilitengenezwa kwa ajili yao.
Wachezaji wote hunyweshwa damu hii, haikuwa kazi ngumu kwa Zinedine Zidane kuwaongoza wachezaji wake kuchukua kombe hili mara tatu mfululizo kwa sababu tangu akiwa mchezaji wa RealMadrid alikuwa anajua utamaduni wa RealMadrid ni upi.
Ngozi yake iliwahi kuvikwa jezi nyeupe na miguu yake iliwahi kukanyaga nyasi za Santiago Bernabeau.
Nyasi hizi zilimpokea kwa heshima wakati anakuja RealMadrid na zikamuaga kwa heshima wakati anastaafu kucheza mpira.
Tukio ambalo ni nadra kuliona katika klabu ya RealMadrid. Ni ngumu kumuona mchezaji wa RealMadrid kustaafu na jezi ya RealMadrid tena kwa heshima kubwa.
Raul Gonzalenz aliishi miaka 18 tena kwa heshima kubwa akiwa kama mchezaji aliyeitumikia kwa kucheza mechi nyingi pale RealMadrid lakini hakupewa heshima hii.
Inawezekana Iker Casillas ndiye golikipa bora wa muda wote wa RealMadrid na alianza maisha yake pale RealMadrid akiwa na miaka 6 lakini mwisho wa siku alikosa heshima ya kustaafu akiwa na jezi ya timu ambayo aliitumikia kwa muda mrefu tena kwa heshima kubwa.
Roho ilimuuma sana, alikasirika sana na ikiwezekana alitukana sana lakini vyote hivi havikufuta ukweli kuwa muda haukumruhusu kustaafu akiwa na jezi ya RealMadrid.
Wakati mwingine muda huwa ni katili sana, uliwahi kumkatili Iker Casillas, ukamnyima raha Raul Gonzalenz leo hii kuna kila dalili unaenda kumkatili Criatiano Ronaldo.
Mfungaji bora wa muda wote wa klabu ya RealMadrid akiwa na magoli 450 na ballon d’or tano katika mikono yake huku ballon d’or nne akizibeba akiwa na jezi ya RealMadrid.
Jezi ambayo Ferenc Puskas aliwahi kuivaa kwa mafanikio makubwa. Hata aliyewahi kuwa mfungaji bora wa muda wote wa RealMadrid kabla ya Cristiano Ronaldo kuivunja rekodi yake, yani Alfredo De Stefano aliwahi kuvaa jezi hii lakini kwa huzuni kubwa hawakufanikiwa kustaafu na jezi hii.
Hiki ndicho kinachoenda kutokea kwa Cristiano Ronaldo. Hakuna kiongozi wa RealMadrid anayeumia kila akisikia habari za Cristiano Ronaldo kuondoka RealMadrid.
Miaka 33 ni miaka ambayo inaonesha Cristiano Ronaldo ameanza kuondoka katika miguu yake taratibu. Hatokuwa na makali tena kama ambayo aliwahi kuwa nayo.
Akili yake inawaza mkataba mnono, mkataba ambao utakuwa kama mafao yake ya uzeeni, kitu hiki ni kigumu kwa RealMadrid iliyojaa wachaga wengi.
Hawana habari naye, na hawataki kabisa kusikia habari za kumuongezea mkataba wenye mshahara mkubwa. Mengi kashayafanya na vikombe vingi kashavileta katika timu hii, hawafikirii tena kama wataweza kupata vikombe vingine kwenye miguu ya Cristiano Ronaldo.
Hapa ndipo njia panda ya Cristiano Ronaldo kupewa heshima ya Zinedine Zidane inapoanzia.
Moyo wake unatamani kustaafu Santiago Bernabeau lakini matamanio ya viongozi wa RealMadrid ni kuleta wachezaji wapya vijana ambao watatumikia nafasi yake.
Hawataki kuingia hasara ya kipesa, na wanaona huu ndiyo wakati mzuri wa kutengeneza pesa kupitia kumuuza Cristiano Ronaldo. Hakutakuwepo na wakati mwingine mzuri kama huu.
Hakuna anayefikiria kuwa huyu ndiye mfungaji bora wa wakati wote wa RealMadrid hivo anatakiwa kupewa heshima kubwa.
Pesa inaheshima kubwa kwa sasa kuliko miguu iliyozeeka ya Cristiano Ronaldo. Miguu iliyoishiwa kasi, miguu ambayo ni ngumu kufunga magoli mengi kama ilivyokuwa kipindi cha ujana wa miguu yake.