Takwimu za kila aina zilizungumziwa baada ya Atletico Madrid kuchapwa mabao 5-3 na Real Madrid katika uwanja wa San Siro, jijini Milan, Italia, jana Jumamosi. Takwimu ya kwanza ilimzungumzia mshambuliaji wa Kireno, Cristiano Ronaldo ambaye sasa ameshainua vikombe vya klabu bingwa za Ulaya (UEFA) mara tatu akiwa mchezaji. Mwanzo ilikuwa Manchester United 2008 na mara mbili sasa akiwa mshambuliaji wa namba yake maarufu ya saba, Real Madrid (2014 na 2016). Ronaldo ndiyo aliyefunga kazi baada ya kuweka penalti ya mwisho kimiani katika mechi hii kali ya wababe wawili wa Spain. Ushindi wa penalti ulitokona na wafalme hawa kwenda sare – bao moja kwa moja -hata baada ya kipindi cha ziada cha dakika 30- kilichowekwa baada ya mchezo wa kukata na shoka wa saa moja na nusu.
Takwimu ya pili ilizungumzia umahiri wa kocha Zinedine Zidane aliyeingoza timu ya Ufaransa kutwaa kombe la dunia la 1998, na ambaye anahesabika kama mmoja wa wachezaji bora kuzidi wote ndani ya soka duniani. “Zizou” ameweka historia kwa kujiunga na mameneja washindi waliozifikisha timu zao kileleni baada ya pia kuchezea timu hizo miaka ya nyuma. Hili si jambo linalotokea sana, siku za leo ambapo makocha maarufu kama mzee mstaafu Alex Fergusson (Man United) Arsene Wenger na Jose Mourinho hawakuwa wachezaji wa kutisha bali wa kawaida tu.
Baada ya kushindwa kuonesha nguvu zao kama wachezaji walibobea zaidi katika ukocha.
Makocha waliowahi kushinda kombe la klabu za Ulaya kama wachezaji vile vile ni Pep Guardiola (Barcelona) , Carlo Ancelotti (AC Milan) na Luis Miguel Ramis (Real Madrid). Zidane alikuwa kati wachezaji nyota waliovuma miaka kumi na tano iliyopita na kuitwa “Galacticos” – mastaa au wachezaji nyota kuzidi wote- baada ya kununuliwa kwa paundi 46 milioni mwaka 2001. Wengine ni David Beckham, Luis Figo, Kaka, Claude Makelele, nk.
Mchezo wa San Siro ulianza na bao lililotokana na pasi ya Gareth Bale, na kufungwa na Sergio Ramos dakika ya 15 ya dimba. Hata hivyo uongozi wa Real Madrid haukudumu. Dakika ya 79, Yannick Carasco wa Atletico- alisawazisha na kusababisha mechi kuendelea nusu saa zaidi. Kutokana na bao lolote jingine kutofungwa , mchezo uliishia kwa penalti. Kila mchezaji alifunga isipokuwa Juanfran wa Atletico Madrid. Mwishoni, Cristiano Ronaldo hakujivunga na kuifikisha timu yake ubingwani kwa penalti ya mwisho. Angekosa tungekuwa tunazungumzia mengine leo.
Real Madrid na Atletico ni miongoni mwa timu tatu kuu za Spain ambazo zimewahi kushinda vikombe kadhaa ikiwemo La Liga nchini Spain. Atletico Madrid iliyowahi kushinda La Liga mara kumi – haina wachezaji maarufu tunaowajua sana- kama ilivyo Real Madrid, lakini miongoni mwa wanaojulikana ni mshambuliaji Fernando Torres –aliyeshaichezea Liverpool na Chelsea- na Thomas Partey, mzawa wa Ghana. Kocha wao ni Diego Simone aliyekuwa zamani nyota ya Argentina – na kushiriki michuano ya kombe la dunia la 1994 , 1998 na 2002. Simone anasifika kwa kipaji chake cha kuongoza, kuona umbali na ukaribu wa mechi na ufundi kimpira.
Atletico Madrid ilianzishwa rasmi mwaka 1903 ambapo wapinzani wake Real Madrid mwaka 1902. Klabu hizi mbili zina majina ya utani, la Real Madrid ni “Galacticos” ( wachezaji matajiri na nyota) na Atletico huitwa “Los Colchoneros” yaani watengenezaji magodoro. Utani wa godoro unatokana na jezi zao zenye mistari mistari inayofanana na magodoro.
Jezi nyeupe ya Real Madrid ilivumbuliwa mwaka 1955 na haijabadilishwa tena.