Real Madrid wameendelea kuthibitisha umwamba wao kwa kuwafunga Malaga 1-0 na kufikisha mechi 17 za La Liga bila kufungwa.
Katika mechi za mashindano yote, wamefikisha 30 pasipo kupoteza hata moja na wanaongoza ligi kwa kujikusanyia pointi 70 wakifuatiwa an Atletico Madrid wenye pointi 67. Barcelona walikuwa na pointi 63 na mchezo mmoja mkononi.
Cristiano Ronaldo ndiye alipeleka majonzi kwa Malaga waliokuwa wakifundishwa na Manuel Pellegrini hadi msimu uliopita. Madrid sasa wamejihakikishia kwamba wapo imara katika kuwania ubingwa wa Hispania chini ya Kocha Carlo Ancelotti.
Hata hivyo, Real walitarajiwa kupata ushindi mnene zaidi, lakini hawakuwa katika kiwango cha juu Jumamosi hii, huku Malaga wakijitahidi kucheza vizuri kujinusuru na kushuka daraja, kwani wanashika nafasi ya 13 wakiwa na pointi 29 sawa na timu tatu za chini yake, ya nne ikiwa na pointi 28, nyingine mbili 26 na iliyo mkiani 18 ambayo ni Real Betis.
Mara ya mwisho kwa Real Madrid kufungwa ilikuwa Oktoba mwaka jana, ambapo walipigwa na Barca 2-1. Barca wanacheza na Osasuna Jumapili hii wakati Real watawakaribisha Schalke ya Ujerumani Jumanne kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Comments
Loading…