Mambo yameanza vibaya kwa miamba wa Ulaya, Real Madrid, baada ya kikosi kilichojaa nyota wengi kuchapwa na mahasimu wa jijini kwao, Atletico Madrid na kukosa Supercopa dimbani Vincente Calderon.
Hiyo ilikuwa katika mechi ya pili iliyowakutanisha baada ya kwenda sare ya 1-1 kwenye mechi ya awali katika Uwanja wa Santiago Bernabeu. Alikuwa ni Mario Mandzukic aliyewalaza mapema washabiki wa Real kwa bao lake la kwanza kwa timu yake mpya.
Raia huyo wa Croatia aliachia fataki la kima cha paka dakika mbili tu baada ya mechi kuanza na jitihada za nyota wa Real kukomboa ziligonga mwamba, na kuthibitisha kauli ya awali ya kocha Carlo Ancelotti kwamba ni vigumu kupata ushindi kwenye dimba hilo la ugenini ikiwa hawangecheza kwa nguvu na kasi.
Mandzukich alifunga baada ya kipa Miguel Moya aliyechukua nafasi ya Thibaut Courtois aliyerudi Chelsea kiangazi hiki kumtiririshia mpiraAntoine Griezmann aliyesajiliwa kutoka Real Sociedad naye akamkuta Mandzukic aliyekimbia na kumtungua kipa Iker Casillas.
Kocha wa Atletico, Diego Simeone alitolewa nje baada ya kumlalamikia mwamuzi wa akiba juu ya beki wake wa kulia, Juanfran kutoruhusiwa kurudi uwanjani mapema baada ya kutobiwa. Katika kulalamika huko, alimpiga kikofi mwamuzi huyo.
Mchezaji mpya wa Real, James Rodriguez alipata nafasi nzuri zaidi za kufunga lakini mashuti yake yalipita juu ya mtambaa wa panya.
Mcolombia huyo aliyefunga kwenye mechi ya awali alishindwa kucheka na nyavu baada ya kipa Moya kuokoa mchomo mwingine kisha akapiga nje mpira mwingine kwa kichwa.
Rodriguez, Cristiano Ronaldo, Gareth Bale, Toni Kroos na Karim Benzema waliogharimu mamilioni ya pauni walishindwa kabisa kuonesha cheche zao, huku Ronaldo akiwa kana kwamba hayupo uwanjani.
Atletico walicheza na Real kama kufungua pazia la La Liga, na kombe hilo ni mithili ya Ngao ya Jamii hapa England na Tanzania pia. Atletico ni mabingwa watetezi wakati Real ni mabingwa wa Kombe la Mfalme (Copa Del Rey).
Comments
Loading…