*Wawachepua Atletico 4-1
Real Madrid wameweka historia baada ya kutimiza ndoto yao ya kutwaa ubingwa wa Ulaya kwa mara ya 10, hatua ambayo ni maarufu zaidi kwa jina la La Decima.
Walichukua ubingwa huo katika mtanange mkali uliopigwa jijini Lisbon, Ureno, wakikabiliana na wapinzani wao wa Jiji la Madrid, Atletico Madrid.
Haikuwa kazi rahisi kutwaa kombe hilo, kwa sababu Atletico walikuwa wakali tangu mwanzo na katika dakika ya 36 walipata bao la kwanza kupitia kwa Diego Godin na kuweka hai ndoto za Kocha Diego Simeone kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.
Hata hivyo, uzoefu labda na bahati vilikuwa upande wa vijana wa Carlo Ancelotti ambao walicheza kufa na kupona, wakijua ubaya wa Atletico walionyakua ubingwa wa La Liga wikiendi iliyopita.
Wakati Atletico wakijiandaa kusherehekea ‘ushindi’, Sergio Ramos alikatiza ndoto zao kwa kufunga bao dakika za lala salama na kulazimisha mechi kwenda muda wa nyongeza. Ni wakati huo Real walitumia uzoefu wao na kuwamaliza Atletico.
Katika muda mfupi. Katika dakika 10 walifunga mabao matatu na kupeleka kilio kwa wapinzani wao. Alikuwa Gareth Bale aliyefunga dakika ya 110, dakika nane baadaye Marcelo akafunga kabla ya mchezaji bora wa dunia, Cristiano Ronaldo kupigilia msumari kwenye jeneza la Atletico kwa bao la penati dakika ya mwisho ya mchezo.
Angel Di Maria ndiye alikuwa nyota wa mchezo, kutokana na pasi zake za uhakika ambapo kwa ujumla alitoa pasi 71, kupiga majalo 23 na kugusa mpira mara 126 na kutopoteza hovyo umiliki wa mpira.
Kocha Carlo Ancelotti atakuwa ameridhika na msimu huu ulivyomalizika, ambapo ametwaa mataji mawili, moja likiwa ni hili la Ulaya na jingine ni Kombe la Mfalme ambapo aliwafunga Barcelona.
Bale ambaye ni mchezaji aliyenunuliwa kwa fedha nyingi zaidi duniani, alisema kupata ubingwa huo kumetimiza ndoto yake, kumempa furaha na kwamba ni kumbukumbu ambayo haitakaa ifutike akilini mwake.
Comments
Loading…