RATIBA ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imezipagaisha timu za Simba na Yanga zitakazoshiriki michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Februari mwakani.
Klabu ya Simba imepanga kumenyana na timu ya Kiyovu ya Rwanda wakati Yanga itamenyana na Klabu Kongwe Afrika ya Zamalek kutoka Misri katika michezo itakayofanyika katikati ya Februari mwakani.
Timu za Yanga na Simba zimeonekana kuhaha zaidi wiki hii baada ya ratiba kutangazwa ili hali kwa miezi kadhaa zilijua kwamba michuano ya aina hiyo itakuwapo, lakini hazikuwa na mipango ya kuziimarisha timu zao.
Yanga ndiyo iliyozidiwa zaidi kwani, mara baada ya ratiba kutangazwa, kocha mkuu wa timu hiyo Kostadin Papic alitangaza wazi kwamba mechi hiyo ni pasua kichwa kwake.
Papic alisema atatangaza programu akisisitiza kwamba kama itafuatwa itasaidia kuijenga timu hiyo kwa kuikabili Zamalek ambayo kwa miaka mingi imekuwa tishio kwa timu za Tanzania hususan Yanga.
Katika kile kinachoonekana kwamba ni kuitikia mipango ya kocha huyo, Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Lyoyd Nchunga wiki hii alitangaza kwamba timu yake inatarajia kwenda Afrika Kusini kuweka kambi huku akisisitiza kwamba pia itacheza mechi za majaribio.
Miongoni mwa timu alizozitaja kutaka kucheza nazo kabla ya kuwavaa mafarao wa Misri ni Sofapaka ya Kenya na ile ya Mamlaka ya mapato Uganda (URA) ambazo pia zina upinzani mkali nchini mwao.
Wakati Yanga ikiwa na mipango hiyo, naye Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage alitangaza kwamba watazitumia mechi za Ligi Kuu mzunguko wa pili zitakazoanza Januari kujinoa kwa ajili ya kupambana na Kiyovu.
Lakini pia baada ya siku mbili kupita, kiongozi huyo alisema timu yake sasa inatarajia kwenda nchini Malawi kwa ajili ya kambi ambako itapambana na klabu kadhaa za huko.
Rage alisema timu ya Kiyovu alishaiona na kwamba ni ngumu sana kiasi kwamba kwa sasa inamnyima usingizi.
Hatua zote hizo zinachukuliwa na viongozi wa klabu kubwa hizo kama dharura wakati ukweli ni kwamba walijua kuwapo kwa michuano hiyo tangu waliposhika nafasi ya kwanza na ya pili mwaka jana.
Baadhi ya wapenzi wa soka nchini walikosoa maandalizi ya papara wanayofanya viongozi wa klabu hizo wakisema walichotakiwa ni kuwaweka wachezaji katika mazingira ya kucheza michuano ya kimataifa tangu mwanzo.
“Maandalizi ya zimamoto ndiyo yanayoziua timu za Tanzania”, alisema mwanamichezo maarufu na shabiki wa Man U, aliyejitambusha kwa jina la Brighton Mwakasumbula.
Alisema kwa kawaida viongozi wa timu hizo walitakiwa kuwa na programu mbili ambazo ni ile ya ligi kuu na nyingine ya michuano ya kimataifa tangu walipopata tiketi ya kushiriki michuano mikubwa Afrika.
Lakini baadhi ya mashabiki wa timu hiyo walisema pamoja na kuchelewa kwa maandalizi, wana imani timu zao zitafanya vizuri.
Comments
Loading…