in , ,

Ramani ya Vincent Kompany kwa Bayern Munich

RATIBA ya Ligi Kuu ya Ujerumani imefika mechi 10 kati ya 36. Ligi ya Ujerumani inahusisha timu 18 hivyo zinatakiwa kucheza michezo 36. Hadi kufika sasa timecheza mechi 10 bila kuwepo na kiporo cha aina yoyote, hivyo kuanza timu kinara hadi iliyopo mkiani zote zimecheza mechi sawa. Pamoja na mambo mengine, Ligi ya Ujerumani imebaki kuwa mashuhuri duniani na yenye sifa ya kutoa makocha wa kiwango cha juu. katika Ligi hiyo msimu huu imempokea kocha mpya Vincent Kompany raia wa Ubelgiji. 

Kocha huyo alichukua nafasi ya Thomas Tuchel ambaye alisitishiwa kandarasi yake kwa makubaliano na pande zote mbili kwamba msimu ulipomalizika kila mmoja atachukua mwelekeo wake. Hivyo basi Vincent Kompany anakuwa kocha wa kwanza mwenye asili ya Afrika kutoka kwa wazazi waliozaliwa Jmahuri ya Kidemokrasia ya Kongo lakini yeye ni mzaliwa wa Ubelgiji akianza soka viunga vya nchi hiyo kabla ya kuvuka mipaka hadi Bundesliga kisha akaenda kukipiga katika klabu ya Manchester City hadi alipohitimisha muda wake. 

Dhamira ya Vincent Kompany ilikuwa kuwa kocha, hivyo haikushangaza alipoanzia ukocha nyumbani kwao Ubelgiji kabla ya kuibukia Burnley ya England. Umahiri wake ulichangia kuipeleka Burnley hadi EPL. Mikikimikiki ya EPL haikusaidia Burnley kudumu hivyo ikashuka tena daraja hadi Championship. Vincent Kompany akanyakuliwa na vigogo wa kijerumani, Bayern Munich. Mjadala mkubwa hapa London na kwingine Ulaya ulikuwa kama ataweza kuipaisha timu hiyo. 

Swali kubwa lilikuwa ni hili, vipi nahodha huyo wa zamani wa Manchester City na Ubelgiji atamudu kuipa makali Bayern Munich? Swali la pili lilitokana na uzoefu mdogo kuliko inavyodhaniwa; kwamba Kompany ambaye alishindwa kuipaisha Burnley katika Ligi Kuu England atamudu vipi presha za Bundesliga? Hata hivyo msimu tangu umeanza na sasa kuna mechi 10 baadhi ya majibu yametolewa. Vilevile katika mashindano ya UCL je kocha huyo atawaletea nini Bayern Munich

Kompany atarudisha utawala wa Bayern Munich?

Katika Bundesliga utawala wa Bayern Munich ulitikiswa msimu uliopita baada ya kushuhudia wapinzani wao Bayer Leverkusen wakitawazwa kuwa mabingwa chini ya kocha Xabi Alonso. Kupepesuka kwa Bayern Munich kulizusha malumbano miongoni mwa mashabiki na viongozi. Baadhi ya viongozi wa klabu hiyo walimtuhumu wazi wazi aliyekuwa kocha wa wakati huo Thomas Tuchel kwa madai hakuna ubora alioongoza kwenye timu hiyo. 

Ikumbukwe Bayern Munich ilikuwa ikitamba kwa misimu saba mtawalia ikibeba taji la Bundelisga kadiri wanavyojisikia. Hata hivyo Xabi Alonso akawasambaratisha vibaya Bayern Munich msimu uliopita. Katika msimu huu 2024/2025 Bayern Munich wapo kileleni mwa BundesLiga. Bayern wana pointi 26 kutokana na michezo 10. 

Nafasi ya pili wapo RB Leipzig wenye pointi 21 wakifuatiwa na Eitratch Frankfurt (nafasi ya tatu kwa pointi 20), bingwa mtetezi Bayer Leverkusen ana pointi 17 yupo nafasi ya nne, huku Freiburg wakiwa namba 5 kwa pointi 17. Nafasi ya sita imekwenda kwa Union Berlin wakiwa na pointi 16, huku kigogo Borussia Dortmund wanashika nafasi ya saba wakiwa na pointi 16. 

Wakali wa soka wa zamani Werder Bremen wanashika nafasi ya 8 wakiwa na pointi 15, huku Mainz wana pointi 13 katika nafasi ya kumi na M’gladbach wanashikilia nafasi ya tisa wakiwa na pointi 14. Kimsingi Bayern Munich wanafukuzia ubingwa wao waliopokonywa na Leverkusen kisha Vinecent Kompany atafuta taji la kwanza akiwa kocha wa kigogo hicho cha Ujerumani. 

Katika Ligi ya mabingwa Ulaya Bayern Munich haikutamba chini ya Thomas Tuchel, lakini Vincent Kompany anatakiwa kurudisha makali hayo na ikiwezekana kutwaa taji la Ulaya. Siku zote Bsayern Munich hawashindwi kirahisi kutwaa taji la Bundesliga lakini changamoto yao ni dhamira ya kutamba barani Ulaya inavyoshindwa kutimia. Bayern Munich ni miongoni mwa vigogo wa soka barani Ulaya lakini haijaweka mizizi ya kutwaa mataji kwa wingi kama wenzao Real Madrid.

Shauku ya Wajerumani hao wa tamasha la Oktobafest wanatamani kuona timu yao ikiwa bingwa wa mara kwa mara katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini pia kurudisha makali wlaiyoporwa msimu uliopita ni kibarua ambacho kinatakiwa kufanywa na Vincent Kompany. Kwa hoja ya uzoefu wa kuijua Ligi ya Ujerumani, Kompany ni mtu sahihi kwa sababu amecheza akiwa mchezaji. Pia kwa kuifahamu Ligi ya Mabingwa Ulaya bado hajaweka mguu wenye dhahabu kwenye michuano hiyo kwa vile Bayern Munich imeshuhudia vipigo kutoka kwa wapinzani wao.

Jukumu zito alilonalo ni kuhakikisha anarudisha utawala wa Bayern Munich ambao ulichukuliwa na Leverkusen. Pia anatakiwa kuhakikisha anaing’arisha Bayern Munich kwenye mashindano ya Ulaya. Kwahiyo pande zote mbili  wanataka kutawala, na matumaini yao makubwa yapo kwa kocha kijana Vincent Kompany. Je anaweza kurudisha ufalme wa Bayern Munich katika BundesLiga? Je ataing’arisha timu hiyo kwenye mashindano ya Ulaya? Je ramani yake ya ushindi itambakiza Bayern Munich au atakuwa mhanga mwingine? Maswali ni mengi lakini itoshe kusema BundesLiga ni shamba darasa lingine katika mpira wa miguu.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Alifanya Mkwasa na Maximo, Gamondi anamalizia..

Tanzania Sports

Ni nani huyu kocha Abdihamid Moalin?