WAKATI Rais wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Alhaji Shaaban Mintanga akipanda kizimbani jana, bondia pekee aliyetarajiwa kushiriki michezo ya Olimpiki, Emilian Patrick ameondolewa.
Patrick, anashikiliwa kisiwani Mauritius akiwa na mwenzake, Petro Mtagwa na kocha wao, Nassoro Michael na Watanzania wengine watatu, wakihusishwa na dawa za kulevya aina ya heroine walizonaswa nazo mwezi uliopita.
Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), ilieleza jana kuwa Emilian ameachwa katika kikosi hicho kinachotarajiwa kwenda Beijing, China kutokana na kutokuwa na kuwa kizuizini akikabiliwa na kesi ya jinai.
Mintanga alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka mawili yanayomkabili ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Euphamia Mingi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Charles Kenyela alidai kuwa Mintanga na wenzake sita wanashtakiwa kwa kula njama na kusafirisha dawa hizo aina ya heroin zenye uzito wa kilo 4.8 na thamani ya Shilingi milioni 120 kutoka Tanzania kwenda Mauritius.
Alidai kuwa Juni 10 mwaka huu, mshtakiwa pamoja na wenzake hao walisafirisha dawa hizo kinyume na sheria, lakini Mintanga alipoulizwa mahakamani hapo jana alikana kuhusika na tuhuma hizo.
ACP Kenyela aliiambia mahakama hiyo kuwa upelelezi kuhusu kesi hiyo bado haujakamilika, na aliiomba isitoe dhamana kwa mshtakiwa kwa kuwa Sheria ya Kudhibiti Dawa za Kulevya hairuhusu mshtakiwa kupewa dhamana.
“Mheshimiwa hakimu napinga mshtakiwa kupewa dhamana kwa sababu sheria hairuhusu, pia mshtakiwa hatakiwi kupewa ikiwa thamani ya dawa inazidi Shilingi milioni 10,” alidai ACP Kenyela.
Hata hivyo, Wakili wa Mintanga, Jerome Msemwa alisimama na kudai kuwa mteja wake ana haki ya kupewa dhamana kwa kuwa hana hatia hadi mahakama itakapothibitisha.
“Mazingira hayaonyeshi ushahidi wa yeye kuhusika, na pia ni vema wahusika watuletee cheti chenye kuonyesha dawa hizo zina thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 10,” alidai wakili huyo.
Hata hivyo, mshtakiwa alinyimwa dhamana na kesi hiyo iliiahirishwa hadi Julai 16 mwaka huu.
Mintanga anadaiwa kufanikisha kuwasafirisha Case Ramadhan aliyejitambulisha kama meneja wa timu, Ally Msengwa (daktari) na Nathalia Eliya (kocha msaidizi).
Watuhumiwa hao walifuatana na mabondia Emillian Patrick, Petro Mtagwa na kocha Nassoro Michael waliokwenda Mauritius kushiriki michuano ya ubingwa wa Afrika.
Wakati huo huo, Sosthenes Nyoni anaripoti kuwa Tanzania haitakuwa na mwakilishi katika mchezo wa ngumi wakati wa michezo ya Olimpiki kutokana na mwakilishi wake, Emilian Patrick kuondolewa.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC), Filbert Bayi alisema uhamuzi wa kujitoa unatokana na kikao cha pamoja kati ya kamati hiyo, serikali na Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania(BFT) kilichoketi hivi karibuni kujadili juu ya uwakilishi kupitia ngumi.
Alisema kuwa kikao hicho kilifikia uamuzi huo baada ya kupitia kwa makini suala la kuendelea kushikiriwa kwa Emilian na kugundua kwamba bondia huyo hajafanya mazoezi kwa takribani mwezi mmoja mpaka sasa na hivyo kuwa na athari kubwa kwa maendeleo yake.
Bayi alisema kuwa baada ya kutolewa uamuzi huo kikao kilitoa maagizo kwa BFT kufanya mawasiliano na Shirikisho la Kimataifa la Ngumi za Ridhaa(AIBA) kuwatarifu juu ya uamuzi huo wa kujitoa.
Comments
Loading…