|
||||
RAIS Jakaya Kikwete amewataka wachezaji wa Taifa Stars kutobweteka na ushindi walioupata dhidi ya Sudan na kupata tiketi ya fainali za Afrika au kuogopa majina makubwa ya timu wanazokwenda kushindana nazo nchini Ivory Coast, badala yake waende wakifahamu kuwa wana changamoto ya kutakiwa kufanya vizuri katika fainali za Mataifa za wachezaji wa ligi za ndani (CHAN).
Akizungumza na wachezaji na makocha wao Ikulu, Dar es Salaam jana wakati wa chakula cha mchana alichowaandalia, Kikwete alisema wachezaji hao wamefikia kiwango kizuri cha kuitangaza soka ya Tanzania, lakini wafahamu bado wana safari ndefu ikiwamo ya kuhakikisha wanafanya vyema katika fainali za Mataifa ya Afrika yanayoanza baadaye mwezi huu.
Alisema wanachotakiwa kufahamu wachezaji hao ni kuwa mashindano hayo ni makubwa na kutokana na juhudi zao za kuingia fainali kwa kiasi kikubwa wamesafisha jina la Tanzania kisoka kwani ni takribani miaka 30, haikuweza kushiriki mashindano yoyote makubwa.
“Mmeonyesha mafundisho mliyoyapata kutoka kwa mwalimu wenu (Marcio Maximo) yamezaa matunda kwa kiasi kikubwa na sisi Watanzania tumepayaona na juhudi zenu zinaonekana kila siku…naamini tunaweza kufanya maajabu na mnatakiwa kujiamini kwani huu ndio wakati wenu wa kuonyesha uwezo na ujuzi mlioupata,”Alisema.
Aidha, alivitaka vyama vya michezo nchini hasa wizara husika kuwekeza katika michezo ili kufikia malengo na hasa kuinua vipaji kwa vijana waliopo mashuleni kwani wao ndio watakaoweza kuitangaza zaidi nchi kimichezo.
Pia, aliwashukuru wadhamini mbalimbali ambao wamekuwa bega kwa bega na timu hiyo hadi kufikia mafanikio iliyoyapata kwa sasa, lakini TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) nao wasibweteke kwani fedha zikiwamo wanazozipata katika viingilio vya michezo mbalimbali vitumike kuiendesha timu na kuiandalia michezo ya kujipima nguvu ili kupata uzoefu.
Comments
Loading…