Baada ya malalamiko yaliyotolewa na uongozi wa Simba kuhusiana na fedha walizokatwa ‘juu kwa juu’ na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufidia gharama za uharibifu wa viti kwenye Uwanja wa Taifa, shirikisho hilo halijawakata mabingwa watetezi Yanga kiasi cha Sh. milioni 5 wanachodaiwa kutokana na hasara iliyosababishwa na mashabiki wao baada ya nao kuharibu viti kwenye uwanja huo wa kisasa.
Mapema mwezi huu Simba ilikatwa Sh. milioni 5 kutoka kwenye mgao wao wa mechi ya Ligi Kuu ya Bara dhidi ya Kagera Sugar kulipia uharibifu uliofanywa na mashabiki wake wakati wa mchezo wao wa Kombe la Shirikisho uliofanyika Machi 4 dhidi ya Kiyovu kutoka Rwanda.
Lakini Yanga ambao walifanya vurugu katika mchezo wao wa Machi 10 dhidi ya Azam, hawajakatwa fedha zozote ikiwemo za mechi yao ya juzi dhidi ya African Lyon iliyofanyika kwenye uwanja huo huo unaomilikiwa na serikali.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alilaani kitendo cha TFF kuwakata fedha hizo na kudai kwamba wasiporejeshewa watasusia kuutumia uwanja huo pamoja na kuwashawishi mashabiki wake kutoingia uwanjani ikiwemo kwenda kuishangilia timu ya taifa (Taifa Stars) inapocheza uwanjani hapo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa, alisema kwamba wamepokea mgao wao wa mechi zote kama kawaida na hakuna makato yoyote ambayo tumeshakatwa.
Mwesigwa alisema, hata hivyo, walipokea jana asubuhi barua ya adhabu hiyo iliyowaangukia asubuhi na hivyo utekelezaji wake unafanyiwa kazi ya ofisi yake.
“Tumepokea mgawo wa mechi zote mbili kama kawaida, ila leo (jana) mchana ndio tumepokea barua hiyo ya adhabu ya uharibifu wa viti uliofanyika,” aliongeza Mwesigwa.
TFF kwa muda mrefu imekuwa na utaratibu wa kuzikata klabu fedha za faini au madeni mengine moja kwa moja kutoka kwenye mapato yao ya milangoni.
Yanga pia wanatakiwa kulipa faini ya Sh. milioni 4.5 kutokana na kadi nyekundu na vitendo vya vurugu vilivyofanywa na wachezaji wao wakati wa mechi dhidi ya Azam.
Wakati huo huo, Serikali kupitia kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imesema kuwa kuanzia sasa TFF itatakiwa kulipa faini ya Sh. milioni 10 kwa uharibifu utakaotokea kwenye Uwanja wa Taifa wakati wa mechi.
Akisoma taarifa iliyotolewa na waziri wa wizara hiyo, Emmanuel Nchimbi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo wa Wizara hiyo Leonard Thadeo alisema kuwa TFF imepewa taarifa hiyo ili ichukue hatua za kudhibiti vurugu zinazotokea uwanjani na kupelekea uharibifu wa viti uwanjani hapo.
“Lengo ni kuzuia uharibifu huu, Serikali inaitambua TFF kama msimamizi wa mpira wa miguu na ndio wanaoomba kutumia uwanja. Kuanzia sasa hawatalipa Sh. milioni 5 tena badala yake watalipishwa Sh. milioni 10 kwa ajili ya kugharamia uharibifu utakaotokea,” alisema Nchimbi katika taarifa hiyo iliyosoma na Thadeo.
Aidha alisema kuwa Serikali imeitaka TFF kukomesha mara moja vitendo vya vurugu vinavyotokea uwanjani hapo kabla Serikali haijachukua hatua.
Alisema kuwa Serikali haitasita kuufunga uwanja huo pindi uharibifu utakapotokea tena uwanjani hapo.
Comments
Loading…