Hatimaye Queen Park Rangers walioshuka daraja msimu uliopita wamefanikiwa kurejea Ligi Kuu ya England (EPL) baada ya kuwafunga Derby kwenye mechi ya mwisho ya mchujo katika Uwanja wa Wembley.
Alikuwa mkongwe Bobby Zamora aliyefunga bao hilo muhimu na la aina yake katika dakika ya 90 na kumpa faraja kocha wa siku nyingi, Harry Redknapp aliyeshuka na klabu hiyo, ambako alijiunga baada ya kufutwa kazi Tottenham Hotspur.
Zamora (33) anaonekana mtu mwenye bahati ya mabao muhimu, na matatu ya mwisho ameyafunga katika dakika ya 90 au baada ya hapo. Katika mechi hii alikuwa benchi hadi Redknapp alipomwingiza dakika ya 57. Bao lilitokana na mkwaju wake wa kwanza na wa pekee kwa timu nzima uliolenga goli.
QPR walimaliza wakiwa 10 baada ya mchezaji wao Gary O’Neil kupewa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya dhidi ya Johnny Russell.
QPR wanaungana na Leicester na Burnley kwenye EPL wakati Norwich, Fulham na Cardiff wameshuka kwenda ligi daraja la pili, maarufu kwa jina la Championships. Kocha Redknapp alisema hakutarajia iwapo timu yake ingeshinda mechi hiyo.
Klabu hiyo kwa kupanda daraja itapata pauni milioni 80 kutoka kwa wadhamini, hivyo wanatakiwa kujipanga juu ya nini cha kufanya kwenye usajili kuweza kukabiliana na timu zilizopo EPL.
Msimu uliopita walipata hasara ya pauni milioni 65.4, ambapo kabla ya kushuka daraja walisajili wachezaji wenye majina makubwa kama Loic Remy Loïc Remy kutoka Marseille, Chris Samba kutoka Anzhi Makhachkala, Jermaine Jenas na Andros Townsend kutoka Spurs.
Comments
Loading…