Hivi karibuni Mfuko wa Pensheni wa PSPF ulitoa semina kwa waheshimiwa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali.
Katika semina hiyo iliyofanyika katika Hotel ya Ramada, jijini Dar es Salaam, Meneja Mawasiliano, Masoko na Uenezi wa PSPF Costantina Martin alipata fursa ya kutoa mada juu ya PSPF.
Mada ya meneja huyo wa PSPF ilijikita katika maeneo yafuatayo; historia ya PSPF, wanachama wa PSPF, Mpango wa Uchangiaji wa Hiari, mpango wa lazima, mafao yatolewayo na PSPF.
Mikopo itolewayo na PSPF, kikokotoo cha mafao, uwekezaji, huduma kwa wateja, utunzaji wa kumbukumbu kwa wanachama, mafao yaliyolipwa kwa wastaafu, wastaafu na thamani ya Mfuko.
Baada ya mada hiyo waheshimiwa mabalozi walihamasika na uimara wa Mfuko na hatimaye wengi kujiunga na Mpango wa uchangiaji wa Hiari.
Kiwango cha uchangiaji katika mpango wa uchangiaji wa hiari ni kuanzia shilinghi 10,000/- au zaidi. Michango itawasilishwa moja kwa moja kupitia akaunti ya benki au wakala wa malipo wa M-Pesa, Tigo-Pesa, Airtel-Money au Maxmalipo.
PSPF ilianzisha mpango huu ili kuhakikisha kila mtanzania anafaidika na Hifadhi ya Jamii, PSPF kupitia mpango wake wa Uchangiaji wa Hiari tumeendelea kusajili watanzania na wasio watanzania ambao wanaishi nchini katika mpango huu.
Pia tunatoa huduma hii hata kwa watanzania wanaoishi nje ya Tanzania, lengo hapa ni kuhakikisha kila mtanzania anakuwa salama katika Hifadhi ya PSPF. Lengo la mpango huu ni kupanua wigo wa wanachama kwa kuandikisha wananchi waliojiajiri au kuajiriwa katika sekta rasmi na isiyo rasmi.