Kocha wa timu ya soka ya Taifa Stars, Jan Poulsen amesema kuwa majina ya wachezaji ama klabu kubwa havitasaidia katika utaratibu wake wa kuteua wachezaji wa kuunda timu ya taifa na mfano alishauonyesha nchini Algeria ambako aliwaacha nje nyota wote kutoka kwa mabingwa wa soka nchini, Simba.
Mdenmark huyo aliyechukua madaraka ya kuifundisha Stars kufuatia kumalizika kwa mkataba wa Mbrazil Marcio Maximo, alisema jana katika semina ya siku moja na waandishi wa habari za michezo kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa, ni viwango tu vitakavyowapa wachezaji tiketi ya kuchezea timu ya taifa.
Poulsen alisema daima amekuwa akiangalia umuhimu wa mechi katika kuchagua wachezaji wa kikosi cha kwanza na kwamba ataendelea na hali hiyo bila ya kujali jina la mchezaji wala klabu anayotokea.
“Sitapendelea mchezaji wala timu, huu ndio mfumo wangu wa kazi,” alisema.
Kocha huyo alisema katika ufundishaji wake, hupenda kutumia mfumo wa 4-5-1, ambao mara nyingine hunyambulishwa zaidi na kuwa 4-2-3-1.
Poulsen, ambaye leo anatarajiwa kukutana na wahariri wa habari za michezo katika semina kama ya jana yenye lengo la kuwaweka karibu wadau wa soka na menejimenti ya timu hiyo, alitumia fursa hiyo pia kuwataka mashabiki wa soka kuacha kuwapa mashinikizo wachezaji wa timu ya taifa kwani mambo hayo huchangia kushusha viwango vya wachezaji.
Alisema yeye kamwe hatakuwa akimwonyeshea kidole mchezaji mmoja pale inapotokea timu imeshindwa kufikia malengo kwa maelezo kuwa kama ni mafanikio ni ya timu mzima, na kama kushindwa ni timu mzima.
Baada ya kukaririwa mapema juzi akisema kuwa uwanja wa Jamhuri Morogoro ni mbaya unaowanyima fursa wachezaji kuonyesha uwezo wao ambao anahitaji kuufahamu katika kuteua timu, Poulsen, katika kikao hicho pia aliuponda Uwanja wa Mkwawani wa mjini Tanga kwamba haufai kwa kuwa na dimba la hovyo la kuchezea.
Wakati huo huo, Msemaji wa TFF, Florian Kaijage alisema jana kuwa ratiba ya Ligi Kuu imefanyiwa marekebisho mengine madogo, ambapo mechi baina ya African Lyon na Kagera Sugar iliyokuwa ichezwe Septemba 29 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, sasa itachezwa Jumanne Septemba 28 kwenye uwanja huo.
Comments
Loading…