*Wachukua kompyuta makao makuu
*Zico ajitokeza ili kumrithi Blatter
Uchunguzi juu ya mwenendo wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) katika kashfa nzito za rushwa unaendelea kwa kasi, ambapo polisi wa Uswisi wamezikamata kompyuta zenye taarifa nyeti juu ya yaliyojiri.
Askari hao walioanza uchunguzi wa mchakati wa kupata uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2018 na 2022 uliotolewa kwa Urusi na Qatar katika mtiririko huo, waliingia Makao Makuu ya Fifa, Zurich, kuzitaka kompyuta husika na maofisa wa Fifa wakawakabidhi.
Huko, walifanikiwa kunakili taarifa zote muhimu, ikiwa ni pamoja na zile za kutoka kwenye ofisi ya Sepp Blatter, rais aliyechaguliwa tena majuzi kwa muhula wa tano lakini siku nne baadaye akatangaza kwamba ataachia ngazi.
Taarifa hizo zinaweza kutoa mwelekeo mzuri wa awali juu ya mambo yatakavyokuwa kwa uenyeji wa fainali hizo mbili, lakini pia uwezekano wa Blatter, anayeshikilia urais huo kwa mwaka wa 17 sasa kuhusishwa na rushwa na hivyo kukamatwa.
Anatarajiwa kuachia ngazi Desemba mwaka huu, ambapo kuanzia sasa hadi wakati huo, anadai kwamba anasuka mipango ya mageuzi makubwa katika shirikisho hilo na soka kwa ujumla, ili mrithi wake acute mipango mizuri mezani.
Hata hivyo, wapo waliotabiri kwamba huenda akalazimishwa kuondoka ofisini mapema zaidi, kutegemeana na mwendelezo wa uchunguzi unaofanywa na Uswisi, lakini pia ule wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) ambalo limeshadaka maofisa saba wa Fifa na wengine saba kutoka nje ya shirikisho hilo.
Wanahusishwa na tuhuma za wizi wa fedha, rushwa na utakatishaji wa fedha, nyingi zikiwa na uhusiano na uenyeji wa mashindano au vitendo ambavyo Fifa au mashirikisho na nchi, waliona inabidi kulipiwa fedha.
Qatar wanaandamwa zaidi vibaya na matumizi ya hongo kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa Fifa uliowaidhinisha kuwa wenyeji,lakini pia maofisa wa Fifa, wakiwamo marais au viongozi wa mashirikisho ya soka ya mabara, likiwamo Afrika – Caf.
Polisi walichukua takwimu kwa njia ya teknolojia ya habari kutoka kwenye ofisi za Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke na Mkuu wa Masuala ya Fedha wa Fifa, Markus Kattner. Pamekuwa na madai kutoka kwa baadhi ya vigogo wa Fifa kwamba wao ndio walioitisha uchunguzi huo, lakini ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Uswisi inasema kwamba Fifa ndio majeruhi wenyewe.
Hatua hii imekuja muda mfupi tu baada ya Katibu Mkuu Valcke kusitisha zabuni kwa ajili ya mchakato wa kupata uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2026, akisema ingekuwa upuuzi kuendelea nao katika mazingira yaliyopo.
Urusi na Qatar zinakana kufanya lolote nje ya sheria na kanuni kutafuta na kupata uenyeji huo. Haya yanakuja pamoja na mengine, ambapo Afrika Kusini wanadaiwa kutoa pauni milioni 10 kwa Fifa ili kupata uenyeji wa 2010, ambao ilipata.
Hata hivyo, Afrika Kusini wanadai kwamba hizo zilikuwa fedha kwa ajili ya kuendeleza program za soka kwa Waafrika walioko Caribbean. Ufuatilizi wa fedha hizo unaonesha kwamba ziliingia kwenye akaunti ya Shirikisho la Soka la Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean (Concacaf) na kisha kuchukuliwa binafsi au kwa mkopo na aliyekuwa mkuu wake, Jack Warner.
Hata hivyo, Warner aliyedai kwamba Marekani wanaendesha uchunguzi huo kama kulipa kisasi kwa kukosa uenyeji wa fainali hizo, ameahidi kumwaga hadharani yote yaliyokuwa yakitokea Fifa, ikiwa ni pamoja na mlungula uliohusisha maofisa waandamizi.
Jamhuri ya Ireland wanadaiwa kulipwa euro milioni 10 na Fifa kama kuwaziba mdomo wasifungue kesi kupinga kukoseshwa kufuzu kwa fainali za 2010 pale Thierry Henry alipofunga bao akiwa ameshashika mpira na waamuzi wakaliruhusu.
Wakati hayo yakijiri, kiungo wa zamani wa Brazil, Zico, ambaye majina yake kamili ni Arthur Antunes Coimbra, 62, ametia nia ya kuwania nafasi ya Blatter uchaguzi utakapoitishwa Desemba mwaka huu.
Zico ambaye jina jingine ni ‘Pele Mweupe’ alizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari ulihudhuriwa na waandishi wengi, akasema ni jukumu lake kugombea ili kuongoza soka na kwamba mzozo wa rushwa ndani ya Fifa umemsikitisha sana.
“Inasikitisha kwa mchezo wetu huu kuona kinachotokea katika soka leo – rushwa …na kazi ngumu iliyofanywa na watu wengine wema imepotezwa bure – hivyo naona ni jukumu langu kutumia uzoefu na elimu kujaribu kuwania urais,” akasema.
Pamoja na kucheza na kuwa kocha kwenye nchi mbalimbali sehemu nyingi duniani, Zico ana uzoefu mdogo katika utawala wa soka katika ngazi ya juu. Anachukuliwa kuwa mmoja wa wanasoka mahiri katika historia ya Brazil na alicheza fainali tatu za Kombe la Dunia – 1978, 1982 na 1986.
Nyumbani kwao alitwaa mataji 12 akiwa na klabu ya Flamengo alikocheza tangu 1971 hadi 1983 kisha akaenda Udinese hadi 1985 akarudi Flemengo kisha akaenda Kashina Antlers 1991 hadi 1994.
Baada ya hapo alijitumbukiza kwenye ukocha, ikiwa ni pamoja na Japan, CSKA Moscow nchini Urusi na Fenerbahce huko Uturuki. Kwa sasa anawafundisha FC Goa iliyo Ligi Kuu ya India, akiwa kocha wake wa kwanza.